Ziara ya Papa alikozaliwa Nabii Abraham yakwama, ataenda kwa sala

lAtarajiwa kuwasili Misri katikati ya wiki

Vatican City,

ILE ziara ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo ll katika eneo la Uru ya Wakaldayo alikozaliwa Nabii wa kale Abrahamu haitakuwepo tena kwa sababu za kiusalama.

Badala yake imetangazwa mjini hapa kwamba Baba Mtakatifu atafanya ibada maalum kwa ajili ya suala hilo Jumatano ijayo, kabla ya kupanda ndege kesho yake na kuelekea Misri, ambako pia anafanya ziara ya kiroho.

Ziara hiyo ya Uru kusini mwa nchi ya Iraq, ilikuwa ni sehemu ya mfululizo wa ziara za Papa Yohane Paulo ll, katika maeneo muhimu ya kihistoria kwa mujibu wa Agano la Kale na Jipya vya Biblia. Papa aliwaambia mahujaji na watalii mwishoni mwa wiki mjini hapaa kuwa kwa vile hali ya kiusalama haimruhusu kutembelea kitongoji cha Uru, basi atatumia siku ambayo angepaswa kuwa huko kwa sala za kumkumbuka Abrahamu, ambaye ni Baba wa Taifa la Israeli na Baba wa Imani kwa Wakristo wa Agano Jipya.

Papa anatarajiwa kuondoka mjini Vatican kuelekea Misri Februari 24, mwaka huu, na akiwa huko anatarajiwa kupanda mlima Sinai ambako Nabii Musa alipokea Aamri Kumi kutoka kwa Mungu.

Baada ya ziara hiyo Papa akiwa huko huko Mashariki ya Kati atatembelea maeneo mengine ya kihistoria ya Jordan na nchi Takatifu ya Israeli, mwishoni mwa Machi.

Mapema Desemba, mwaka jana Serikali ya Irak, ilimtahadharisha Papa kwamba haina uhakika juu ya usalama wake katika ziara hiyo ya kutembelea eneo la Uru, nchini humo.

Kabla ya tahadhari hiyo timu ya watu kutoka Vatican ilienda Irak kumwandalia Papa mazingira mazuri ya ziara yake hiyo, lakini walikumbana na vikwazo kadhaa vy akidiplomasia ambavyo vilitia dosari uhakika kwamba kweli Papa angetembelea eneo hilo mwezi huu.

Serikali ya Irak, yenyewe imekuwa ikipendelea ziara hiyo iwepo, japo mataifa kama Marekani na Uingereza yalianza kupinga tangu ilipotangazwa, kwa madi kuwa ingeipa Irak kiburi.

Wapambe wa Bin Laden kizimbani nchini Yordani

WANAHARAKATI wa Kikundi cha Al Qaedah, kinachohusishwa na Gaidi la kimataifa la Kiislamu Osama Bin Laden wameshitakiwa kwa makosa mbali mbali ya ugaidi nchini Yordan.

Shirika la Habari la nchi hiyo Petra, lilisema mwishoni mwa wiki kuwa

watu hao wapatao kumi na wanne wanajumisha Muirak mmoja, Wajordani 12 na Mualgeria mmoja.

Kwa mujibu wa Shirika hilo la habari, magaidi wamekiri kuhusika na matukio kadhaa ya ugaidi.

Osama Bin Laden, ambaye ni Msaudia, amekuwa akiongoza kampeni za mashambulizi ya kigaidi katika maeneo mbali mbali duniani hususan dhidi ya Wamarekani na amekuwa akisakwa kwa uudi na uvumba na taifa hilo kubwa kwa muda mrefu sasa bila mafanikio.

Agosti 7, mwaka 1998 wapambe wa gaidi huyo walizishambulia kwa mabomu balozi za Marekani nchini Tanzania na Uganda na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 200 wasio na hatia katika eneo hilo la Afrika Mashariki.

Wakati huo huo; Rais wa Sudan Omar al -Bashir, alianza ziara nchini Saudia Arabia.

Ziara hiyo imeelezwa kuwa ni ya kuboresha uhusiano wa nchi hizo ambao uliharibika kutokana na uhasama kati ya Saudi Arabia na Irak, hususan baada ya Saudi Arabia kuwa na ukaribu na Mrekani ambayo ni hasisi mkubwa wa Irak.

Katika ziara hiyo Rais Omar al-Bashir, ameongozana na mawaziri wake kadhaa akiwemo wa Fedha.

Waandishi wa habari 86 waliuawa mwaka uliopita

 

 

Brussels, Viena

KATIKA mwaka uliopita wa 1999,zaidi ya waandishi wa habari 80 na wafanyakazi katika vyombo vya habari waliuawa na kuufanya mwakahuo kuwa mbaya zaidi ya iliyooita.

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni ya Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari (IFJ).

Katibu Mkuu wa shirikisho hilo Aidan White, amesema wanahabari na wafanyakazi katika vyombo vya habari waliouawa mwaka jana na miaka iliyopita, waliuawa kwa sababu mbali mbali kama wahanga wa visa vya migogoro mbali mbali.

Mwaka 1999 ulishuhudia vifo 86, ambapo 69 vilithibitishwa na 17 vingali katika uchunguzi.

Wengi kati waandishi hao waliuawa katika maasi ya Balkans, Rusia na Sierra Leone.

Taarifa hiyo inaonyesha kuwa waandishi wa habari 25 waliuawa huko katika Jamhuri ya Yugoslavia, ambapo 16 walikuwa wahanga wa mashambulizi ya mabomu ya NATO yaliyorushwa katika kituo cha televisheni cha Serbia huko Belgrade, Aprili, mwaka jana.

Waandishi wa habari na vyombo vya habari wamekuwa wakiuawa karibu kila penye machafuko.

Nchini India waandishi wa habari walijikuta hatarini katika mgogoro wa mipaka na Kashmir, wakati huko Checnya, Warusi walivishambulia kwa mabomu vituo vya habari.

Barani Afrika, vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Siarra Leone vilipoteza maisha ya waandishi wa habari wapatao 10 wa ndani ya nchi hiyo.

Hata hivyo taarifa hiyo imeonya kuwa waandishi wa habari wenyewe wanaweza kupunguza uadui kati yao na umma wowote kwa kuwa wakweli na waaminifu.

Taarifa ya IFJ imesema wakati mwingine waandishi hujisababishia kuuawa kwa kukubali kwao kutumiwa na baadhi ya watu kwa maslahi yao bila kuzingatia maadili.

Mimba zinazotolewa Ugiriki ni sawa na idadi ya watoto wanaozaliwa

Athens, Ugiriki

CHAMA cha Uzazi wa Mpango nchini Ugiriki kimesema idadi ya mimba zinazotolewa nchini Ugiriki ni sawa na ile ya watoto wanaozaliwa.

Taarifa za vyombo vya habari mwishoni mwa wiki zimesema kuwa japo idadi ya vitendo vya utoaji mimba nchini Ugiriki imepungua katika miaka ya karibuni, lakini bado kiwango kilichopo hivi sasa ni kikubwa kuliko nchi nyingine yoyote barani Ulaya na pengine duniani.

Katika mkutano uliofanyika hivi karibuni nchini humo, ilielezwa kuwa kati ya mimba 100,000 na 120,000 zinazotungwa nchini humo kwa mwaka hutolewa, wakti idadi ya watoto wanaozaliwa ni hiyo hiyo.