Biblia yenye maudhui ya Kiafrika yachapishwa nchini Kenya

Na Aana, Nairobi Kenya

BIBLIA ambayo ni maalumu kwa Waafrika na Makanisa ya Kiafrika tu imechapishwa mjini Nairobi Kenya hivi karibuni, ambapo nakala zake zimeishaanza kusambazwa.

Shirika la habari la 'All Africa News Agency' lililoko chini ya Kanisa Katoliki limeelezea kwenye taarifa yake kuwa Biblia hiyo mpya imechapishwa na shirika la Watawa la Paulines Publications Africa , la jijini Nairobi, Kenya na itakuwa ikiuzwa kwa bei ya dola 10 za Kimarekani kwa kila nakala.

Biblia hiyo mpya ya Kiafrika imetoa kipaumbele kwa baadhi ya mila na tamaduni za kiafrika kusudi ipate kuwafikishia injili kwa urahisi na kuwaweka Waafrika wa ngazi ya chini karibu na Injili ya Bwana zaidi.

Biblia hiyo ambayo kwa lugha ya kimombo inaitwa 'The African Bible' imepitishwa na Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Kenya, inazo kurasa zipatazo 2,147 na inayo dibaji, maoni, rejea na michoro inayowaweka Waafrika karibu na Yesu kiasi cha kupelekea waonane naye kiroho hapa hapa Afrika.

Biblia ambayo imetokana na ile ya 'New American Bible' utayarishaji wake ulifanikiwa kwa kazi ya wanazuoni na tena wanathiolojia wapatao 30 ambao miongoni mwao walikuwemo Waafrika na Wazungu.

Kazi ya utafiti wa Biblia hii mpya na uhariri wake kabla ya kuchapishwa ilifanywa na Bw. Victor Zinkuratire na Bw. Angelo Colacrai, ambao licha ya kusimamia utafiti wake walikuwa ndio Wahariri wakuu.

Sehemu ya dibaji, utangulizi na rejea za maoni, zote zimetiwa saini na Askofu John Njue, ambaye ndiye ni Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Kenya.

Kwenye maelezo yake katika dibaji ya Biblia hiyo Mtawa wa Kanisa Katoliki nchini Kenya Sr. Teresa Marcazzan, anaelezea kuwa chapisho hilo jipya la Biblia ya Kiafrika imetokana na changamoto aliyoitoa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Yohane Paulo wa pili wakati alipozindua Uinjilisti mpya wa Milenia ya tatu kunako mwaka 1994.

Mtawa huyo amenukuu kauli ya Papa aliyoitoa wakati wa uzinduzi huo wa uinjilisti mpya kwa Millenium ya tatu ambapo alielezea kuwa.

"Ili kuwezesha neno la Mungu kusambaa, jitihada lazima ziongezwe katika kuweza kuwawezesha waumini kuelewa aina tofauti za maandiko ama kwa tafsiri nzima za Biblia ama sehemu yake"

Papa alielezea kuwa hilo litawezekana tu kwa ushirikiano na Makanisa jamii ya wahubiri pamoja na machapisho ya miongozo ya maombi ya kusaidia jamii na familia kuyajua maandiko.

Mtawa Sr. Marcazzan ameeelezea kuwa katika Biblia hii mpya ya Kiafrika michoro iliyotumiwa na watu walioitayarisha ni ile inayowezesha Msomaji kufahamu kwa urahisi mazingira ya kihistoria na Kijiografia ya sehemu husika inayozungumziwa ndani ya Biblia hiyo.

Katika kauli yake ya maoni kuhusu kutolewa kwa chapisho la Biblia mpya ya Kiafrika, Askofu Robert Sarah, ambaye ni Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Conacry huko Guinea ameelezea kuwa Ukristo unaweza kuimarishwa na kupewa uhai zaidi kwa watu watashiriki siyo sakramenti na Liturujia peke yake bali pia kwa kuyasoma maandiko kila siku.