Vatican yawawekea ngumu watalaka

Vatican City, Vatican

MAKAO Makuu ya Kanisa Katoliki duniani mjini Vatican yamesema kanisa litaendelea na msimamo wake wa kutowapa sakramenti ya mkate waumini wake ambao wameoa au kuolewa na kuachana.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kanisa hilo mjini Vatican wiki hii wanaume walioacha wake zao na wanawake walioachwa wataruhusiwa kupata Sakramenti hiyo endapo itathibitika kuwa hawafanyi tena t tendo la ndoa.

Taarifa hiyo ya mwishoni mwa wiki imesema sheria za Kanisa Katoliki kamwe hazitavunjwa kutokana na malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa kwa muda mrefu sasa na watalaka kuwa wananyimwa haki.

Sheria ya Kanisa hilo hairuhusu watu walioona kuachana isipokuwa katika mazingira kwa wahusika.

Linatambua tu ndoa ya kwanza, hata kama imevunjika na wanandoa wakaoa au kuolewa tena.

Hata pale ambapo Kanisa linalazimika kubatilisha ndoa, hati za kufanya hivyo hupatikana kwa ugumu mkubwa.

Wakatoliki wengi ambao ndoa zao zimevunjika hususani nchi za Magharibi wamekuwa wakiomba kufikiriwa na kanisa ili waruhisiwe kuoa au kuolewa tena na ndoa zao zitambuliwe.

Wazungu Zimbabwe wakubali kuuza mashamba yao

Harare, Zimbabwe

CHAMA cha Wakulima wa Kizungu nchini Zimbabwe (Commercial Farmers Union) kimesema Wazungu nchini humo wako tayari kuuza mashamba yao yapatayo 400 kwa Serikali ya Zimbabwe ili yagawiwe kwa raia weusi.

Kwa mujibu wa Kiongozi mmoja wa chama hicho Bw. Jerry Grant, hakuna sababu ya Serikali kuendelea kuchukua mashamba yao kwa nguvu kwani wao wako tayari kuyauza.

Bw. Grant alisema mwishoni mwa wiki kwamba chama chake kinakubaliana na wazo la kuwepo uwianowa umiliki wa mashamba nchini humo kati ya Wazungu na Weusi.

Hivi karibuni Serikali ya Zimbabwe ilitoa notisi ya mwezi mmoja ambayo ilimalizika Julai 3 mwaka huu ikitaka Wazungu wajitetee kwanini mashamba yao yapatayo 804 yasitwaliswa na Serikali na kugaiwa kwa raia.

Wazungu hao walikata rufaa na bado wangali wanasubiri uamuzi wa rufaa hiyo.

Mvutano kati ya maveterani wa vita vya ukombozi nchini humo umedumu kwa miezi kadhaa sasa na watu kadhaa hususani Wazungu wamekuwa katika nyakati mbalimbali baada ya mashamba yao kuvamiwa.

Uingereza na Jumuiya ya Kimataifa zimekuwa zikimlaumu Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo pamoja na Chama chake kinachotawala cha ZANU-PF kwa kushindwa kuheshimu utawala wa Sheria.

Mugabe amekuwa akituhumiwa kwamba anachochea uvamizi wa mashamba ya wazungu.

Kundi la Sankoh kuzibiwa ‘riziki’

Washington, Marekani

BARAZA la Usalama la Umoja wa Mataifa, limepitisha azimio la kuzitaka nchi zote na wafanyabiashara wa kigeni kutonunua madini ya almasi kutoka nchini Sierra Leone kwani imebainika kuwa biashara hiyo ndiyo inayoshamirisha vita vya waasi wa RUF waliokuwa wakiongozwa na Bw. Fodau Sankoh.

Sambamba na hatua hiyo, serikali ya Sierra Leone imetakiwa kuhakikisha inawanyang’anya waasi hao machimbo yote ya dhahabu ambayo wamekuwa wakiyamiliki au kuyashikilia kwa nguvu.

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, hatua hiyo imepingwa mwishoni mwa wiki na Balozi wa nchi ya Mali katika Umoja wa Mataifa, Bw. Moctar Ouane, kwa maelezo kwamba inaingilia uchunguzi wa Tume ya mataifa ya Afrika ya Magharibi kuchunguza suala hilo.

Utajiri wa madini nchini Sierra Leone ndicho chanzo kikuu cha kutomalizika kwa vita kati ya serikali ya waasi wa Revolutionary United Front, ambao kiongozi wao mkuu Bw. Foday Sankoh alikamatwa Mei, mwaka huu.

Afrika ya Kusini yaogofya

Johannesburg, Afrika Kusini

SERIKALI ya Afrika Kusini imesema itawachukulia hatua kali wanaume wawili wanaotuhumiwa kuwabaka na kuwaua wanawake wapatao 32.

Wauaji hao ambao wanakabiliwa na kesi 53 zinazohusiana na makosa hayo pia waliwaua watoto 17 wenye umri kati ya miaka minane na kumi na moja.

Msemaji wa polisi nchini humo Henriette Bester, alikaririwa akisema mwishoni mwa wiki kuwa tayari watu hao waliokuwa wakisakwa vikali kwa mauaji hayo ya hivi karibuni wamekwishakamatwa.

Shirika la habari la Uingereza Reuters nalo lilikaririwa likisema Afrika Kusini hivi sasa inaelekea kuongoza kwa uhalifu wa mauaji duniani.

Lilisema wakati nchini Marekani watu sita tu kati ya laki moja huuawa kwa mwaka nchini Afrika Kusini. Watu 53.3 huuawa kati ya watu laki moja.

Mtu anayeongoza kwa uhalifu huo nchini Afrika Kusini ni Bw. Moses Sithole ambaye yeye peke yake amewahi kuua watu 38 na kuwabaka wanawake 40