Make your own free website on Tripod.com

Baba Mtakatifu aongoza mkutano, Jubilei ya Wamisionari

VATICAN

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, ameongoza mkutano mkuu wa wamisionari uliofanyika nchini Vatican na kuhudhuriwa na maelfu ya wamisionari ulimwenguni.

Mkutano huo Mkuu wa wamisionari ulifanyika Oktoba 18 hadi 21 mwaka huu.

Katika salamu zake, Jumapili iliyopita, Baba Mtakatifu alisema jumuiya yoyote ya watu, haiwezi kuishi bila ushuhuda wa wamisionari ambao kati yao, wapo waliotoa uhai kwa ajili ya Kristo.

Jumla ya Wakristo 70,000 waliokuwa wakiwakilisha mataifa 124 ya dunia, walikutana katika viwanja vya Mtakatifu Petro mjini Roma kuadhimisha Jubilei ya Wamisionari iliyofanyika jumapili hiyo ya Oktoba 22, mwaka huu.

Maadhimisho hayo yalitanguliwa na mkutano mkubwa wa wamisionari uliowakutanisha wawakilishi 1200 kutoka pande mbalimbali za dunia wakiwamo maaskofu 47, na zaidi ya mapadre 3000.

Maadhimisho ya Jubilei ya Wamisionari, yalianza asubuhi kwa nyimbo, ngoma na shamrashamra za kila namna kutoka katika mataifa mbalimbali huku bendera za mataifa hayo zikipeperuka kwa pamoja kama ishara ya umoja na mchanganyiko wa mataifa.

Wakati huo huo: Katika ibada hiyo ya mahujaji wa imani mjini Roma, Papa Yohane Paulo alisema katika mahubiri yake, alielezea maana na misingi ya umisionari katika Kanisa.

Alisema Kristo ndiye mfano mzuri kama mmisionari wa kwanza na akafupisha maelezo yake kwa kusisitiza nguzo kuu nne za umisionari.

Baba Mtakatifu alizitaja nguzo hizo kuwa ni huduma, umaskini, uvumilivu na msalaba.

Alitoa mfano wa Kristo mwenyewe kwamba hakuja duniani ili kutumikiwa bali kuwatumikia wengine na kutoa maisha yake kwa watu.

Alisema, "Kama mmisionari unatakiwa kutoa maisha yako kwa watu na kumtangaza Kristo katika misingi ya kanisa, kutoa muelekeo na njia kwa yule amtafutaye Kristo," alisema Baba Mtakatifu na kuongeza , "Kamwe hatuwezi kupoteza matumaini ya kuishi milele na wamisionari wanapaswa kuchangia kwa kiasi kikubwa, kizazi kipya cha umilelele kwa kuonesha njia inayofaa."

Aliwakumbusha wamisionari ambao kila siku bila ya msaada wowote wa kibinadamu, wamekuwa wakimtangaza Kristo na kuwa mashahidi wa upendo wa Kristo hata kupoteza uhai kwa ajili ya Kristo kama ilivyotokea hivi karibuni ambapo wamisionari watano kutoka nje waliuawa barani Afrika.

Wengine walioshiriki ibada hiyo ni baadhi ya makardinali, Rais wa Kamati ya Jubilei na maaskofu wengine 50, wakuu wa jumuiya za umisionari na mapadre 700.

Baba Mtakatifu alimalizia kwa kukumbushia maneno aliyozungumza miaka 20 iliyopita katika viwanja hivyo aliposema, "Msiogope, fungueni milango na mkamtangaze Kristo duniani kote."

Kisha, Baba Mtakatifu aliwateua wasaidizi wake12 kati ya wamisionari na kuwakabidhi msalaba na kuwatuma kutangaza Injili katika mabara yote ya ulimwengu huu.

Baadhi ya wamisionari walimkabidhi Baba Mtakatfu udongo kutoka katika mabara waliyoyawakilisha na kisha ulichanganywa na kutumika kupanda mti wa alizeti.

Askofu Mkuu ataka uchumi wa Kenya usitegemee misaada ya nje

NAIROBI, Kenya

ASKOFU Mkuu wa Nairobi, Raphael Ndingi Mwananzeki, amesema kuwa nchi ya Kenya kuendelea kutegemea misaada ya wafadhili ili kuinua uchumi wake, ni sawa na kitendawili kisicho na jibu.

Askofu Mkuu huyo aliyasema hayo hivi karibuni wakati akiongoza ibada ya shukurani kufuatia msamaha wa madeni uliotolewa kwa nchi maskini na Mfuko wa Kimataifa wa Fedha.

Ibada hiyo ilifanyika mapema mwezi huu katika Basilika ya Familia Takatifu

Kiongozi huyo alisema hatua ya kusamehe madeni kwa mataifa maskini, itawasaidia Wakenya endapo tu, serikali ya nchi hiyo itanuia kwa dhati kupambana kikamilifu na rushwa na kuunda upya mikakati thabiti ya kuinua uchumi.

Alisisitiza kuwa ingawa mambo yanaweza kuwa yanaonekana kwenda vizuri, haimaanishi kuwa sasa huu utakuwa mwisho wa matatizo ya Wakenya kiuchumi.

UNICEF, WHO yafungua vituo kupambana na UKIMWI Burundi

BUJUMBURA, Burundi,

SHIRIKA la kimataifa linaloshughulikia huduma za akinamama na watoto (UNICEF) na Shirika la kimataifa la Afya (WHO) yaliyoko nchini Burundi, yamefungua rasmi vituo vya kuelimisha jamii juu ya mbinu na umuhimu wa kupambana na janga la kimataifa la UKIMWI katika mkoa wa Gitega nchini Burundi.

Ugonjwa wa UKIMWI unaelezwa kuwa unaenea kwa kasi nchini humo ambapo sasa asilimia 20 ya wakazi wa mjini hapo, wanaelezwa kuwa na virusi vya ugonjwa huo hatari ambao mpaka sasa, haujapata kinga wala tiba.

Habari zinasema vituo hivyo vya kuelimisha raia jinsi ya kupambana na ukimwi, vimeanzishwa rasmi ili kuwahamasisha wakazi wa Gitega, waufahamu na wauchukie ugonjwa huu wa UKIMWI.

Mkoa huo ni miongoni mwa mikoa inayokaliwa na Watutsi na kuna uwezekano mkubwa wa kuambukizwa ugonjwa huo.

Mwakilishi Mkazi wa UNICEF katika nchi ya Burundi Bw. Mourisen alisisitiza umuhimu wa kuwapa watu mafunzo juu ya namna ya kupambana na UKIMWI pamoja na umaskini na kuacha uzinzi.

Polisi waopoa maiti 20 Ziwa Nyasa

 

BLANTYRE, Malawi

MAITI 20 waliokufa baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama katika Ziwa Nyasa, wameopolewa na Jeshi la Polisi nchini Malawi; limesema Jeshi hilo.

Kwa mujibu wa habari toka kwa msemaji wa Polisi, juhudi zaidi za kuwatafuta maiti wengine zilikuwa bado zinaendelea kwa vile waliohofiwa kufa niwengi kuliko idadi iliyokisiwa awali na kutolewa katika taarifa za awali.

Awali,ilitangazwa kuwa, watu 17 walikufa katika ajali hiyo ya hivi karibuni.

Msemaji huyo wa polisi alisema mpaka sasa idadi kamili ya watu waliopoteza maisha yao katika ajali hiyo iliyotokea wakati boti hiyo imezama upande wa Malawi katika Ziwa Nyasa, haijajulikana.

Watu hao walikuwa wakisafiri kwenda Chipoka.

Msemaji huyo amesema kuwa, jeshi lake halitasitisha zoezi la uopoaji wa maiti hao hadi hapo litakaporidhika kuwa hakuna maiti zaidi waliosalia ziwani.