Make your own free website on Tripod.com

Wapinzani wa Museveni wapinga kuulizwa watawaliweje

Kampala, Uganda

WAPINZANI wa Serikali ya Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, wamepinga hatua ya serikali hiyo kuitisha kura ya maoni kuwataka Waganda waamue kurejeshewa mfumo wa vyama vingi, au waendelee na mfumo wa sasa wa chama kimoja.

Wakati zoezi la upiagaji kura hiyo lilianza Alhamisi iliyopita, kulikuwa na idadi ndogo ya watu waliopiga kura hususan katika maeneo ya Kaskazini ya nchi hiyo.

Rais Museveni mwenyewe anadai kuwa kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini humo kutazua vita na kuleta maafa kama yale yaliyowahi kuikumba nchi hiyo katika miaka ya nyuma.

Lakini wapinzani wa Rais Museveni, licha ya kupinga dhana hiyo, wamesema pia kwamba hata zoezi lenyewe la upigaji kura kuchagua mfumo gani wa siasa kati ya ule wa chama kimoja na vyama vingi ni batili, kwa vile suala la utawala wa vyama vingi ni haki isiyohitaji kuhojiwa.

Hivi sasa Uganda inaongozwa bila kuwepo kwa chama chochote.

Watu wapatao milioni mbili kati ya raia milioni 20 wa Uganda walijiandikisha kupiga kura hiyo ambayo matokeo yake yanatarajiwa kutangazwa leo,

Licha ya Uganda kutokuwa na chama chochote cha siasa yapo makundi mengi yasiyo rasmi na yenye majina ambayo yamekuwa yakiipinga serikali hiyo na baadhi ya makundi kama vile Lord's Resistance Army, kuendesha vita dhidi ya Serikali.

Rais Museveni alitwaa madaraka ya nchi hiyo mwaka 1986 baada ya mapambano ya msituni ya takriban miaka mitano.

Uchumi wa Uganda umekuwa ukipanda katika miaka ya karibuni, pamoja na kutokuwepo kwa mfumo wa vyama vingi, jambo ambalo linaaminiwa kuwa linaweza kuwafanya Waganda wakaamua kuendelea na mfumo wa sasa usio na chama.

Kiongozi wa zamani wa Ujerumani akana kula rushwa

Berlin, Ujerumani

KIONGOZI wa zamani wa Ujerumani, Chansela Helmut Kohl, mwishoni mwa wiki amekanusha madai ya muda mrefu kwamba yeye alipokea rushwa wakati alipokuwa madarakani.

Akitoa ushahidi mbel ya kamati ya Uchunguzi ya Bunge la Ujerumani, Kohl, juu ya kashfa ya chama chake kuwa alipokea michango haramu, alisema hajawahi kupokea fedha kwa ajili ya kutoa upendeleo wa kisiasa.

Hata hivyo, Bw. Kohl, alikiri kupokea dola milioni mbili za kimarekani kama msaada kwa chama chake cha CDU, lakini alishikilia msimamo wake wa awali wa kutowataja waliompa fedha hizo.

Alidai kuwa kuitwa kwake katika kamati hiyo ya

Bunge ni njama za makusudi za kutaka kumchafulia jina na kuchafua kazi yote aliyoifanya ikiwa ni pamoja na kufanikisha muungano kati ya Ujerumani ya Mashariki na Magharibi.

Bw. Kohl, ambaye alidumu madarakani kwa miaka kumi na sita, aliitwa mbele ya kamati hiyo baada ya mpelelezi wa serikali kuiambia kamati kuwa mamia ya mafaili katika ofisi ya chansela huyo yaliharibiwa mara baada ya kushindwa kwake katika Uchaguzi mkuu wa Septemba, mwaka 1998.

Mpelelezi huyo alieleza kuwa zipo nyaraka nyingi zilizoharibiwa mwezi mmoja kabla ya Bw. Kohl kukabidhi madaraka.