Wapiganaji wa Kiislamu waua 24 Algeria

Algiers, ALGERIA

WATU zaidi ya 24 nchini Algeria, wameuawa kutokana na shambulio lililofanywa na wapiganaji wa Kiislamu.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, miili ya watu hao ilikutwa kwenye dimbwi la damu.

Habari zinasema miili hiyo iligunduliwa na walinzi wa jadi wa eneo hilo.

Baba wa baadhi ya marehemu hao ambao ni mwanajeshi wa serikali, inasemekana kuwa, kwa muda wa siku mbili sasa (hadi kufikia jana), alikuwa hajulikani alipo.

Machafuko yaliyoanza Jumatatu iliyopita na kuendelea hadi sasa nchini Algeria, licha ya kuwepo kwa ulinzi mkali, mwanzoni yalisababisha vifo vya askari watatu na wengine miili yao haikuonekana.

Hata hivyo watu wengine kadhaa, waliripotiwa kujeruhiwa katika shambulio hilo la waasi.

2000 washambuliwa na kipindupindu

Kwazurunatal, AFIKA KUSINI

Ugonjwa wa kipindupindu uliolipuka kipindi cha mwezi Agosti mwaka huu nchini Afrika Kusini, unazidi kuenea licha ya juhudi zinazofanywa kuudhibiti na sasa umefikia Jimbo la KwazuluNatal.

Maofisa wa afya wa jimbo hilo wamesema kuwa ugonjwa huo tayari umekwisha sababisha 22 kupoteza maisha na wengine karibu 2036, kuathirika.

Waziri wa afya nchini Afrika Kusini, Manto Shabalala, alisema kuwa japokuwa kiwango cha vifo si cha kutisha sana, ameagizia mamlaka za afya kudhibiti ugonjwa huo.

Mtoto wa Chiluba ataka wanahabari wasimfuate

Lusaka, ZAMBIA

MTOTO wa Rais wa Zambia ameviomba vyombo vya habari viache kufuatilia mambo yake ya kifamilia.

Mtoto huyo wa Rais, Nicholous Chiluba, amesema kuwa katika tangazo lilochapishwa katika magazeti mbalimbali ya Lusaka kuwa, kila familia inakabiliwa na matatizo ya aina mbalimbali.

Alisisitiza kuwa hiyo isiwe sababu kwa jamii kuanza kujadili mambo ya familia yake.

Hatua hiyo imekuja baada ya vyombo vya habari mjini Lusaka kuripoti kuwa baba yake Nicholous, Fredrick Chiluba, amemhamisha mke wake kutoka nyumbani kwao, baada ya uvumi kuwa hakuwa mwaminifu.

Wakati huo huo: Zambia imekataa mkopo uliotolewa na benki ya dunia ili kusaidia vita dhidi ya ukimwi.

Kiasi cha dola bilioni 4 kimetengwa na benki hiyo kwa ajili ya nchi za Kusini mwa Afrika ambazo zambia ingegawiwa kiasi.

Waziri wa Afya wa Zambia, David Mpamba alisema nchi yake imekataa msaada huo kutokana na masharti kwamba pesa hizo zipelekwe kwenye taasisi za utafiti wa ukimwi na watoa ushauri nasaha.

Palestina na Israel zaanza mkutano

JERUSALEM, Israel

MKUTANO wa amani kati ya Israel na Palestina ulianza jana chini ya mkurugenzi wa idara ya upelelezi ya Marekani.

Mkutano huo ni dalili ya kuwepo ufanisi katika juhudi za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Koffi Annan kuingilia mgogoro huo binafsi.

Maafisa waandamizi wameeleza kuridhishwa kwao na hatua hiyo ya kupatanisha pande tatu za Israel, Palestina na Marekani na maofisa wa usalama kwenye kamati ya mwaka 1998.

Maafisa wanadai kwamba juzi Rais Bill Clinton alizungumza kwa muda wa nusu saa na Bw. Annan kwa ajili ya kutafuta mbinu za kutafuta maridhiano huko Mashariki ya Kati.