Make your own free website on Tripod.com

Uganda yatiwa kabali na Umoja wa Mataifa

Kampala, Uganda,

HATIMAYE Serikali ya Uganda imenyoosha mikono na kuamua kuanzia jana kuhamisha majeshi yake yaliyokuwa yakipambana na yale ya Rwanda katika Janhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, baada ya Umoja wa Mataifa kutishia kuziwekea vikwazo vya kiuchumi nchi hizo.

Hatua hiyo imekuja baada ya kauli iliyotolewa mwanzoni mwa wiki na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan, kuwa nchi hizo, yaani Uganda na Rwanda ambazo zimekuwa katika mapambano makali katika eneo la Kisangani nchini Kongo, kwa wiki kadhaa sasa.

Habari kutoka mjini Kampala zimeeleza kuwa kauli hiyo ya Annan, imeishitusha serikali ya Uganda na kwanda hatua ya sasa ya kuhamisha majeshi huko Kisangani inatokana na shinikizo hilo.

Kwa mujibu wa msemaji wa majeshi ya Uganda aliyekaririwa na Shirika la habari la Uingereza (BBC) zoezi la kuondoa majeshi huko Kisangani ambako yameshasababisha madhara makubwa ikiwa ni pamoja na mauaji holela na kujeruhi raia litachukua siku saba.

Uganda na Rwanda zimekuwa katika mapigano kwa majuma kadhaa sasa, licha ya kauli zinazopingana za kila mmoja kudai kuwa mwezie ndiye asiyetaka kusitisha mapigano.

Mapema mwishoni mwa wiki, miili ya maafisa kadhaa wa jeshi la Uganda waliouawa katika mapigano hayo iliwasili mjini Kampala, tayari kwa kila mmoja kwenda kuzikwa katika eneo analotoka nchini humo.

Mugabe awaweka roho juu wazungu

Harare, Zimbabwe,

RAIS Robert Mugabe wa Zimbabwe, ametangaza mwishoni mwa wiki kuwa anakusudia kunyang'anya migodi yote ya madini nchini humo kutoka mikononi mwa wazungu na kuikabidhi wa raia weusi.

Hatua hiyo inakuja huku zikiwa zimebakia siku chache kufanyika Uchaguzi Mkuu nchini humo, na miezi michache tangu mashujaa wa kale wa vita nchini humo walipovamia mashamba ya wazungu na kuyamiliki kwa nguvu. Rais Mugabe amekuwa akishutumiwa vikali kwa kuunga mkono uvamizi huo wa mashamba.

Kumbe Askofu Misago alisingiziwa!

Kigali, Rwanda,

HATIMAYE Mahakama ya Rwanda imeweka bayana kuwa yule Askofu wa Kanisa Katoliki, nchini humo aliyekuwa akishitakiwa kwa tuhuma za kujihusisha na mauaji ya halaiki ya mwaka 1994, hana hatia.

"Madai yote dhidi ya Askofu Misago yamefutwa, sasa Misago yuko huru, ameshinda kesi," alikaririwa akisema Kiongozi wa Mahakama maalum inayoshughulikia mauaji hayo ya halaiki ya mwaka 1994, ambapo malaki ya raia wa Kitutsi na Wahutu wachache waliuawa.

Awali upande wa mashitaka ulidai katika Mahakama hiyo kuwa Askofu Misago, alishiriki kikamilifu kuchochea na kusaidia mauaji dhidi ya raia wa Kitutsi nchini humo.

Tuhuma hizo pia zilidai kuwa Askofu Misago, alishirikiana na utawala wa nchi hiyo katika kuendesha mauaji hayo mabaya ambayo yaliishitua karibu dunia yote.

Kutokana na hisia kwamba Askofu huyo alikuwa akishiriki katika mauaji, Wanamgambo wa Kihutu waliwaua mapadre watatu na wanafunzi kadhaa katika Jimbo

Katoliki analoliongoza Askofu huyo la Gikongoro, kusini mwa nchi hiyo ndogo iliyo katika eneo laMaziwa Makuu.

Nguvu za Kijeshi: Urusi yahofia usalama duniani

Berlin, Ujerumani,

Rais Vladimir Putin, wa Russia, ameonya kuwa kuendelea kupanuka kwa Umoja wa Kujihami wa nchi za Ulaya Magharibi (NATO) ni hatari kubwa kwa usalama wa dunia.

Hofu ya Putin, inatokana na azimio la nchi za Estonia, Latvia na Lithuania, ambazo zilijitoa katika dola kubwa ya Russia (USSR).

Putin, amesema kujiunga kwa nchi hizo ambazo zinapakana nayo kwa karibu zaidi kutaifanya nchi yake ijione iko hatarini, na kwa sababu hiyo kuiweka hali ya usalama duniani katika mashaka.

Bw. Putin pia, ameonya kuwa ya azimio la Marekani kuunda mfumo wake mpya wa usalama wa anga, nayo ni hatua nyingine ya kuiweka dunia mashakani.