Wakatoliki, Wapentekoste watakiwa kutoogopana, mbingu ni moja

Vatican (CNS)

WAKATOLIKI na Wapentekosti hawatakiwi kuogopana na kubaguana badala yake wanatakiwa kuwa kitu kimoja ili kujifunza kutoka kwa mwenzake.

Hayo yamesemwa na Askofu, Carl H.Montgomery wa Umoja wa Makanisa ya Kipentekosti ya Marekani wakati alipokuwa akizungumza kwenye mkutano ulioshirikisha ujumbe wa Maaskofu wapatao 170 wa Kanisa hilo na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Yohane Paulo wa II.

Askofu Montgomery ameelezea kuwa Wapentekosti na Wakatoliki hawapaswi kuogopana wala kubaguana tena kwa sababu kwa sasa hivi Roho kama yule aliyemwagwa wakati wa Pentekoste anawashukia wote Wakatoliki na Wapentekosti "The Spirit of the Lord is being poured out on all in this time.

"Catholics and Protestants are all experiencing the Pentecost Experience"

Askofu huyo ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa msafara wa Maaskofu 170 wa Kipentekosti waliomtembelea Papa huko Vatican ameendelea kufafanua kuwa hakuna haja ya Wapentekosti na Wakatoliki kubaguana hapa duniani wakati watakapofika mbinguni kwa baba watakuwa kitu kimoja.

"We are all going to be with the Lord in heaven, when this is over so why be Segregated here?" Ameendelea kufafanua kwa nguvu ya kiroho sasa imevuka mipaka ya kidhehebu na haiangalii kama huyu ni Mpentekosti ama ni Mkatoliki bali inatenda kazi sawa kwa watu wa pande zote mbili.

"We see a lot of things coming together"

'Tunaona mambo yetu mengi yakifungamana sasa"

Alipokuwa akizungumza na Ujumbe huo wa Maaskofu wa Kipentekosti waliotembelea huko Vatican February 9 mwaka huu, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Paulo Yohane II alisema kuwa anayo matumaini kuwa ziara yao huko Roma itazidi kuimarisha baina ya Wakatoliki na Wapentekosti.

Askofu Montgomery wakati wa hotuba yake pia ameendelea kusisitiza umoja baina ya pande zote mbili uzidi kupewa kipaumbele kwa sababu ushirikiano kama huo unaweza ukapata kibali kwa Roho wa Mungu kuliko tofauti za madhehebu kiitikadi zikiendelezwa.

Naye Askofu Delano Ellis wa Umoja wa huo huo wa Makanisa ya Kipentekosti "The United Pentecostal Churches of Christ" ameelezea kuwa wangependa kuona wanapiga hatua katika mapatano baina yao na wakatoliki kiasi cha kutoka katika hali ya kirafiki waliyo nayo sasa hivi na kufikia mapatano kamili kwenye maeneo wanayotofautiana.

Askofu Ellis ameendelea kufafanua kuwa kwa vile wameanza vizuri mapatano wangependa yaendelezwe na waone na kushuhudia nini inakuwa hatma yake.

Ujumbe wa Maaskofu 170 wa Kipentekosti walikuwepo mjini Roma katika ziara maalum ya kukutana na Papa kuanzia Feb 7 mpaka 15 ambapo wakiwa huko pia walishiriki misa kwenye Kanisa Katoliki lililoko mjini Roma.

Mamia ya Waislamu, Wakristo wauana Nigeria

Lagos, Nigeria

WATU zaidi ya 300 wameuawa katika mapigano ya kidini katika Jimbo la Kaduna, nchini Nigeria kutokana na Wakristo wa jimbo hilo kupinga kuanzishwa utawala wa Sharia za Kiislamu.

Kufuatia mapambano hayo maiti za watu zimekuwa zikikutwa zimezagaa mabarabarani na Jeshi la nchi hiyo limekuwa na kazi kubwa ya kukusanya maiti na kuwazika katika makaburi ya pamoja kwa vile ndugu na jamaa za marehemu wamekuwa wakijificha ama kukimbia makazi yao.

Maelfu ya wananchi katika jimbo hilo wamekimbilia katika kambi za jeshi kujihami na mashambulizi hayo yasiyo na huruma.

Habari zinasema Jeshi la nchi hiyo limekubali kutoa hifadhi kwa wahanga hao wa vita hususan wanawake na watoto.

Afisa mmoja wa kijeshi alikaririwa akisema kuwa maiti zaidi ya 30 zilionekana zikiwa zimeoza kando ya barabara wakati zaidi ya maiti 210 walikuwa katika hospitali moja, mali ya chuo cha ufundi.

Katika vyumba vya maiti katika Hospitali Kuu ya Jimbo la Kaduna, maiti wamelazwa ardhi baada ya kukosekana mahali pa kuwahifadhia.

Kufuatia mapambano hayo, mali nyingi zimeharibiwa ikiwa ni pamoja na makanisa, misikiti, nyumba za watu,magari na mali nyingine.

Hali hiyo imeleta mashaka makubwa kuhusu hatma ya kiusalama ya maisha ya Wanigeria wapatao milioni 108 ikiwa ni chini ya nwaka mmoja tangu Rais wa nchi hiyo Olusegun Obasanjo alipotwaa madaraka kutoka kwa utawala wa kijeshi uliodunu kwa zaidi ya miaka 15.

Hivi karibuni jimbo jingine la Zamfara nchini humo lilipitisha rasmi utawala wa sheria za Kiislamu, ambapo siku chache tu baadaye kijana mmoja aliyezini alichapwa viboko 100 na makahaba wameahidiwa kupewa mitaji ili waache tabia zao mbaya.