Make your own free website on Tripod.com

Ziara ya Papa nchini Misri yasubiriwa kwa hamu

Roma ,Italia

VIONGOZI wa Kanisa Nchini Misri wamezipokea kwa furaha taarifa za matarajio ya Papa Yohane Paulo wa II kutembelea nchi hiyo yenye Waislam wengi mapema mwezi huu

"Hili ni tukio la kihistoria; nchi ya Kiislam ambapo Wakristo wachache waliopo karibu wote ni Waorthodoksi itamkaribisha Papa. Kwa vijana wetu itakuwa furaha na faraja" alisema Padri Ibrahim Isak Sedrach alipokuwa akiongea na Shirika la habari la Fides, hivi karibuni.

Padri Sedrach ni mkufunzi katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Leo mjini Cairo, ambako Papa anatarajiwa kufanya mazungumzo ya Kiekumenia katika ziara hiyo ya Februari 24 hadi 26, mwaka huu.

Mazungumzo hayo yanatarajiwa kutilia mkazo mahusiano mema kati ya jumuia ya Wakatoliki Waorthodoksi, Padri Boulos Garas, ambaye pia anafundisha katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Leo, alikaririwa akisema kuwa Wakatoliki wapatao 200,000 wameelezea kufurahishwa kwao na ziara hiyo ya Papa barani Afrika.

Alisema wengi walio mbali wamesema kwamba wako tayari kupanda garimoshi na kusafiri kwa zaidi ya saa 12 ili kushuhudia tukio hilo la Kihistoria.

Misri ni miongoni mwa nchi zenye Waislam wengi barani Afrika, lakini Rais wake Hosni Mubarak, ameweza kuweka hali ya usawa na mahusiano mema kati ya Wakristo na Waislamu licha ya vikundi vya Waislam wenye siasa kali kumshutumu na hata kulipua mabomu au kujaribu kumdhuru mara kadhaa.

 

Rais wa Sudan ahitaji msaada nchi za Kiarabu

Khatoum, Sudan

RAIS Omar Al- Bashir wa Sudan yuko katika ziara ya nchi za Kiarabu kwa lengo la kufufua mahusiano na nchi hizo yaliyokuwa yamedorora.

Habari zimesema pamoja na masuala ya Kimahusiano Rais Omar Al- Bashir pia anatumia ziara hiyo inayozihusisha pia nchi za Oman, Yemen, Libya na hata Misri kuomba msaada wa kiuchumi na kuungwa mkono Serikali yake katika msuala ya kisiasa.

Sudan imekuwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu katika eneo lake la kusini huku Serikali yake ikishutumiwa kuwanyanyasa Wakristo waishio eneo hilo.

Mahusiano na misaada ya nchi za Kiarabu kwa Sudan yaliathiriwa na kuvurugika kwa ushirikiano miongoni mwa nchi za Kiarabu katika miaka ya hivi karibuni kwa hiyo Rais Al- Bashir anataka kuitumia hali shwari iliyopo hivi sasa kuirejesha hali ya awali na zaidi kupata nguvu za kuwashinda wapinzani wake wa kisiasa.

 

Bilionea anayetaka mihadarati ihalalishwe ashutumiwa vikali

Washington, Marekani

GEORGE SOROS, bilionea maarufu wa kimataifa anayefanya kampeni ili madawa ya kulevya yahalalishwe kisheria kwa madai kwamba yatashuka thamani na kufunya yasishabikiwe na watumiaji kama ilivyo hivi sasa, ameshutumiwa vikali na magazeti mawili maarufu nchini Uingereza na Marekani.

Katika tahariri yake ya hivi karibuni gazeti la Sunday Times la Uingereza lilisema si ajabu kwamba kuna ongezeko la watu wanaounga mkono kuhalalishwa kwa mihadarati lakini kwa vile kuna pesa nyingi nyuma ya mpango huo.

Gazeti la Executive Intelligence Review, (EIR) la Marekani likiunga mkono hoja hiyo limemtaja moja kwa moja bilionea George Soros kama mtu anayemwaga pesa kutaka mihadarati ihalalishwe kisheria duniani kote.

Soros mwenyewe amekuwa akisema anataka kuhakikisha mihadarati inapatikana kwa bei nafuu mithili ya sigara ili kupunguza kiherehere cha watumiaji ambao baadaye wataona ni kitu cha kawaida.

Hata hivyo EIR toleo la hivi karibuni linasema huo ni upuuzi mtupu.

Gazeti hilo linasema bei ya chini itawavutia watumiaji wapya, Serikali zitageuka waenezaji wa mahadarati wale watumiaji ambao wakishaanza wakikosa wanaugua w Gazeti hilo pia katika toleo lake la Januari 21 mwaka huu lilibeba makala ndefu ikimshutumu Saros na wapambe wake katika kampeni nzito inayoungwa mkono na viongozi kadhaa wa Serikali huko Australia.

Nchini Australia kumekuwa na mjadala mkali miongoni mwa viongozi wa Serikali baadhi wakidai kuwa yafaa kuwa na huduma rasmi kwa ajili ya kuwachoma sindano walevi wa madawa ya kulevya aina ya Heroin katika miji ya Sydrey, Melbourne na mji mkuu wa Canberra.

Hata hivyo hatua hiyo imekuwa ikipigwa vikali kwani madhara ya Heroin yaliyokwishajitokeza ni makubwa na yanaendelea kukua.

 

Ulaya na Marekani zadaiwa kuwageuza Waarabu soko la silaha

Tehran, Iran

MATAIFA kadhaa ya bara la Ulaya na Marekani yameshutumiwa kwamba yamekuwa yakitengeneza kwa makusudi mazingira ya hofu miongoni mwa nchi za Kiarabu ili kuziuzia silaha.

Redio ya taifa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekaririwa ikisema mwishoni mwa wiki kuwa nchi hizo zikiwemo Ufaransa na Uingereza zimekuwa zikisingizia kwamba Iran ni tishio kwa usalama wa eneo la Ghuba na Uarabuni kwa ujumla na kufanikiwa kuziuzia nchi za Kiarabu ikiwemo Kuwait silaha.

Redio hiyo imesema wakati nchi za Ulaya na Marekani huzishawishi nchi hizo za Kiarabu ziamini kuwa silaha hizo zinaimarisha usalama, ukweli ni kwamba zinaongeza kiburi, hofu na kuhatarisha zaidi usalama wa eneo hilo.

Madai hayo yanasema hali hiyo pia inatoa mwanga kwa mataifa hayo ya Ulaya na Marekani kuingilia kwa urahisi masuala ya ndani ya wateja wao hao wa silaha.

Ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza nchini Kuwait, Februari 2, mwaka huu pia imehusishwa na jitihada za nchi hiyo kuimarisha soko lake la silaha kwa mujibu wa Redio ya Iran.