Make your own free website on Tripod.com

Mwanamke Myahudi aeleza Papa alivyomuokoa

lAlimtorosha toka kambi ya mauaji ya Hitla na kumbeba mgongoni kwa kilomita nne

JERUSALEMU (ZENIT)

ALHAMISI iliyopita haitasahauliwa kamwe na Edith Zirer, mwanamke wa Kiyahudi aliyezaliwa nchini Poland, anakotokea Karol Wojtila(Papa Yoahane Paulo ll) ambaye alimwokoa na mauti miaka 55 iliyopita.

Wakati ule, Edith Zirer, anasema: "Nakumbuka vizuri. Nilikuwa pale, nikiwa msichana mdogo wa miaka 13, peke yangu, mgonjwa na dhaifu. Nilikuwa nimekaa katika kambi iliyolindwa sana ya Wajerumani katika hali ya kufa. Na kama malaika,Karol Wojtila, aliokoa maisha yangu; kama njozi ya mbinguni: akanipa kinywaji na chakula, kisha akanibeba mgongoni mwake umbali wa kilomita 4 akitembea juu ya barafu hadi tulipopanda gari moja na kuokoka."

Huo ulikuwa wakati wa mauaji yaliyofanywa na Dikteta Adolf Hitla, dhidi ya mamilioni ya Wayahudi mwaka 1945, ambapo yeye pekee alipona katika familia yake yote.

Edith ambaye hivi sasa ana umri wa miaka 66, ana watoto wawili na anaishi mjini Haifa, Israeli.

Ushuhuda huo mwema ulitolewa na mwanamke huyo wa Kiyahudi Alhamisi iliyopita wakati alipohudhuria katika ziara ya Papa nchini Israeli, ambako alikwenda kuhiji.

Wakati huo huo: Ibada ya Misa ya Papa Jumatano iliyopita mjini Bethlehemu, iligongana kwa muda na adhana ya Waislamu kiasi cha kumfanya Papa atulie kwa muda kabla ya misa kuendelea.

Papa alisema anamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kumpa frursa ya kutembelea eneo hilo takatifu, ambalo amekuwa mwenyeji wake wa muda mrefu kupitia Biblia.

Kiama kidogo chatua Afrika Kusini,vifo milioni 8

Durban, Afrika Kusini

KIFO cha mtu mmoja tu hata katika familia iliyo kubwa zaidi, huweza kuleta majonzi ya kutosha kuwakosesha amani wana familia, ndugu na marafiki.

Ebu fikiria juu ya vifo vipatavyo milioni nane katika nchi moja!

Ni hali ya kutisha lakini ni ndiyo hali inaotarajiwa kuikumba Afrika ya Kusini katika kipindi cha miaka 10 tu ijayo kutokana na ugonjwa usio na tiba wala kinga-Ukimwi.

Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Kamati ya maandalizi ya Mkutano wa 13 wa Kimataifa juu ya Ukimwi ,imesema katika kipindi hicho watoto wapatao milioni 15 watazaliwa nchini humo, lakini milioni 3.25 kati yao watakufa mapema kutokana na maambukizo ya Ukimwi.

Afrika ya Kusini inakuwa mnara wa kuonyesha hali

mbaya inayozikabili nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara.

Profesa Coovadia, anayeshiriki maandalizi ya mkutano huo alisema hiyo inaonyesha ni kwa kiasi gani jumuia ya kimataifa inadaiwa kufanya jambo fulani kuokoa maisha ya watu.

Profesa huyo anaamini kuwa watu wote duniani wanapaswa kuunganisha nguvu na kujisikia wenye wajibu wa kupambana na ugonjwa huo na kutumia ujuzi na uwezo wa kisayansi kuupatia ufumbuzi wa tiba ugonjwa huo.

Mkutano huo unatarajiwa kufanyika Julai, 2000.

Papa rafiki wa Waislamu,Wayahudi

ROMA, ITALIA,

ZIARA ya Papa Yohane Paulo ll huko Mashariki ya kati imeelezewa kuwa ya manufaa makubwa kwani imedhihirisha kwamba kweli Papa ni rafiki wa Wayahudi na Waislamu.

Taarifa ya Shirika la Habari la ZENIT iliyomkariri Mtaalamu mmoja wa Mazungumzo kati ya Wakristo na Waislamu, Padri Thomas Michael, imesema, "ziara ya Papa haina kiwingu. Hakwenda huko kama kiongozi wa kisiasa kuongea na kujadili, bali kuhiji."

"Lakini hii haimaanishi kwamba ziara yake haitakuwa na umuhimu katika masuala ya mazungumzo ya amani katika Mashariki ya Kati; kinyume chake inatarajiwa kuwa itaimarisha matumanini kwamba kwa ziara hiyo Papa ataweza kujenga mahusiano mazuri zaidi miongoni mwa dini mbali mbali." imesema taarifa.

Padre Michael, amesema inashangaza kuona kuwa Wayahudi na Wapalestina wanataka amani, lakini wanaogopana. Hivyo ziara hii ya Askofu wa Roma ni ya muhimu kwa ajili ya mahusiano ya jamii hizo mbili.

"Heshima aliyo nayo kwa Wayahudi na Waislamu ina nafasi kubwa ya kuwaondolea uhasama," alisema.

Papa Yohane Paulo ll, alianza ziara yake huko Mashariki ya kati mwanzoni mwa wiki, ambapo pia ametembelea maeneo matakatifu katika historia ya Biblia.