Kenya yahitaji nusura kuokoa uchumi wake

Nairobi, Kenya

SERIKALI ya Kenya inahitaji kiasi cha shilingi bilioni 11.5 ili kuweza kukabili athari za ukame ulioikumba na kusababisha kukosekana kwa umeme wa kutosha kuendesha shughuli za kiuchumi.

Rais Daniel arap Moi, wa nchi hiyo alisema wiki hii kuwa kiwango hicho cha fedha kinachohitajika kikipatikana asilimia 85 itaelekezwa katika kukabili upungufu wa chakula, wakati asilimia 15 itaelekezwa katika miradi ya afya,maji, kilimo na elimu.

Akijibu shutuma za wapinzani wake ambao wanasema serikali ya Kenya, ilifanya uzembe katika kujiandaa kwa balaa kama hilo, Moi alisema haoni mantiki kwa lawama hizo.

"Mimi sitengenezi mvua. Haya yaliyotokea (ukame) katika miaka minane iliyopita ni ya kimaumbile," Moi amekaririwa na redio moja akisema.

Kwa takribani mwezi mmoja sasa kumekuwa na umeme wa mgao nchini Kenya, kutokana na ukame uliopelekea kukauka kwa maji katika mabwawa yake ya kuzalishia umeme.

Hali hiyo, imesababisha kushuka kwa kiwango kikubwa kwa uzalishaji nchini humo, kwa vile viwanda vingi havifanyi kazi katika kiwango cha awali, licha ya baadhi ya huduma za jamii kama vile afya na elimu kuathirika vibaya.

Katika mji maarufu wa Mombasa umeme umekuwa ukipatikana kwa nusu siku tu, hali ambayo imeelezwa kuwa imeathiri vibaya sekta ya utalii katika mji huo.

Uhalifu wa watoto Japan wakithiri

lMmoja amchinja mwenzie na kutundika kichwa darasani

Tokyo, Japan

WANANCHI nchini Japan, wameanzisha harakati za kuishinikiza serikali ya nchi hiyo irekebishe sheria zinazohusiana na uhalifu wa watoto kwa vile sheria iliyopo sasa inawalinda kupita kiasi watoto na imeleta madhara makubwa.

Redio ya nchi hiyo imekaririwa ikisema mapema wiki hii kuwa matukio ya watoto kufanya uhalifu wa kutisha nchini humo yameongezeka na kumekuwa na matukio mengi ya watoto kuua watoto wenzao kwa vile sheria ya nchi hiyo ni legevu mno katika kudhibiti uhalifu wa watoto.

Kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo watoto ni wale wenye umri wa chini ya miaka 16 na watu wa umri huo wanapofanya makosa kuna mahakama maalum ya masuala ya familia ambayo hairuhusu kufungwa bali kupatiwa ushauri nasaha au kuhifadhiwa kwenye kituo maalum na kupatiwa ushauri kwa muda mfupi tu.

Kadhalika sheria hiyo hairuhusu makosa ya watoto hao yatangazwe hadharani kwa madai kwamba hatua kama hiyo itawaatihiri kisaikolojia katika siku za baadaye.

Oriko Take, ambaye ni mama wa mtoto mmoja aliyeuawa na mwenzie, alisema hivi sasa familia zaidi ya 30 za wazazi ambao watoto wao wameuawa na wenzao zimeungana kuishinikiza serikali irekebishe sheria hiyo na kuna matumaini kwa vile tayari muswada unaandaliwa kupelekwa bungeni licha ya kupuuzwa katika bunge lililopita.

Moja kati ya matukio ya kutisha lilitokea mwaka 1997 katika mji wa Kobe, Japan ambako mtoto mmoja alimchinja mwenzie na kukitundika kichwa chake katika mlango wa darasa.

Duniani Kwa Ufupi

Israeli yataraji kupatana na Lebanon

Jerusalem, Israel

NAIBU Waziri Mkuu wa Israeli, Bw. Benjamin Ben Eliezer, emesema ni matarajio ya serikali yake kuwa hatua waliyochukua hivi karibuni ya kuondoa majeshi katika mipaka yake na Lebanon itasaidia katika kuboresha mazungumzo ya amani kati ya nchi hizo.

Mahakama yaamuru kampuni idhoofishwe

Washington, Marekani

MAHAKAMA moja nchini Marekani imeamuru kugawanywa kwa kampuni kubwa kuliko zote ya Kompyuta duniani, MICROSOFT kwa vile imejikusanyia ukiritimba unaozidi kiasi.

Watu kadhaa nchini humo wamepongeza hatua hiyo ya mahakama na kusema itawapa wengine fursa muhimu ya kutengeneza na kuuza Kompyuta, lakini mmiliki wa Microsoft Bw. Bill Gate, amesema atakata rufaa kupinga hukumu hiyo.

mapigano ya Kongo yaua 100, kujeruhi 700

Kinshasa, JKK

Bado mapigano yanaendelea katika mji wa Mashariki wa Kongo Kinshasa - Kisangani licha ya makubaliano kuweka chini silaha kati ya Uganda na Rwanda.

Watu wasiopungua mia moja wameuawa na wengine takribani 700 kujeruhiwa tangu ripoti za nchi hizo mbili zinazowaunga mkono makundi ya waasi wa kongo Kinshasa yalipoanza upya kupigana Jumatatu iliyopita.

Awali Maraisi wa Unganda na Rwanda Bw. Yoheri Museveni na Paul Kagame walikubaliana kuweka silaha zao silaha chini.

Uamuzi huo wa kuweka silaha chini, ulitokana na upatanishi wa Katibu Mkuu, na wa Balozi wa Marekani katika umoja huo.

India yakubali kupunguza silaha kali

New Delhi, India

WAZIRI wa Mambo ya Nje wa India, Bw. George Fernandes, amesema analishauri Bunge la nchi hiyo kupitisha azimio la kupunguza silaha kali.

Alisema wiki hii kuwa Serikali yake inakusudia kusaini mkataba wa kimataifa uitwao CTBT wenye makusudi ya kupunguza silaha kali na hasa majaribio ya silaha za kinyuklia.

Albright ataka ulimwengu kupambana na ujambazi

New York, Marekani

WAZIRI wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Bi. Madeleine Albright, ametoa wito wa hatua za pamoja kupambana na janga la ujambazi ulimwenguni.

Akihutubia mkutano wa akinamama anasema kwamba uhalifu huo umepindukia na kuvuka mipaka ya kuvumiliwa mipaka.

Biashara ya ujambazi inaathiri uchumi,, inatesa jamii na kuwapokonya matumaini ya mamilioni ya watu ulimwenguni.