Make your own free website on Tripod.com

Kofi Annan ajitosa kusaida mgogoro wa Chechnya,Russia

Moscow, Russia

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan mwishoni mwa wiki aliwasili nchini Russia kwa ziara ya siku tatu ambapo anatarajiwa pamoja na mambo mengine kuzungumzia mashambulizi ya kijeshi ya Russia huko Chechnya.

Annan, ambaye hakuzungumza chochote na waandishi wa habari mara alipotua uwanja wa ndege, alikuwa anatarajiwa kukutana na Kaimu Rais Vladmir Putin kwa mara ya kwanza jana Ijumaa.

Putin alichukua madaraka ya Urais kutoka kwa Boris Yeltsin Desemba 31, mwaka jana.

Bw. Annan anatarajiwa kurejea wito wake na kuwepo kwa mazungumzo ya amani ili kumaliza mgogoro cha Chechnya ambako majeshi ya Russia yamekuwa yakiwashambulia waasi wanaotaka kujitengaa kwa jimbo hilo kwa miezi minne sasa.

Russia inawashutumu wapiganaji wa msituni wa Chechnya kwa kuendesha hujuma za ulipuaji wa mabomu na uhalifu mwingine katika ardhi ya Russia.

Hata hivyo, wapiganaji hao wa Chechnya wanakana kuhusika na milipuko hiyo ya mabomu.

Pia Annan, anatarajiwa kuzungumzia amani katika nchi ambazo zamani zilikuwa sehemu ya Russia zikiwemo Tajikistan, na jimbo la Abakhazia linalotaka kujitengaa na Geogria na jimbo la Nagomo -Karabakh lililojitenga kutoka Azerbaijan mwaka 1989.

Annan alitarajiwa kukutana na Spika wa Bunge dogo la Russia,Gennady Seleznyov.

Pia Annan alikutana katika mikutano tofauti na mkuu wa Idara ya Usalama ya Russia, Jenerali Vyacheslav Trubnikov, Waziri wa Mambo ya Nje Igor Ivanov na maafisa wa Umoja wa Mataifa waliopo mjini Moscow.

Leo Jumamosi atakutana na viongozi wa Kanisa la Orthodox kabla hajaondoka kwenda Geneva, Uswisi, ambako anatarajiwa kukutana na viongozi wa Wagiriki na Wagiriki- Wakuruputi (Greek Cypriots) na Waturuki-Wakuruputi (Turkish Chpriots).

Katibu huyo Mkuu wa Umoja wa Mataifa anatarajiwa kurejea New York, Marekani Jumanne ijayo.

Clinton amtabiria mkewe ushindi

WASHINGTON, Marekani

RAIS Bill Clinton wa Mare kani ametabiri kwamba mkewe, Hillary, atashinda katika uchaguzi wa useneta wa jimbo la New York.

Hata hivyo, Clinton amesema kuwa wapinzani wa mkewe katika kinyang'anyiro hicho, Rudy Giuliani, ambaye ni Meya wa jiji hilo, naye ana sifa zinazomwezesha kushinda.

"Nadhani wote ni wagombea shupavu," akasema Clinton katika mahojiano na atelivisheni moja.

"Wote wana rekodi nzuri ya mafanikio katika maisha yao kuhusiana na kuitumikia jamii," akaongeza.

Hata hivyo, Clinton akammwagia zaidi sifa mkewe ambaye anatarajiwa kutangaza kugombea kwake cheo hicho mwezi ujao.

"Mke wangu anastahili kufanya kazi hii ya unaseta," akaongeza "Nafikiri miaka yake 30 katika masuala ya utoaji elimu na afya kwa jamii, huduma kwa watoto imempa uzoefu mkubwa unaoweza kumsaidia kutekeleza majukumu ya useneta" ameongeza kusema Rais Clinton.

"Hii ndio maana nafikiri atashinda katika uchaguzi huo, ingawa pia sina maana kwamba mgombea mwenzake hafai kwa kazi hii" ameeleza.

Rais Clinton ambaye anaondoka madarakani januari 2001 baada ya kumaliza muda wake akasema kuwa anajaribu kuangalia jinsi atakavyoweza kumuunga mkono mkewe kama atashinda katika uchaguzi huo.

Clinton na mkewe wamenunua nyumba katika kitongoji cha Chappaqua jijini New York ili kumwezesha Bi. Clinton kuwa na sifa ya kugombea useneta wa jiji hilo.

Nafasi ya useneta na New York inaachwa wazi na Senata Daniel Patrick Moynihan wa chama cha Democratic ambaye anastaafu.

Kura za maoni zilizoendeshwa hivi karibuni zimeonyesha kwamba Bibi Clinton anaongoza kwa asilimia 49 dhidi ya mgombea mwenzake.