Ujumbe wa Kwaresma wa Baba Mtakatifu mwaka huu

"MIMI NIPO PAMOJA NANYI SIKU ZOTE, HATA UKAMILIFU WA DAHARI (MAT.28:20)"

Wapendwa Dada na Kaka,

Mwaka huu, adhimisho la kwaresma, ni la kipekee;linatokea wakati wa uongofu na upatanisho lina hali ya pekee likitokea wakati wa Jubilei Kuu ya Mwaka 2000. Kwa kweli wakati wa Kwaresma ni wakati wa kilele cha safari ya kuongoka na kupatanishwa ambao ni Jubilei, mwaka wa Bwana, unatoa fursa kwa waaminifu ili wazaliwe upya katika Kristo na kutangaza uponyaji wake wa miujiza kwa hamu kubwa katika millenia mpya.

Kwaresma inawasaidia Wakristo kuingia kwa undani zaidi katika, " siri iliyofichika kwa zama zote"(Ef 3:9) Inawaongoza Wakristo kukutana ana kwa na Neno la Mungu na kuwataka kuachana na ubinafsi ili wapate kuongozwa na Roho Mtakatifu

Tulikuwa wafu kupitia dhambi(Efe 2:5). Ndivyo Mtakatifu Paulo anavyoielezea hali ya ilivyo kwa mtu asiye na Kristo.

Ndiyo maana Mwana wa Mungu alijifanya mtu, na kuungama na kuwatoa katika utumwa wa dhambi na mauti.

Huu ndio utumwa anao kutana nao kila siku kwa namna ulivyo na mizizi ndani ya moyo wake.(Mat 7:11). Wakati mwingine utumwa huo unajionesha wenyewe kwa njia zisizo za kawaida, kama ilivyotokea katika matukio makubwa ya karne ya ishirini, yaliyogusa kwa undani maisha ya jumuia na watu wasihesabika, Waathirika wa vurugu za kikatili, kuhamishwa kinguvu katika makazi,uangamizaji wa watu na kunyimwa haki zao za msingi za kibinadamu.haya ndiyo maovu yanayo unyanyasa ubinadamu hadi leo.katika maisha ya kila siku, pia tunashuhudia aina mbalimbali za utapeli, chuki, mauaji na udanganyifu ambao mwanadamu ndiyo chanzo chake na ndiye muathirika pia.

Ubinadamu unakabiliwa na dhambi. Hali mbaya ya binadamu inatukumbusha kilio alichotoa Mtume Paulo kwa mataifa: "Hakuna mwenye haki hata mmoja" (Rum 3: 10; Zab. 14: 3)

Kwa sura ya giza la dhambi na kushindwa kwa binadamu kujiokoa mwenyewe, ndipo inapotokea katika mwonekano wote, kazi ya ukombozi wa Kristo. "Ambaye Mungu amekwisha muweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake ili aoneshe haki yake" (Rum. 3:25)Kristo ni Mwanakondoo wa Mungu aliyechukua dhambi za ulimwengu.(Yn. 1:29). "Tena alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba."(Flp. 2:8)ili kumkomboa mwanadamu toka utumwa wa dhambi na kumrudisha katika asili ya ubinadamu wake kama Mwana wa Mungu.

Hili ni Fumbo la Pasaka ambalo kwalo, tunazaliwa upya.Hapa ni kama utaratibu wa Pasaka unavyosema, "Kifo kilishindana na maisha, shindano lililoisha kimaajabu."

Mababa wa Kanisa wanakiri kwamba katika Kristo Yesu, shetani ambaye huvamia ubinadamu na kuushikamanisha na kifo, mtu huwekwa huru kwa uwezo wa ufufuko.

Katika Bwana Mfufuka, nguvu za kifo huangamizwa na kupitia imani, mtu huingia na Mungu katika Jumuia.

Kwa waamini, maisha ya Kimungu hutolwa kwa utendaji wa Roho Mtakatifu. "Zawadi ya kwanza kwa Waamini" (Sala ya Ekaristi IV).

Hivyo, ukombozi uliokamilishwa msalabani huufanya upya ulimwengu na kuleta upatanisho kati ya mungu na mtu, na kati ya mtu na mtu.

Jubilei ni wakati wa neema ambapo tunaalikwa kujifunua kwa namna ya pekee kwa huruma wa Baba, ambaye kupitia Mwana, amemfikia mtu na kutuletea upatanisho ambao ni zawadi kubwa aliyotupa kristo.

Kwa hiyo, mwaka huu, si tu kwa Wakristo, bali pia kwa watu wenye mapenzi mema, unapaswa kuwa wakati mwafaka wa kushuhudia uwezo wa Mungu katika kupenda na kusamehe.

Mungu humhurumia yeyote anayekuwa tayari kupokea huruma hiyo hata kwa aliye mbali, na mwenye mashaka.Watu wa nyakati zetu waliochoshwa na matumaini ya uongo, wanapewa nafasi kupitia kwenye njia ya ukamilifu wa maisha.

Kwa mtazamo huu, Kwaresma ya Mwaka Mtakatifu wa 2000 ni"wakati uliokubalika-siku ya Wokovu"(2Kor.6:2)na ni nafasi inayofaa "kupatanishwa na Mungu" (2Kor.5:20).

Wakati wa Mwaka Mtakatifu, Kanisa linatoa nafasi mbalimbali kwa mtu binafsi na kwa jumuiya. Kila jimbo limependekeza maeneo maalumu ambapo waamini wanaweza kwenda ili kushuhudia uwepo wa Mungu,kwa kutambua madhambi yao kupitia mwanga wake, na kwa Sakramenti ya Upatanisho, waingie katika njia mpya ya maisha.

Umuhimu wa pekee unahusishwa na kuhiji katika Nchi Takatifu ya Roma, sehemu mahsusi za kukutana na Mungu kutokana na umuhimu wake wa kipekee katika historia ya Wokovu.

Tutashindwaje japo kiroho, kuelekea nchi ambayo miaka elfu mbili iliyopita, ilimshuhudia Bwana akiipita? Hapo, "Neno alifanyika mwili" (Yn.1:14) na "akazidi kuendelea katika hekima na kimo,akimpendeza Mungu na wanadamu (Lk.2:25)."hapo, alikuwa akizunguka katika miji yote akihubiri Habari Njema ya ufalme na kuponya yote na udhaifu wa kila aina" (Mat 9:35); hapo alikamilisha jukumu alilopewa na Baba. (Yn.19:30)na kuvuvia Roho Mtakatifu kwa kanisa la Mwanzo. (Yn.20:22).

Pia, natumaini hasa wakati wa Kwaresma ya Mwaka 2000, kuhiji katika Nchi Takatifu pale ambapo imani yetu ilianzia, ili kuadhimisha Jubilei ya miaka elfu mbili ya umwilisho.Ninawaalika Wakristo wote kuungana nami kwa sala zao wakati mimi mwenyewe katika hatua mbalimbali zakuhiji, nitaomba msamaha na upatanisho kwa Wanakanisa na watu wote.

Njia ya kuongoka hutufikisha katika upatanisho na Mungu na hutuingiza kwenye ukamilifu wa maisha mapya katika Kristo, maisha ya imani, matumaini na upendo.

Fadhila hizi tatu hujulikana kama fadhila za "kiteolojia" kwa sababu zinatuelekeza moja kwa moja kwa mungu katika Fumbo lake. Zimekuwa pia kiini cha mtazamo wa pekee kwa kipindi cha miaka mitatu ya matayarisho ya Jubilei Kuu. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu yana mualika kila Mkristo kuziishi na kuzishuhudia fadhila hizi tatu kwa namna ya ukamilifu zaidi.

Zaidi ya yote, neema za Jubilei zinatutaka kuimarisha imani yetu binafsi.Hii inahusisha kuendelea kutangaza Fumbo la Pasaka ambalo kwalo waamini wanatambua kwamba katika Kristo Msulubiwa na Mfufuka katika wafu,wamepata Wokovu. Siku hadi siku, wanamtolea maisha yao, wanakubali kila kitu anachokikusudia Bwana kwa ajili yao na kwa uhakika kwamba Mungu anawapenda. Imani ni "ndiyo" ya kila mtu kwa Mungu, na ndiyo "amina" yao.

Kwa Wayahudi, Wakristo na Waislamu kadhalika, Abrahamu ni mfano, kwa kuziamini ahadi aliifuata sauti ya Mungu iliyomtaka kuelekea asikokujua. Imani inatusaidia kuzigundua alama za upendo wa Mungu katika uumbaji,watu, matukio ya historia na zaidi ya yote, kupitia matendo na ujumbe wa Kristo kadri anavyowaamsha watu kujitafiti wenyewe na kufikia pale ambapo Fumbo la Upendo wa Mungu kwa kila kiumbe wa Mungu hudhihirika.

Kupitia neema za Jubilei, Bwana anatualika pia kuimarisha matumaini yetu. Kwa kweli, wakati wenyewe unakombolewa katika Kristo na kufungua matarajio ya furaha isiyo na mwisho kwa muungano kamili na Mungu.Kwa Wakristo, muungano unaashiriwa na matarajio ya sherehe za milele ambazo hutabiriwa kila siku kwenye meza ya ekaristi wakitazmia furaha ya milele, "Roho na Bibi harusi wasema Njoo." (Ufu. 22:17)

Wanadumisha matumaini ambayo huukomboa wakati kutoka hali yake ya kujirudia na kuupa maana yake halisi.

Kupitia fadhila ya matumaini, Wakristu hushuhudia ukweli kwamba ndani ya uovu wote, historia huzaa mbegu ya wema ambayo Bwana ataiwezesha kufikia ukamilifu wake. Kwa hiyo Wakristu wanatazamia katika Milenia mpya kukabliana bila wasiwasi na changamoto na matazamio ya baadaye kwa uhakika wenye msingi katika imani inayotokana na ahadi ya Bwana.

Hatimaye, kupitia Jubilei Bwana anatuomba tuimarishe upendo wetu.

Ufalme ambao Kristo ataufunua katika ukamilifu wake mwishoni mwa nyakati tayari umejidhihirisha pale ambapo watu wanaishi kwa kadri ya mapenzi ya Mungu.

Kanisa linaalikwa kushuhudia amani na upendo ambavyo ni alama pekee za ufalme. Katika jukumu hili jumuiya ya Kikristo inajua kwamba imani pasipo matendo imekufa.(Yak.2:17).

Hivi kwa upendo, Wakristo huonyesha upendo wa Mungu kwa mtu, unaojifunua katika Kristo na kudhihirisha uwepo wa Kristo duniani "mpaka mwisho wa nyakati." Kwa Wakristo, upendo sio tu kitu cha fikra, bali ni mwendelezo wa uwepo Kristo anayejitoa mwenyewe.

Wakati wa Kwaresma, tajiri na maskini wanaalikwa kuuwezesha upendo wa Kristo uwepo kwa matendo mema.

Wakati huu wa mwaka wa Jubilei, upendo wetu unapaswa kuonekana ukishuhudia upendo wa Kristo kwa ndugu zetu ambao wanakosa mahitaji muhimu ya maisha, wanaoteseka kwa njaa, magomvi na dhuluma.

Hii ndiyo njia ya kufanya fikra za ukombozi na ndugu zionekane katika Maandiko Matakatifu, zionekane kuwa kitu cha kweli, fikra ambazo mwaka mtakatifu huziweka mbele kwa mara nyingine.

Jubilei ya kizamani ya Kiyahudi kwa hakika ilitaka kuachiwa huru wafungwa, kufuta madeni na ktoa msaada kwa maskini. Leo hii aina mpya za utumwa na miundo mibaya ya umaskini huathri idadi kubwa ya watu, hasa kwenye zile zinazoitwa nchi za dunia ya tatu.

Hiki ni kituo cha wanaoteseka na kukata tamaa, ambacho lazima kisikike na kupatiwa jawabu kwa wote wanaoipita njia ya Jubilei. Tutawezaje kuomba neema za Jubilei kama hatujali mahitaji ya maskini, kama hatujitahidi kuona kwamba wote wanapata mahitaji muhimu kwa maisha ya kisasa?

Basi Milenia hii iwe wakati ambao kilio cha ndugu zetu wasio na mahitaji kinasikika na kupatiwa jawabu muafaka.

Ni matumaini yangu kwamba Wakristo wa ngazi zote watakuwa mstari wa mbele kudumisha jitihada zitakazopelekea usawa katika ugawanaji rasilimali na kudumisha maendeleo kamili ya kila mtu.

"Mimi niko pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari." Maneno hayo ya Yesu yanatuhakikishia kwamba katika kuitangaza na kuiishi Injili ya upendo hatupo peke yetu.

Kwa mara nyingine wakati huu wa Kwaresma ya mwaka 2000 anatualika tena kumrudia Baba anayetusubiri atuwezeshe kuwa ishara hai za upendo wake wenye huruma.

Kwa Maria Mama wa wote wanaoteseka na Mama wa Huruma ya Mungu tunamkabidhi nia zetu na maazimio yetu. Basi, awe nyota inayong’ara katika safari yetu ya Milenia mpya.

Kwa maneno haya namtakia kila mmoja wenu Baraka za Mungu Mmoja katika Utatu, Mwanzo na Mwisho wa vitu vyote, ambaye kwake tunamtaka " mpaka mwisho wa nyakati," wimbo wenyeBaraka na sifa kwa Kristo.

"Kwa njia yake, pamoja naye na ndani yake, katika Umoja wa Roho mtakatifu unapata heshima na utukufu wote, Baba Mwenyezi, daima na milele. AMINA."

Yohane Paulo ll, Vatican.