Papa afichua siri kubwa iliyofichwa kwa miaka 80

lMapapa wawili waliotangulia waliisoma wakaificha kwenye chumba cha siri

VATICAN City,

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, amefichua siri nzito ya Kanisa iliyofichwa kwa zaidi ya miaka 83 na wakati huo huo, kuwatangaza kuwa Wenyeheri, watoto wachungaji Yasinta na Fransisko.

Sista Lucia, ambaye ni mtawa wa Shirika la Wakarmeli, akiandika juu ya siri tatu za Fatima ambazo mbili kati yake zilifunuliwa, alisema wakati akiandika katika usimulizi wake wa tatu Julai hadi Agosti, 1941 kuwa siri hiyo ya Fatima, ilizuiliwa hadi kibali kutoka mbinguni kitakapopatikana.

"Siri ya tatu sitaifumbua kwa sababu sijapata kibali kutoka mbinguni", alisema Sr. Lucia.

Tukio hilo lilitokea hivi karibuni wakati Papa alipotembelea Kanisa Kuu la Fatima, Ureno.

Sista Lucia hivi sasa ni mkongwe wa miaka 93. Aidha, sehemu ya kwanza ya siri inahusu moto wa milele na sehemu ya pili inahusu ibada kwa moyo safi wa Maria.

Sehemu hiyo ya kwanza ya moto wa milele, Lusia alieleza jinsi Bikira Maria alivyowaonesha watoto hao wa Fatima bahari kubwa ya moto .

Ilielezwa kuwa ndani ya bahari, yamo mashetani yaliyozama, na roho zenye sura kama watu zikiwa zimezama ndani ya bahari ya hiyo yamoto ....Ni roho bila uzito wala mzani wowote. Daima ni vilio vya hofu na mitweto ya mateso na kukata tamaa vinavyotawala......

Kufumba na kufumba tu, maono hayo yalifumbuliwa bada ya Bikira Maria kuwambia watoto hao kuwa

"Sasa mmeona moto wa milele ambamo roho za wakosefu maskini ndimo huenda .......Mungu anataka patengenezwe duniani ibada kwa moyo wangu safi. Iwapo haya niwaambiayo yatatimizwa, roho nyingi zitaokolewa na itakuwapo amani duniani.

Vita itakwisha (Hii inahusika na Vita ya Kwanza ya Dunia 1914-1918). Lakini ikiwa watu hawatakoma kumkosea Mungu, Vita mbaya zaidi kuliko hii itatokea wakati wa utawala wa Pio wa Kumi na moja.(Vita hii ni ya 1939-1945 lakini fujo hasa ilianza 1938)

Katika siri ya pili Bikira Maria aliwaambia watoto wa Fatima kuwa Mungu alitaka paanzishwe ibada kwa moyo safi wa Maria hapa duniani, na ya kwamba Bibi yetu angerudi tena kutaka nchi ya Urusi itolewe kwa moyo safi kwa kusudi la kuzuia vita isitokee mara nyingine.

Alitaka pia ifanyike Komunio ya malipizi Jumamosi ya kwanza ya kila mwezi.

Watoto hao pamoja na binamu yao Lusia ambaye yu hai na sasa ni mtawa wa Shirika la Wakarmeli walimuona Bikira Maria mara sita kati ya Mei 13 na Oktoba 13, 1917 mahali ambapo leo hii lipo basilika la Fatima.

Wakati wa matokeo hayo Fransisko alikuwa na umri wa miaka 9; Yasinta miaka 7 na Lusia miaka 10. Fransisko alikufa Aprili 4,1919 akiwa na miaka 11 na Yasinta alifariki Februari 20, 1920 akiwa na miaka 10. Wote wawili wamezikwa ndani ya basilika la Fatima.

Mwaka 1960,Papa Yohane wa 23 alifungua bahasha ya siri ya Fatima, sehemu ya tatu lakini aliamua asiwatangazie watu.

"Papa aliifungua bahasha, akayasoma yale yaliyomo," Kardinali Ottaviani alitoa habari mbele ya waandishi wa habari mjini Roma, Februari 11, 1967 na kuongeza, "Ingawaje habari iliandikwa kwa Kireno, alivyoniambia Papa, alifahamu kabisa kila kitu kilichoandikwa; kisha aliiweka katika bahasha mpya, akaifunga kwa muhuri (seal), akairudisha katika chumba cha nyaraka za siri".

"...Sasa ikiwa yeye aliyekabidhiwa hati ameamua kusema ya kwamba sasa sio wakati muafaka kuutangazia ulimwengu siri hiyo, basi turidhike na uamuzi wake wenye busara, kwamba siri iendelee tu kuwa siri," alisema Mwadhama Ottaviani.

Naye Papa Paulo wa sita aliisoma hati ya siri na kama mtangulizi wake Papa Yohane wa 23 alivyofanya, naye aliamua iendelee kubaki siri.

Lakini muda mfupi baadaye, Papa aligusia juu ya Fatima katika kikao cha Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatikano na alimtaja Bikira Maria kuwa Mama wa Kanisa na alifunga safari kwenda Fatima kusali na kuombea amani kwa ajili ya Kanisa na ulimwengu.

Akitangaza siri ya tatu baada ya Misa ya kuwatangaza Fransisko na Yasinta wenye heri, Muadhama Angelo kardinali Sodano, Waziri wa nchi wa Vatikan alisoma sehemu ya siri ya Fatima kwa Kireno.

Ifuatayo ni tafsiri ya matini;

"Tunapohitimisha maadhimisho ya ibada hii, kwa niaba ya wote waliopo hapa, ninapenda kumtakia matashi mema ya dhati mpendwa wetu Baba Mt. Yohane Paulo wa pili kwa sherehe za Jubilei ya miaka 80.

Aidha ninamshukuru kwa kazi muhimu ya kichungaji anayoitenda kwa manufaa ya Kanisa zima takatifu la Mungu".

Wakati wa ziara yake huko Fatima, Papa aniliagiza nitoe tangazo hili. Kama mjuavyo, nia ya ziara yake huko Fatima ni kuwatangaza wenye heri wachungaji hawa wadogo wawili".

"Hata hivi anapenda hija yake iwe alama mpya ya shukrani kwa Bikira Maria kwa ulinzi wake wakati wote wa kipindi chake cha upapa.

Ulinzi huu unaonekana kuhusiana na kitu kinachoitwa Sehemu ya Tatu ya Siri ya Fatima".

"Matini hii inayo maono ya kinabii mithili ya ile ipatikanayo katika Maandiko Matakatifu. Haielezi kinaganaga mambo ya baadaye bali inaunganisha (sanisi) na kufupisha mambo ikijiegemeza kwenye mazingira ya matukio sare yaliyotawanyika katika muda fulani kwa mfuatano na kipindi kisichoelezwa bayana. Hivyo matini hii haina budi kufafanuliwa kwa maelezo ya ishara".

"Matokeo ya Fatima yanahusu, zaidi ya yote, jinsi vita ilivyopigwa na mifumo ya mkanamungu dhidi ya kanisa na wakristo, na inaelezea pia mateso makubwa waliyopata mashahidi wa imani wa karne ya mwisho ya milenia ya pili. Ni njia ya Msalaba ya kufululiza iliyoongozwa na mapapa wa karne ya ishirini.

Katika kuelezea siri hiyo iliyokuwa imefichwa kwenye maono ya watoto hao ambao awali waliona kwa jinsi ya ajabu mtu mwenye mavazi meupe ya kiaskofu ambaye alipigwa risasi, kama ilivyomtokea Papa mwaka 1981 alisema:

"Kwa mujibu wa maelezo ya ‘watoto wachungaji’ ambayo yalithibitishwa hivi karibuni na Sista Lusia, Askofu aliyevikwa mavazi meupe anayesali kwa ajili ya waamini wote ni Papa (Yohane Paulo ll).

Kadiri alivyokuwa anajitahidi kuuendea msalaba kati ya maiti (maaskofu, mapadre, watawa wa kiume na wa kike na walei wengi) naye alianguka chini, kama mfu, kwa mlipuko wa mashambulizi ya mapigo ya bunduki".

"Baada ya jaribio la mauaji ya Mei 13, 1981, Papa aliona ni wazi kuwa mkono wa kimama ndio ulioongoza njia ya risasi na kumuwezesha Papa mfu kusimama mbele ya kizingiti cha mauti.

Wakati wa ziara ya aliyekuwa Askofu wa Leiria-Fatima huko Roma, Papa aliamua kumpa askofu huyo risasi iliyobaki kwenye gari baada ya jaribio la mauaji ili liwekwe madhahabuni huko Fatima.

Kwa amri ya askofu, risasi baadaye iliwekwa kwenye taji la sanamu ya Bikira Maria wa Fatima.

"Matukio ya mfuatano ya mwaka 1989 yalipelekea kuanguka kwa utawala wa Kikomunisti huko Urusi na nchi nyingi za Ulaya Mashariki ambazo zilikuza ukanajimungu. Kwa hilo nalo Papa anatoa shukrani zake za dhati kwa Mama Bikira Maria".

"Hata hivyo, katika sehemu nyingine za dunia mashambulio dhidi ya kanisa na wakristo, pamoja na mateso yanayoambatana nayo yanaendelea kwa huzuni kubwa".

"Hata kama matukio yanayorejewa katika shehemu ya tatu ya siri ya Fatima yanaonekana kuwa ya kale, lakini mwito wa Mama Bikira Maria wa kutaka mageuzi na toba uliotolewa mwanzoni mwa karne ya ishirini umebaki ni wa wakati muafaka na wa muhimu hivi leo". Bibi wa ujumbe anaonekana kusoma alama za nyakati - alama za nyakati zetu kwa ujuzi maalumu wa kina".

Mwito wa daima wa Maria mtakatifu sana wa toba ni dhihirisho la ushirika wake wa kimama kwa ajili ya majaliwa ya familia ya binadamu inayohitaji uongofu na msamaha.

"Ili waamini waupokee ujumbe wa Bikira Maria wa Fatima vizuri zaidi, Baba Mtakatifu ameagiza idara ya Kanuni ya Imani iwatangazie watu sehemu hii ya tatu ya siri baada ya maandalizi ya fasiri ya kufaa".

"Tumshukuru Bikira Maria wa Fatima kwa ulinzi wake. Kwa maombezi yake tuliaminishe Kanisa kwa milenia ya Tatu".

"Tunakimbilia ulinzi wako, Mzazi Mtakatifu wa Mungu".

"Uliombee Kanisa la Mungu. Umuombee Baba mtakatifu Yohane Paulo wa Pili! Amen", ujumbe huu unamaliza.