Ethiopia na Eritrea waendelea kutwangana

Adis Ababa,

WAKATI Ethiopita ilitangaza Alhamisi iliyopita kuwa mzozo wa mpaka kati yake na Eritrea umekwisha, baada ya kutwaa maeneo iliyokuwa aikiyakalia, imeelezwa baadaye kwamba hali bado sio shwari miongoni mwa mataifa hayo jirani.

"Vita imekwisha, tumeshasinda na kuchukua maeneo yetu yaliyokuwa yameshikwa na adui," Meles Zenawi, Waziri Mkuu wa Ethipia alikaririwa akisema Alhamisi iliyopita. Hata hivyo,kwa mujibu wa taarifa za Redi ya Ujerumani, Ijumaa mwishoni mwa wiki hii, sambamba na mapendekezo hayo, Serikali ya Ethiopia ilitangaza kuzuka kwa mapigano mapya miongoni mwa nchi hizo.

Ethiopia imesishutumu Eritrea kwa mashambulio yake iliyofanya katika eneo la mshariki ya Ethiopia ambapo makombora yake yalisababisha uharibifu mkubwa na kuua watu wapatao wawili.

Kwa mujibu wa taarifa za redi hiyo, hakukuwa na taarifa zaidi zilizotolewa kuhusiana na mapigano hayo mapya kutoka upande wowote kati ya Eritrea na Ethiopia.

Katika hatua za kuzipatanisha pande hizo mbili kwa mazungumzo Waziri wa sheria wa Algeria bw. Ahmed Oyahya, kwa msaada wa Umoja wa nchi huru za Kiafrika (OAU) amekuwa akiendesha mazungumzo ambayo yanatoa mwanga kidogo wa kuweza kutatua mgogoro huo.

Watetezi wa Uhai washinda rufaa ya kesi Ujerumani

London, Uingereza

MAHAMAKA ya rufaa nchini Ujerumani imewaruhusu watetezi wa uhai (Pro-lifers) kufananisha utoaji mimba na mauaji kama yale ya Nazi yaliyoangamiza mamilioni ya Wayahudi zama za Adolf Hitler..

Awali uongozi wa hospitali ya Nuremberg ambako utoaji mimba hufanyikia ulishinda kesi ya kutaka watetezi wa uhai wapigwe marufuku kufanya kampeni zao za kusambaza vipeperushi (leaf leats)vinavofananisha utoaji mimba na uuaji.

Mahakama ya shirikisho huko Karlsruhe,katika kupindua hukumu hiyo ilisema kuzuia kampeni hizo ni kuvunja haki ya msingi ya binadamu ya kujieleza.

Utoaji mimba nchini Ujerumani kimsingi hauruhusiwi ila unaweza ukaruhusiwa katika mazingira fulani fulani.

Taarifa ya utafiti iliyotolewa na UNICEF hivi karibuni imesema kuwa vitendo vya utoaji mimba utokanao na uchaguzi wa jinsia za watoto umepelekea kuwepo kwa upunguzu wa wanawake wapatao milioni 60 duniani.

"Ni wahanga wa familia zao wenyewe waliouawa kwa masusudi au kwa kutelekezwa, kwa vile tu ni wa jinsia ya kike" gazeti la Independent la Uingereza lilieleza.

Polisi wajifanya waandishi kumnasa mhalifu

Wasserbillig, Luxemburg

YULE Mtekaji nyara aliyewateka watoto wapatao 25 katika shule katika nchini ambayo imelezimika kufunga gereza lake kutokana na uchache wa matukio ya uhalifu, hatimaye amejeruhiwa kwa risasi na polisi na watoto wote aliowateka kuachiliwa huru.

Mtekaji nyara huyo, ambaye amekuwa gumzo la wiki duniani, tangu alipofanya kitendo hicho mwanzoni mwa wiki, alinaswa kwa mtego wa kupumbazwa kwamba waandishi wa habari walikuwa wakienda kumhoji, na ndipo polisi wakajifanya waandishi na kubeba kamera ya video ambayo ilikuwa ina risasi kama bunduki na ndiyo iliyotumika kumjeruhi kichwani na kufanikiwa kuachiwa kwa watoto aliokuwa amewashikilia, akidai serikali ya Luxemburg, impatie ndege ya kwenda Libya.