Ziara ya Clinton India yapokelewa kwa hisia tofauti na Makanisa

lBaadhi wadai Clinton ni muuaji

lMaskini wa India nao wasema ziara yake itazidi kuwapora haki zao

Catholic News Service, New Delhi

ZIARA ya Rais Bill Clinton wa Marekani iliyomalizika hivi karibuni katika nchi kadhaa za Asia, imepokelewa kwa hisia tofauti na vikundi vya makanisa nchini India.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kupitia shirika la habari la Kanisa Katoliki CNS taasisi ya "WaJesuit" ya India 'Jesuit run India Social Institute' imeelezea kuwa inaunga mkono vikundi vyote vilivyoipinga ziara ya Cliton wakati alipoitembelea India hivi karibuni.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini India, Father Donald D'souza amesema kuwa India pamoja na Kanisa ilimkaribisha Clinton wakati wa ziara yake kwa sababu ni kiongozi wa nchi, lakini pamoja na hayo kanisa na jamii nchini humo havikubaliani na matendo ya Marekani.

Father D'souza alieleza kuwa Kanisa nchini India linapinga vikali hatua inayoendelea kuchukuliwa Marekani ya kusambaza sera zake na kuweka dunia nzima chini ya himaya yake pasipo kujali kuwa hali ya maisha nchini India ni tofauti. Ameita hatua hiyo kuwa ya hatari kwa Wahindi wa ngazi ya chini kimaisha.

Naye Father Ambrose Pinto, ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Mambo ya Kijamii ya India "Indian Social Institute" amesema kuwa ni aibu kwa serikali kama ya India inayohimiza sera za kujitegemea kukaribisha mianya itakayopelekea sera za Magharibi za kutawaliwa kiuchumi kupenya na kuingia ndani ya India.

Father Pinto, pia amehoji kuhusu rekodi ya utendaji kazi wa Bill Clinton inayodhihirisha wazi kuwa hadumishi haki za binadamu hata kidogo. Ameeleza kuwa hilo linathibitishwa na maelfu ya watu waliochinjwa huko Irak, Yugoslavia na Sudan kwa jina lake.

Rais Bill Clinton, alitembelea jiji la New Delhi Machi 19 kwa ajili ya ziara ya siku 6 ambayo ilizihusisha nchi za Bangaladesh, India na Pakistan ambapo siku ya Machi 20 alielekea Dhaka Bangaladesh, na siku hiyo hiyo akaondoka Dhaka kurejea Marekani wakati wa alasiri.

Baada ya kukutana na viongozi wa kisiasa na viongozi wa wafanyabiashara wa India, kati ya Machi 21 na 22 Rais Clinton alitembelea mji wa kitalii wa Jaipur, ulioko Magharibi mwa India Machi 23. Miji mingine aliyoitembelea wakati wa ziara yake ni pamoja na Hayderabad ambao unaongoza kwa biashara na teknolojia ya Kompyuta kusini mwa India ambapo ziara yake pia ilimchukua mpaka Bombay, Magharibi mwa India.

Vishnu Hari Dalmia, Kiongozi wa Fungamano la Madhehebu ya Kihindu Duniani "World Hindu Forum" amesema kuwa wao waliipinga ziara ya Clinton kwa sababu Marekani inaendelea kuisaidia na kuiunga mkono Pakistani pamoja na kuwa nchi hiyo inaendelea kujihusisha na vitendo vya ugaidi wa Kiislamu.

Mapema Machi 19, vikundi vya maandamano ya hiari viliandamana kwenye mitaa ya mji mkuu wa India New Delhi, ambapo vilipeleka barua ya wazi kwa Balozi wa Marekani nchini India. Ndani ya barua yao vikundi hivyo vilidai kuwa Marekani imeteka Shirika la Fedha Duniani IMF, Fungamano la Wafanyabiashara Duniani WTO na Benki ya Dunia 'World Bank' ambapo inatumia vyombo hivyo kukandamiza nchi zingine duniani . Maandamano hayo pia yalikwenda sambamba na tukio la kuchomwa hadharani sanamu ya Bill Clinton na Bendera ya Marekani.

Aliyemuombea Papa laana ya kifo anashikiliwa na Polisi

lYadaiwa ndiye aliyemsomea dua ya laana Rabin

Catholic News Agency

POLISI nchini Israeli wamemhoji mtu mmoja anayedhaniwa kuwa kiongozi wa kikundi kilichofanya tambiko la kuomba dua mbaya ili kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Yohane Paulo wa Pili apatwe na laana ya kifo alipotembelea Israeli.

Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Israeli Shlomo Ben Ami amewaambia waandishi wa habari kuwa kiongozi wa kikundi hicho Meir Baranes alifikishwa polisi Machi 21 na kuwekwa chini ya uangalizi mkali.

Baranes pamoja na wenzake wa kikundi cha Wayahudi wa Kiorthodox wanatuhumiwa kuwa walimuombea dua mbaya Papa usiku wa Machi 16, katika sherehe waliyoifanya makaburini huko Safed, kaskazini mwa Israeli.

Televisheni ya Israel ilitoa picha iliyorekodiwa kwenye eneo la tambiko hilo kipindi kifupi kabla Papa hajawasili nchini Israeli.

Baada ya kukamatwa na polisi wanachama wa kikundi hicho walidai kuwa walitumia tambiko la aina hiyo linalojulikana kama 'Pulsa de Nura' ( michubuko ya moto) kumwombea dua mbaya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Israel Yitzhak Rabin na kipindi kifupi tu toka watambike alipigwa risasi na Yighal Amir.

Hata hivyo Waziri Ben Ami, amesema yeye binafsi hafikiri kama kikundi hicho ni tishio kiasi hicho kwa usalama nchini Israel isipokuwa waliwakamata wahusika kwa sababu walitoa vitisho.