Make your own free website on Tripod.com

Polisi waokota maiti ya Kasisi Mkatoliki

KINGSTONE, Jamaica

JUMAPILI iliyopita, Polisi waliokota mwili wa Kasisi Mkatoliki katika eneo la Kusini mwa Jamaica ukiwa umetupwa pembezoni mwa barabara baada ya kufanyiwa mauaji.

Habari zinasema mauji hayo yalifanyika yapata umbali wa kilomita 50 kutoka mji mkuu wa Kingstone.

Inasadikiwa kuwa Kasisi huyo Mkatoliki, Haward Luther, aliuawa na majambazi ambao walitaka kupora gari lake.

Habari zinasema Padre huyo aliua wakati akiendesha gari lake ambapo watekaji nyara walimsimamisha kabla ya kumfyatulia risasi akiwa ndani ya gari lake.

Zinasema baada ya kumpiga kwa risasi na kumuua, majambazi hao waliutupa mwili wake pembezoni mwa barabara kuu iendayo Kingstone.

Padre huyo mwenye umri wa miaka 40, alikuwa ni kipenzi cha watu katika Parokia yake ya Mtakatifu Yosefu aliyokuwa anafanyia kazi hadi kifo chake.

Parokia hiyo ya Mtakatifu Yosefu ipo katika mji wa Spanish, Mashariki mwa mji mkuu Kingstone ambapo ni karibu kabisa na eneo yalipofanyika mauaji hayo.

Papa awataka wanamichezo kuchunguza dhamira zao

vatican

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, amewasisitiza wanamichezo na viongozi wao kuzichunguza dhamira zao ili iwe kiungo bora cha kudumisha mahusiano miongoni mwa jamii.

Aliyasema hayo wakati akiongoza ibada ya misa ya Jumapili iliyopita wakati akihitimisha Jubilei ya Michezo mjini Roma.

Baba Mtakatifu alisema wanamichezo hasa vijana katika karne hii, wanayo nafsi kubwa kuimarisha matumaini ya michezo kuwa kiungo muhimu katika kuletamahusiano bora baina ya mataifa na akatoa wito kwa dunia kuendeleza michezo ili kuhakikisha kuwa dunia inaendeleza uhusiano mzuri baina ya mataifa kwa njia ya michezo.

Jumla ya watu 70,000 walijumuika pamoja katika viwanja vya Olimpiki na kutoa salamu zao kwa Baba Mtakatifu kama ilivyo ada kwa viongozi wengine wakati wa mashindano makubwa ya michezo hususan mpira wa miguu.

Hii ni mara ya tatu kwa Baba Mtakatifu kuingia kwenye viwanja vya mpira mjini Roma, akisindikizwa kwa wimbo wa Zaburi huku bendera za mataifa mawili ya timu za mpira wa miguu zikipeperushwa angani.

Kundi la kwanza kufungua mashindano hayo lilikuwa ni la mashindano ya mbio za baiskeli kwa walemavu ambapo walikimbia umbali wa mita 200.

Wapo pia wachezaji nyota walionyakua medali za dhahabu mjini Sidney, Australia ambao walishiriki mashindano hayo.

Mchezo wa kwanza kuingia uwanjani ulikuwa ni kati ya Italia na timu ya wageni ambao walitoka bao 0-0.

Wakati huo huo: Kuna habari kuwa, Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, amezitaka pande zote mbili zinazopingana baina ya Waislael na Wapalestina, kukaa pamoja na kujadili mgogoro wa Mashariki ya Kati wa kusitisha vitendo vya utumiaji nguvu, baina ya pande hizo mbili.

Akizungumza na Balozi mpya wa Lebanon huko Vatican hivi karibuni, Baba Mtakatifu alisema kuwa anayo matumaini makubwa ya kutungwa kwa sheria za kimataifa zitakazo kuwa za kudunumu ili kuleta umoja baina ya Waislaeli na Wapalestina.

Alisema Vatican imekuwa ikifanya juhudi kubwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita, juu ya kuwepo kwa sheria za kudumu za kimataifa katika eneo zima la Mashariki ya Kati.

Ebola yazidi kuua Uganda

KAMPALA, Uganda

IDADI ya watu waliokufa kwa ugonjwa wa Ebola nchini Uganda, imezidi kuongezeka na kufikia watu 80 huku ukizidi kusambaa katika maeneo kadhaa nchini humo.

Tangu ugonjwa huo wa hatari ulipuke nchini Uganda mwezi uliopita, tayari watu wapata 250 wamekwisha ripotiwa kuathirika na kuna habari kuwa, Wizara ya Afya nchini humo imesema, watu117, wamekwisha tibiwa na kupata nafuu.

Ugonjwa Ebola kwa mara ya kwanza ulianza kulipuka katika mji wa Gulu, Kaskazini mwa nchi hiyo. Hivi karibuni mtu mmoja aliripotiwa kukumbwa na ugonjwa huo katika mji wa Mbarara.

Habari zaidi zinasema mmoja wa askari wa jeshi la nchi hiyo, alikumbwa na ugonjwa huo akiwa kambini baada ya kutembelea kambi ya Mbarari umbali wa takribani kilomita 425, Kusini mwa mji huo wa Gulu ulipolipuka ugonjwa huo kwa mara ya kwanza nchini humo.

Siku tano baada ya kuonekana dhahiri dalili za ugonjwa huo, askari huyo alifariki dunia.

Baadhi ya dalili za ugonjwa wa Ebola, ni pamoja na homa kali, kumwa tumbo, kuharisha na kutokwa damu kila sehemu yenye tundu katika mwili.

Wataalamu wa Shirika la Kimataifa la Afya (WHO), na Shirika la Centers for Disease Control la Atlanta, Marekani kwa muda upatao majuma mawili sasa, wamekuwa Gulu wakiisadia serikali ya Uganda kukabiliana na ugonjwa huo.

Watuhumiwa wawili wa mauaji ya Rwanda waachiwa huru

KIGALI, Rwanda.

WAKATOLIKI wawili ambao ni watuhumiwa wa mauaji nchini Rwanda wameachiwa huru na kufutiwa mashitaka ya mauaji na makosa ya kuvunja haki za binadamu.

Mahakama ya Rufaa ya Ruhengeli, imeamuru kuachiwa huru mara moja kwa watuhumiwa hao, Mchungaji Nzolye na Mchungaji Francis Kayeranga, waliokuwa wametuhumiwa kwa mauaji 1994.

Habari zinasema kuwa Mchungaji Nzolye na Mchungaji Kayiranga, waliruhusiwa kutoka gerezani Kigali wakiwa huru baada ya miaka miwili na nusu na walipokelewa getini na askofu wao.

Juni 15, Mahakama ya Rwanda ilitoa kibali cha kuwa huru, Askofu Augustine Misago ambaye alikuwa anatuhumiwa kwa makosa ya mauaji ya mwaka 1994.

Askofu Misago alikamatwa Aprili mwaka jana, na akawekwa gerezani kwa miezi 12 akisubiri kuhukumiwa licha ya afya yake kuwa mbovu.