Make your own free website on Tripod.com

Maaskofu wazungumzia mafuriko ya Msumbiji

lPapa ayaita ya aina yake

Preptoria, Afrika Kusini

MAASKOFU wa Kanisa Katoliki eneo la Kusini mwa Afrika wametaka wahanga wa Mafuriko nchini Msumbiji wasaidiwe kwa hali na mali ili kuwawezesha kurejelea hali waliyokuwa nayo kabla ya kukumbwa na pigo la mafuriko hayo.

Wito wa Maaskofu hao wameutoa Marchi 7 mwaka huu mjini Preptoria kwa vyombo vya habari ambapo wamefikisha ujumbe wao wa salama za rambirambi kwa ndugu na jamaa za waliopoteza maisha kwenye mafuriko hayo na wakaeleza kuwa wanaungana nao katika kuviomboleza vifo hivyo.

Taarifa ya Maaskofu hao imeelezea kuwa mafuriko hayo mabaya pengine kupita mengine yote yaliyopata kutokea barani Afrika katika kipindi cha miaka 100 yamekatisha maisha ya mamia ya watu huku yakiacha mamia ya maelfu wakiwa hawana makazi na chakula huku wakikabiliwa na hatari ya njaa na magonjwa ya kuambukiza.

Awali kabla Maaskofu hao wa nchi za Kusini mwa Afrika hawajatoa kauli kama hiyo kwa vyombo vya habari, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Yohane Paulo wa Pili, aliyataja mafuriko hayo kuwa ni mabaya kupita mengine yaliyopata kutokea.

Maaskofu hao wamewataka Wakristo wote kote Duniani katika mwaka huu wa Jubilei wa furaha na tumaini kuwaombea kwa bidii wahanga wa mafuriko ya Msumbiji ili Mungu aweze kuwasaidia kurejelea maisha mema.

Pamoja na kutoa shukrani zao za dhati kwa nchi wahisani na mashirika ya Kimataifa ya kutoa misaada yanayoendelea kutoa huduma kwa watu walioathiriwa na mafuriko nchini Msumbiji. Maaskofu hao pia wametaka watu popote pale walipo kutoa msaada wa hali na mali ili hicho walichonacho wake na kaka na dada zetu wa Msumbiji katika kipindi hiki kigumu.

Wakati watu walioathiriwa na mafuriko hayo sasa wameanza kurejea majumbani mwao ili kujenga makazi yao upya, Maaskofu hao wamefungua mfuko maalum wa kusaidia waathirika ambapo fedha zote zitapelekwa jengo la 'Khanya House' lililoko mtaa wa Visagie, jijini Preptoria.

Tukio la Mafuriko ya Msumbiji liliandama na miujiza kadhaa ambapo mama mmoja mjamzito aliweza kujifungua mtoto wa kike salama juu ya mti aliokokwea ili kuyanusuru maisha yake.

Mama wa mtoto huyo ambaye tayari ambaye amepewa jina la Marina, amekuwa gumzo kwenye vyombo vya habari kote duniani ambapo ametoa wito kuwa anachohitaji kwa sasa ni Blanketi na chakula tu kwa ajili ya kumsetiri yeye na mwanaye.

Mafuriko ya Msumbiji pia yameleta hatari nyingine ya kufukua mabomu ya ardhini yaliyokuwa yamefukiwa chini. mabomu hayo yaliyofukuliwa na maji ambayo sasa yametapakaa nje yameleta hatari kubwa kiasi cha kuwapelekea raia wanaotembea sehemu mbalimbali hususani mashambani wasijiamini kwa kuhofiwa kulipuliwa.

Msumbiji ambayo ilikuwa iko kwenye kipindi cha kupona kiuchumi baada ya vita vya miaka mingi kati ya Magaidi wa MNR na chama cha FRELIMO, mafuriko hayo yameathiri uoto wa mazao na kuleta hatari kubwa ya njaa na kupoteza ndoto ya kupata mavuno mengi kama yalivyopatikana 1999.

Waislamu wampiga mawe shetani

Mecca, Saudi Arabia,

WAISLAMU wapatao milioni 2.7 wiki iliyopita walifurika mjini Makka, Saudia Arabia katika kutimiza moja kati ya nguzo tano za dini ya Kiislamu ya kufanya hija, mjini hapo.

Kati ya Waislamu hao waliohudhuria hija mwaka huu, wastani wa 400,000 ni wenyeji wa Saidi Arabia, wakati milioni 2.3 wanatoka maeneo mbali mbali duniani.

Habari kutoka mjini Makka, zinasema hadi mwishoni mwa wiki hija ilikuwa shwari na hapakuwa na matatizo yoyote.

Mapema Waislamu hao walitimiza moja ya desturi za hija yao kwa kila mmoja kurusha mawe saba kama ishara ya kumpiga shetani.

Kufanya hija mjini Makka ambako kuna jiwe jeusi linaloheshimiwa na Waislamu liitwalo Kaaba ni moja kati ya mambo muhimu katika ibada ambayo kila Muislamu mwenye uwezo anapaswa kufanya.

Kadhalika katika hija hiyo Waislamu huchinja maelfu ya ngamia na wanyama wengine kama ishara ya kukumbuka wakati ambao Nabii Ibrahimu aliagizwa na Mwenyezi Mungu kumchinja mwanawe Ishaq (Isaka) kuwa dhabihu.Wakati wa kilele cha Sikukuu hiyo yaani Id-El- Haj, Waislamu wote ambao hawakuweza kufika katika hija huko Makka, hutakiwa pia kuchinja wanyama.