Waisraeli waishi chini ya ardhi kuhofia mashambulizi ya mabomu

lPapa aahidi kuiombea upatanisho awapo ziarani

Jerusalemu, Israeli

WAKAZI wa mji wa Kiryat Shmona, nchini Israeli wanaendelea kushi katika nyumba maalum zilizojengwa chini ya ardhi ili kujihami na tishio la mashambulizi kutoka kwa kikundi cha magaidi cha Hizbollah cha Lebanon.

Hali hiyo inafuatia mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Jeshi la Israeli linayoyafanya kusini mwa Lebanon,

kufuatia kikundi hicho cha Hizbollah kinachoungwa mkono na Iran kuwaua askari sita wa Israeli hivi karibuni.

Waziri wa Mawasiliano wa Israeli Bw. Binyamini Ben-Eliezer, alikaririwa akisema wiki hii kuwa mwaka jana askari wapatao 13 wa Israeli waliuawa na kikundi hicho cha Hizbollah, hivyo hatua ya hivi karibuni ya kufufua tena mauaji hayo haiwezi kufumbiwa macho na mamlaka ya kijeshi ya Israeli.

Mashambulizi ya Israeli huko Lebanon yalianza Jumanne iliyopita na tayari yameharibu maeneo kadhaa muhimu ikiwa ni pamoja na vituo vya umeme ambavyo vililipuliwa kwa mabomu.

Alhamisi iliyopita vyombo vya habari viliripoti kuwa ndege za Israeli ziliingia Lebanon na kushambulia meneneo kadhaa muhimu na kurejea salama.

Baraza la Usalama la Israeli limekutana mwishoni mwa wiki kupanga mbinu bora zaidi za mapambano huko Lebanon huku hofu ikiwa ingali imetanda miongoni mwa wananchi wanaohofia kushambuliwa na Hizbollah.

Waziri Mkuu wa Israeli Bw. Ehud Barak, amessisitiza wananchi wake kuendelea kujificha kwa vile bado hali si ya kuaminika.

Wakati hayo yakitendeka Baba Mtakatifu Yohane Paulo ll amesema ataiombea upatanisho nchi hiyo takatifu ya Israel katika ziara yake anayotarajia kuifanya Machi, mwaka huu nchini humo.

Habari za CNS kutoka Vatican zimesema Papa ametoa wito kwa Wakristo wengine wote kushirikiana naye katika maombi yake hayo.

 

Ziara za Papa zinasema mengi kuliko maneno

Vatican (CNS)

Baba Mtakatifu Yohane Paulo ll, anapowatembelea viongozi wengine wa kidini kokote duniani kama anavyotarajiwa kufanya hivi karibuni nchini Misri, ziara yake hiyo huwa na mafanikio makubwa kuliko vile mazungumzo ya mbali yanavyoweza kufanya kwa miaka kadhaa.

"Kuwepo kwa Papa mbele ya mtu hubadili fikra mtazamo na hali," Padre Roberto Tucci, ambaye amekuwa akimtangulia Papa katika ziara zake na kuongozana naye tangu mwaka 1982 amekaririwa na Shirika la Habari la Kanisa Katoliki la Vatican (CNS) akisema hivi karibuni.

Padre Tucci, alisema ukweli huo unathibitishwa pia na ziara za hivi karibuni za Papa alizozifanya huko nchini Romania na Georgia ambako alikutana na viongozi wa Kanisa la Kiorthodox.

Papa anatarajiwa kutembelea nchini Misri Februari 24 hadi 26, mwaka huu ambako atakutana na viongozi kadhaa wa kidini akiwemo kiongozi wa Kanisa la Waorthodox wa Koptiki 'Papa' Shenouda lll, na wakuu wa dini ya Kiislamu kabla ya kupanda mlima Sinai.

Mlei achaguliwa kuongoza Shirikisho la Makanisa

Bingerville (AANA)

BW. B.D. Amoa, wa nchini Ghana ambaye ni Mkristo wa Kawaida amekuwa Mkristo wa kwanza mlei kuchaguliwa kuliongoza Baraza la Shirikisho la Mabaraza ya Kikristo na Makanisa katika Afrika ya Magharibi-FECCIWA.

Uchaguzi huo ulifanyika hivi karibuni nchini Cote d'Ivoire, katika mji wa Bingerville .

FECCIWA ambayo ilianzishwa mwaka 1996 ikiwa imelenga katika kuimarisha mabaraza ya Kikristo katika eneo hilo la Afrika Magharibi, pamoja na kuchochea mazungumzo yanayoleta mahusiano mema na umoja miongoni mwa dini na madhehebu mbali mbali.

Shirikisho hilo pia lina jukumu la kuendeleza na kulinda amani, upatanishi, haki za binadamu na mambo kama hayo katika eneo lake.

Katika tamko lililotolewa katika uchaguzi huo FECCIWA ilisema ni lazima hadhi ya mwanadamu ilindwe kwani yeye ameumbwa kwa mfano wa Mungu.

"Ni lazima tuthibitishe kuwa ndugu zetu, dada na kaka wanakuwa vyombo vya mabadiliko ya kijamii na kupanua ushirikiano wetu na watu wa imani nyingine.

Shirikisho hilo pia pia katika tamko lake lilihamasisha kuondolewa kwa ubaguzi na kila aina ya ukatili na upendeleo katika jamii ikiwa ni pamoja na kuwajali wanawake.