Askofu Mkuu ahojiwa kwa kuilaumu waziwazi serikali

lAdai inachochea ubaguzi wa rangi

HARARE, ZImbabwe

ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini Zimbabwe, Mhashamu Pius Nhkube, amehojiwa na maafisa wa upelelezi nchini humo baada ya kuilaumu katika barua ya wazi serikali ya nchi hiyo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa gazeti moja la kila siku la nchini Zimbabwe, Askofu Mkuu huyo aliwaambia maofisa hao wawili wa upelelezi waliokuwa katika mahojiano hayo kuwa yeye hajihusishi na masuala ya kisiasa katika chama chochote nchini humo. Katika barua hiyo ya wazi, Askofu Mkuu huyo Nkhube, aliwalaumu waziwazi wavamizi wa mashamba ya Wazungu na kumlaumu Rais Roberti Mugabe wa nchi hiyo kwa madai kuwa wanachochea vitendo vya ubaguzi wa rangi.

Serikali ya Rais Robert imekwisha chukua mashamba 841 yanayomilikiwa na Wazungu kwa ajili ya kuyagawa upya kwa Waafrika wasikuwa na ardhi.

Nchi hiyo imepitsha sheria ya kuchukua mashamba yanayomilikiwa na Wazungu bila kutoa fidia.yoyote.

Sheria hiyo mpya imewezekana baada ya nchi hiyo kufanya marekebisho ya katiba mwezi uliopita

Shria inatamka wazi kuwa anayestahili kulipa fidia ni Uingereza iliyokuwa mtawala wa zamani wa Zimbabwe.

Marekebisho hayo ya sheria yamekuja baada ya kuvamiwa kinyume cha sheria mashamba zaidi ya 1300 yaliyokuwa yanamilikiwa na Wazungu hao

hata hivyo, serikali ya Uingereza imesema iko tayari kutoa shilingi bilioni kwa ajili ya ugawajupya wa ardhi kwa ajili ya wakulima wadogo wadogo endapo ugawaji huo utakuwa unaozingatiwa kwa uwazi na kwa haki.

Mjumbe wa UN ahuzunishwa na hali ya wakimbizi nchini Angola

Luanda, Angola

KATIKA ziara yake iliyochukua juma moja nchini Angola,mjumbe wa Umoja wa Mataifa

Balozi Ibrahim Gambari, alieleza kutoridhishwa kwake na hali ya usalama ilivyo nchini humo.

Jambo lililomhuzunisha zaidi ni hali ya maisha na usalama wa wananchi waliolazimika kuyahama makazi yao kwa sababu za vita kati ya majeshi ya serikali ya nchi hiyo na yale ya waasi wa UNITA wanaoongozwa na Bw. Jonas Savimbi.

Alipotembelea nyanda za juu za kati katika mji wa Huambo, ambao ni jiji la pili nchi Angola, mwishoni mwa wiki, Gambari, alisema: "Ninayoyaona hapa Huambo yananikosesha sana furaha. Ndio maana nimeanza kufanya kazi kutafuta njia bora zaidi ya kuweka mambo sawa."

Gambari ni Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Kofi Annan aliyepewa jukumu maalum la kuangalia na kumshauri juu ya usalama wa Afrika.

Zoraida Mesa, Mratibu wa masuala ya Misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa,

Ambaye alimsindikiza Gambari, wakati alipotembelea eneo la Viana, umbali kama wa kilomita 20 mashariki ya mji mkuu wa Luanda, alisema:

"Naungana na hali ya kujali ya Gambari juu ya hali mbaya ya watu walioyaacha makazi yao. Ziara yake imekuja kwa wakati Serikali ya Angola ikifanya kazi kwa karibu na watoaji wa misaada ya kibinadamu imeanza kutekeleza masuala muhimu

yatokanayo na ripoti ya tathmini juu ya matatizo mazito ya Angola."

Maneno yake hayo yalikuja baada ya kujionea mwenyewe makambi ya wakimbizi ya Viana ambako wa-Angola 6,000 na wakimbizi wengine 6,5000 wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, ambao wanaishi katika mahema yasiyo na hewa ya kutosha na vijibanda vya udongo mtupu.