Ushauri mbaya wa madaktari waua wengi zaidi ya ajali Ujerumani

MAELEKEZO mabaya ya matumizi ya madawa yaliyotolewa na madaktari nchini Ujerumani mwaka jana yaliua watu wengi zaidi ya wale waliokufa kwa ajili za barabarani.

Gazeti moja lilolewalo nchini humo Sluttgarter Nachrichten limeripoti kuwa watu wapatao 25,000 walipoteza maisha katika mwaka huo kutokana na maelekezo potofu ya matumizi ya madawa yaliyotolewa na madaktari.

Kwa mujibu wa toleo la hivi karibuni la gazeti hilo idadi hiyo ya vifo ni mara tatu zaidi ya ile ya ajali za barabarani.

Sababu ya kutokea kwa makosa hayo imeelezwa kuwa ni ujuzi na uzoefu mdogo walio nao madaktari juu ya athari za baadhi ya madawa yanapotumiwa vibaya.

Mtaalamu mmoja wa madawa Bw. Ingolf Cascorbi alikaririwa akisema kuwa angalau vifo 10,000 na matukio 250,000 ya watu walioathiriwa vibaya na madawa nchini humo vingeweza kuepukwa endapo ujuzi na uzoefu wa kutosha ungetumika.

Kadhalika jarida jingine nchini Ufaransa nalo lilikaririwa lilikaririwa likisema kuwa uchunguzi wa kisayansi wa hivi karibuni umebaini kuwa miongoni mwa maelekezo 150,000 ya dawa yaliyotolewa na madaktari nchini humo kwa watu wenye umri unaozidi miaka 70 pekee maelekezo yapatayo 10,700 ama yalikuwa yenye makosa au hayakuzaa matunda kabisa.

Gazeti hilo Sciences et avenir limeripoti kuwa elekezo moja kati ya hamsini yalikuwa ya hatari sana na yenye madhara makubwa.

Nchini Ufaransa limeripoti gazeti hilo kuwa wazee hulazwa hospitalini kwa wastani wa siku milioni moja kwa mwaka kutokana na athari zitokanazo na maelekezo mabaya ya matumizi ya madawa.

Balaa! Katika kila vifo vitano nchini Rwanda vinne ni vya Ukimwi

Kigali, Rwanda

WASTANI wa vifo vinne kati ya kila vifo vitano vinavyotokea nchini Rwanda, kimoja kinatokana na Ukiwmi, imeelezwa.

Waziri wa Afya wa Rwanda, ambayo ina raia kati ya milioni saba na nane, alisema katika mkutano mmoja uliohusu mapambano dhidi ya Ukimwi kuwa watu wapatao 500,000 wamekwishaambukizwa virusi vya ugonjwa huo nchini humo na maambukizo yanaendelea kwa kasi katika kiwango cha kutishia hata usalama. Mkutano huo ulihudhuriwa na ajumbe kutoka nchi za Rwanda, Burundi na Uganda.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la habari la Rwanda (RNA), Wanyarwanda wapatao 180,000 wanaugua ugonjwa huo wakati 150,000 wameshakufa.

Takwimu zinasema watu 500,000 wameshaambukizwa, kiwango ambacho kinakadiriwa kuwa asilimia 6 ya Wanyarwanda wote.

Jumapili iliyopita,Marekani ilionya kwamba Ukimwi unaenea kwa kasi ya kutisha katika baadhi ya nchi za Afrika kiasi ambacho inahofiwa kwamba zitasababisha kushuka kwa uchumi, kuhatarisha majeshi ya kigeni na kusababisha matatizo mengine.

Askari wa Umoja wa Mataifa wauawa Sierra Leone

IRIN, Afrika Magharibi

ASKARI wanne wa majeshi ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani nchini Sierra Leone hawajulikani walipo na wanahofiwa kuuawa, wakati wengine wanane wamejeruhiwa.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Marie Okabe, alisema mwishoni mwa wiki mjini New York kuwa, askari wengine 69 wamewekwa kizuizini, 39 katika eneo la Kaskazini la Makeni na 30 Kailahun upande wa mashariki.

Kadhalika kundi jingine la wanaume 23-lilizingirwa huko Kuiva, karibu na Kailahun, aliongeza Okabe.

Watunza amani wanne wanaohofiwa kuwa ni kutoka katika vikosi vya Kenya vilivyopelekwa huko Sierra Leone kwa ajili ya kutunza amani katika mpango maalum wa Umoja wa Mataifa.

Askari hao walitoweka wakati wanachama wa kundi la Revolutionary United Front (RUF) kuvamia majeshi ya Umoja wa Mataifa huko Makeni na Kailahum.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa mwishoni mwa wiki mjini New York, umoja huo sasa una wanajeshi 8,700 nchini Sierra Leone kati ya 11,000 walioidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja huo kwa ajili ya kutekeleza Makubaliano ya Amani ya Lome, yaliyowekwa Julai, 1999 kati ya serikali na waasi wa RUF kumaliza vita miongoni mwao vilivyodumu kwa miaka minane sasa.

Jumatano iliyopita Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan alisema katika mkutano wa waandishi wa habari kuwa: "Nimevunja moyo na mwenendo wa (kiongozi wa RUF) Foday Sankoh na RUF.

Nawasiliana viongozi wengi nchi katika eneo ambao wanaweza kutumwa wajumbe kuongea naye."

Sankoh alifanya mazungumzo Jumatano iliyopita na Mshauri wa masuala ya Usalala wa Nigeria Jenerali Mohamed Alieu Mohamed, ambapo aliahidi kuwaachia mateka wote waliotekwa na RUF katika maeneo ya Kailahun, Makeni na Magburaka.

Sankoh pia aliahidi "kuendelea na mazungumzo ya amani" na kuwaamuru watekaji kuiachia helkopta waliyoishikilia iondoke kurejea mji wa Freetown.

Kofi Annan alisema tabia ya Sankoh na vikosi vyake " inaharibu mazingira mazuri ya jitihada za kurejesha amani kwenye bara la Afrika na hata inapaka matope hatua na makusudi ya Umoja wa Mataifa kupeleka majeshi nchi Kongo.