Make your own free website on Tripod.com

Rais Kabila kurejesha mamlaka ya Bunge

Kinshasa, DRC

RAIS Laurent Kabila wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC ametangaza kurejesha mamlaka ya Bunge nchini humo ifikapo Julai 1 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Rais Kabila ambaye nchi yake imekuwa katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka mitatu mfululizo sasa Bunge hilo litakuwa na wabunge wapato 300.

Hatua hiyo ya Rais Kabila, imeelezwa kuwa ni yenye lengo la kufanikisha mpango uliokwama wa muda mrefu wa kutejesha demokrasia nchini humo.

Rais Kabila katika hotuba yake iliyochukua zaidi ya saa tatu mwishoni mwa wiki alisema atatumia nguvu zake zote kuhakikisha kwamba Bunge hilo linaundwa Julai1 kama alivyokusudia.

Nchi hiyo imekaa bila kuwa na Bunge tangu Rais Laurent Kabila alipompindua Rais wa Zamani wa nchi hio Bw. Mobutu Seseseko mwaka 1997.

Katika hotuba yake, Kabila alisema bunge hilo litaundwa bila kufanya mjadala wa Kitaifa kwa sababu za kiusalama.

Wakati huo huo: Serikali ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, imepiga marufuku uuzwaji wa vitenge kutoka nchini China.

Taarifa ya Serikali hiyo iliyotolewa mwishoni mwa wiki imesema kuwa Kongo imechukua hatua hiyo kwa vile nchi hiyo inavyo viwanda vyake ambavyo vinazalisha bidhaa hiyo.

Imeelezwa kuwa vitenge vya China vimekuwa vikiuzwa kwa bei ya chini kuliko vile vya Zaire na ndiyo maana kulinda viwanda vyake.

Hata hivyo wachumi nchini humo wamesema viwanda vya nchi hiyo havina uwezo wa kukidhi mahitaji ya soko la vitenge nchini humo.

Wabunge wa Upinzani Kenya waiweka Serikali kwenye kona

Nairobi, Kenya

WABUNGE wa Bunge la Kenya, mwishoni mwa wiki walipitisha muswada wa Sheria ambao unataka kila mbunge wa bunge hilo lenye wabunge zaidi ya 70 apewe Bastola.

Muswada huo ambao ulipitishwa kwa shinikizo kubwa la wabunge wa upunzani ambao walikuwa wengi bungeni huku wakiungwa mkono na baadhi ya wabunge wa chama tawala. Wapinzani walikuwa 41 wakati wale wa chama tawala cha KANU walikuwa 33 tu.

Zaidi ya kila Mbunge kapewa bastola kupitishwa kwa muswada huo pia kunampa haki kila Mbunge wa nchi hiyo kupata hati ya kusafiria ya kibalozi na dereva.

Makamu wa Rais Profesa George Saitoti, alionyesha kuwa Serikali ya Kenya haikupendelea kupitishwa kwa muswada huo.

Alipoona mambo yanaiendea kombo serikali alimwomba Spika wa Bunge Bw. Gitobu Imanyara asimamishe shughuli za Bunge walau kwa dakika tano ili wabunge waweze kutafakari zaidi lakini hata hivyo hatua hiyo haikusaidia kitu.

Mbali ya Profesa Saitoti Mawaziri wengine Bw. Marden Madoka, Bw. Andrew Kiption na Dk. Bonaya Godana nao walifanya jitihada za kuwashawishi wabunge wasipitishwe muswada huo lakini wakaambulia kuzomewa na hoja zao kupuuzwa.

Baada ya kupita kwa hoja hiyo kwa njia ya kupiga kura wabunge wa upinzani walitoka nje wakiwa na furaha na kuanza kupongezana kwa ushindi huo.

Bomba la mafuta lahujumiwa Sudan

Khatoum, Sudan

Bomba linalosafirisha mafuta ambayo hayajasafishwa hadi bandari ya Red Sea

lililipuliwa mapema wiki hii na Beja Congress, washirika wenye silaha wa National Democratic Alliance, televisheni ya serikali hiyo ilitangaza.

Katibu Mkuu wa wizara ya Kazi na Madini alinukuliwa akisema

bomba hilo la kutoa mafuta nje huko Singat, kiasi cha kilomita 345 mashariki

mwa Khartoum, "limefanyiwa kitendo cha hujuma."

Runinga hiyo ya serikali ilisema uuzaji wa mafuta nje hautaathiriwa kwa sababu ya akiba kubwa ya mafuta iliyopo katika Bandari ya Bashir, Red Sea.

Msemaji kwa niaba ya kampuni ya mafuta ya Kanada, Talisman Energy Inc. alisema bomba hilo litarekebishwa katika muda wa siku tatu, Reuters liliripoti.

Kumekuwa na malalamishi makali kuhusu shughuli za kampuni hiyo huko Sudan. Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu (Amnesty International) juma hili lilieleza wasiwasi kuhusu kile linachokiita "bei ya kibinadamu ya mafuta" huko Sudan, likisema ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unafanywa na serikali, wanamgambo, washirika wa serikali na makundi ya upinzani yenye silaha wanaotafuta mafuta.

Wakati huo huo: Katibu-Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan amefurahishwa na tangazo la serikali ya Sudan la kusitisha mapigano kwa sababu za kibinadamu hadi 15,Julai mwaka huu.