Vyama vya Siasa Sudan vyataka maoni juu ya kujitenga eneo la kusini

Khatoum, Sudan,

VYAMA vya kisiasa vya kusini mwa Sudan, pamoja na wanachama kadhaa wa chama tawala cha National Congress, vimetoa wito uanzishwe mwenendo wa kukusanya maoni ya raia juu ya kujitenga kwa eneo la kusini la nchi hiyo.

Habari zilizopatikana wiki hii zimesema kuwa ujumbe wa vyama vitatu ulikutana na Rais wa nchi hiyo Bw. Omar Hassan Al-Bashir, na kumkabidhi waraka wa wito wao, na Rais aliupokea wito huo.

Sudan imekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa kipindi cha miaka kumi na sita sasa vinavyowagonganisha Waislamu wa Kaskazini mwa nchi hiyo wanaofuata tamaduni za Kiarabu na Wakristo pamoja na dini za kienyeji wa eneo la kusini mwa Sudan. Inakadiriwa kuwa katika mapigano hayo zaidi ya watu milioni moja na lakini tano wamepoteza maisha na mamilioni ya wanawake na watoto kuteswa au kuachwa yatima.

Wakati huo huo mwishoni mwa wiki Marekani imeishutumu Serikali ya Sudan kwa kuwafadhili waasi wa Uganda wa Lords Resistance Army (LRA) ambao wamekuwa wakiendesha mapigano dhidi ya Serikali ya Rais Yoweri Museveni huko Kaskazini mwa nchi hiyo, mpakani na Sudan.

Mazungumzo ya Israel na Syria bado magumu

Washington, Marekani

HIVI karibuni Rais Bill Clinton wa Marekani aliweza kuwakutanisha kwa mara ya kwanza viongozi wa Israel na Syria kuzungumzia hali ya usalama katika eneo la Mashariki ya kati ikiwa ni pamoja na suala la Israel kutakiwa kuiachia milima ya Golan.

Mazungumzo hayo yanayowahusisha Waziri Mkuu wa Israel Bw. Ehud Barak na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Bw. Faouk Al-Shara, hata hivyo yameelezwa kuwa ni magumu ndiyo maana Marekani imewataka viongozi hao kuja na mitazamo mipya badala ya ile ambayo imekuwa ikikwamisha mazungumzo hayo tangu yalipovunjika na kusimamishwa mwaka 1996.

Jumatano iliyopita zilikutana Halmashauri mbili kati ya halmashauri nne zinazoshiriki katika mazungumzo hayo na kuna dalili kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Bibi Madeleine Albright, anaweza kumuomba tena Rais Bill Clinton ashiriki kikamilifu katika mazungumzo hayo katika hatua zake tete.

Halmashauri hizo zilijadili juu ya hali ya usalama baada ya kuhama kwa askari wa Israel kutoka milima ya Golan na kuimarisha mahusiano kati ya Israel na Syria.

Hata hivyo hadi Ijumaa iliyopita hapakuwa na taarifa zozote zilizotolewa kuelezea mafanikio yaliyokwishafikia katika mazungumzo hayo ya amani.

Mojawapo ya mambo yanayotiliwa mkazo zaidi na wasuluhishi wa Marekani ni kwamba Israel na Syria waweke wazi na kuafikiana kwanza juu ya wapi yalifikia mazungumzo yao ya mwaka 1996 yaliyovunjwa na Israel kufuatia mlolongo wa mashambulio ya mabomu iliyofanyiwa na Waislamu wenye itikadi kali

Urais wa Putin kuchujwa Machi mwaka huu

Moscow, Russia

Bunge la Russia limetangaza kuwa kura ya Urais itapigwa Machi 26, mwaka huu wakati haiba ya Kaimu Rais wa nchi hiyo Bw. Vladmir Putin, amepanda chati na kuwa katika nafasi nzuri ya ushindi hasa kutokana na usimamizi wake katika mapigano ya Russia dhidi ya waasi wa Chechnya. Bw. Putin aliteuliwa kushika Ukaimu Rais wakati Rais wa nchi hiyo Bw. Boris Yeltsin alipotangaza kung’atuka siku ya mkesha wa mwaka mpya wa 2000.

Hata hivyo mwishoni taarifa za katikati ya wiki zimesema kuwa vikosi vya waasi wa Chechnya vilifanya shambulio kali dhidi ya vikosi vya Russia na kufanikiwa kukomboa sehemu ya kusini ya mji mkuu wa Chechnya, Grozny, lakini Wizara ya Ulinzi ya Russia ilikanusha habari hizo.

Awaua kwa risasi watu 22 wa familia moja

Lima, Peru

.

MTU mmoja nchini Peru wiki hii aliwapiga risasi na kuwaua watu 22 wa familia moja ikiwa ni pamoja na watoto 15 kufuatia ugomvi juu ya hati za kurithi ardhi.

Watu walioshuhudia tukio hilo walisema mtu huyo aliwakusanya watu 15 ndani ya nyumba ktika kijiji cha Andes na kuwafyatulia risasi, wengi wao vichwani.

Mkasa huo umetajwa kuwa ni mmojawapo ilo mbaya sana nchini Peru ambako matukio ya watu kuuana kutokana na migogoro ya ardhi imekuwa ikitokea mara kwa mara kutokana na usimamizi dhaifu wa nchi hiyo katika masuala ya umiliki wa ardhi.