Kiongozi wa dini ya Falun Gong China apelekwa jela miaka kumi na saba

Hong Kong

KITUO cha habari cha Shirika la kutetea haki za binadamu lenye makao yake makuu mjini Hong Kong, kimesema Jenerali wa zamani wa majeshi ya Anga ya China, ambaye ni kiongozi wa madhehebu ya dini ya Falun Gong nchini humo, amehukumiwa kwenda jela miaka 17 kwa sababu za kuendesha dini hiyo kinyume na matakwa ya Serikali ya China.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 74 alihukumiwa na mahakama ya kijeshi ya China na hadi sasa serikali ya China haijasema lolote, kwa mujibu wa kituo hicho cha haki za binadamu.

Kwa mujibu wa taarifa za kituo hicho zilizokaririwa na Redio Ujerumani mwishoni mwa wiki, hatua hiyo imewashtusha majenerali wengine wastaafu wa jeshi la nchi hiyo.

Aprili mwaka jana Kiongozi huyo alifukuzwa nchini China kutokana na madai ya kueneza itikadi za madhehebu ya Falun Gong, ambayo yanapingana na msimamo wa Serikali wa kuyataka madhehebu yote ya dini nchini humo yadhibitiwe na serikali. Alikuwa ameandaa maandamano makubwa ya kupinga unyanyasaji huo wa serikali ya China.

Wakati kiongozi huyo amehukumiwa kwenda jela kwa idadi hiyo ya miaka, hivi karibuni wafuasi wengine kadhaa walihukumiwa vifungo vya miaka kumi na minane jela kwa tuhuma zinazofanana na za kiongozi wao huyo.

Waumini wengine wapatao 300 wamefunguliwa mashitaka wakati hivi karibuni wengine wapatao 5000 walipelekwa katika makambi ya kutumikishwa kwa kazi.

Mvutano kati ya Serikali ya China na vikundi vya dini hauishii tu kwa Falun Gong, kwani hata baadhi ya waumini Kanisa Katoliki na madhehebu mengine yasiyotaka shughuli za dini zisimamiwe na serikali wamekuwa wakipata misuko suko mikali hususan katika miezi ya hivi karibuni.

Marekani yataka tafsiri ya ukimbizi ipanuiiwe

Washington, Marekani

MAREKANI imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutowatambua tu wakimbizi watokanao na vita waliokimbilia nje ya nchi zao, na badala yake iwatambue hata wale ambao kwa sababu za vita wamekosa au kuyaacha makazi yao japo wapo ndani ya mipaka ya nchi zao.

Hayo yameelezwa na Mwakilishi mmoja wa Marekani hivi karibuni wakati alipokuwa akihutubia Baraza hilo la Usalama hivi karibuni. Ilikuwa ni katika mjadala maalum wa Baraza hilo juu ya hali ya wakimbizi barani Afrika.

Alisema mtu yeyote anayekimbia makazi yake kwa sababu za mivutano ya kivita au kwa sababu za kijamii anapaswa kuhesabiwa kama mkimbizi, hata kama mtu amebaki ndani ya mipaka ya nchi yake.

Alifafanua kuwa hakuna tofauti kati ya mkimbizi aliyekimbilia nje ya nchi yake na yule wa ndani, na wote wanahitaji msaada wa kibinadamu kutoka kwa jumuiya yote ya kimataifa.

Mwakilishi huyo wa Marekani alisema kwamba hivi sasa dunia haina budi kuondokana na tafsiri iliyozoeleka kwamba mkimbizi ni mtu yule tu aliyekimbia kutoka mipaka ya nchi yake kwa sababu za kiusalama na kiuchumi katika nchi zao.