Madhehebu ya Kilokole sasa marufuku nchini Rwanda

Durban, Afrika Kusini

SERIKALI nchini Rwanda, imesema itapiga marufuku mara moja vikundi vyote vya kilokole ili kuwaepusha wananchi wake na uwezekano wa kudanganywa na kusababishiwa maafa kama yale yaliyotokea nchini Uganda hivi karibuni.

Shirika la habari la Rwanda, ambayo ina idadi kubwa ya Wakatoliki, imemkariri Waziri wa Sheria na Uhusiano wa Taasisi Mbali mbali, akisema mwishoni mwa wiki kuwa Serikali yake itachukua hatua ya haraka ili kuwaepusha wananchi wake na mahubiri potofu ambayo yanweza kupelekea maafa ya raia wasio na hatia.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo mchujo mkali utafanywa ili kuhakikisha kwamba vikundi vya kilokole havipati usajili nchini humo, na vile vinavyotiliwa mashaka kufutwa.

Maafa yaliyotokea hivi karibuni nchini Uganda ambako waumini kadhaa wa madhehebu ya kilokole katika eneo la Kaungu, waoatao 800 waliuawa kwa kuchomwa moto na wengine kuuawa kikatili na kulundikwa katika makaburi makubwa ya pamoja, yameleta woga mkubwa nchini Rwanda.

Wakati huo huo: Nchini Uganda, Rais Yoweri Kaguta Museveni, amekaririwa mwishosni mwa wiki, nchini Uingereza, akisema kuwa Maafisa Usalama, nchini mwake walitoa tahadhari juu ya kuwepo uwezekano wa waumini wa madhehebu hayo ya Kurejesha Amri Kumi za Mungu, kusababisha maafa, lakini viongozi kadhaa wa Serikali hawakuzichukulia uzito taarifa hizo.

Sambamba na hayo, Polisi nchini Uganda wamesema kuwa wamegundua kaburi jingine kubwa la tatu katika uchunguzi wao dhidi ya mauaji ya kundi hilo la Wanamaombi.

Kaburi hilo, Polisi wamesema liko Kusini Magharibi mwa Uganda, ambako maiti 81 zimegunduliwa wakiwemo watoto 44.

Kaburi hilo limegunduliwa katika nyumba ya mfuasi mmoja wa dini hiyo, na inakadiriwa kuwa waumini hao waliuawa mwezi uliopita kabla ya wale waliochomwa moto wiki mbili zilizopita.

Kardinali atafuta mapadre kwa mtindo wa mabango

 

Chicago, Marekani,

KARDINALI Francis George, wa jimbo la Chicago, nchini Marekani ameanzisha kampeni maalum ya kuwahamasisha vijana kujiunga na upadre.

Kampeni hizo imeelezwa kuwa zinahusisha mabango makubwa makubwa ambayo yamebandikwa katika maeneo mbali mbali ya jimbo hilo.

Matangazo hayo yaliyoandikwa kwa lugha tatu yanasema kuwa, "Kama unangoja ishara kutoka kwa mungu ndipo uitikie wito wa kuwa padre, basi hii ndiyo ishara yenyewe."

Habari zimesema kuwa mabango hayo ambayo yamebadikiwa katika maeneo 12 jimboni humo, yatadumu hadi mwishoni mwa mwaka huu wa Jubilei Kuu ya Kanisa.

Mabango hayo ya kampeni ambayo ilizinduliwa mapema mwezi Machi, na Mwadhama Francis Kardinali George, yametafsiriwa katika lugha tatu ambazo ni Kiingereza, Kihispania na Kipolandi.

Askofu aliyetekwa Kongo kuachiwa huru

Bukavu, Congo

ASKOFU Mkuu Emanueli Kataliko, wa Jimbo Katoliki la Bukavu, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, anatarajiwa kuachiwa huru hivi karibuni.

Taarifa iliyomkariri kiongozi mmoja wa waasi wa Serikali ya Rais Laurent Kabila, wanaomshikilia mateka Askofu huyo, imesema kuwa kiongozi huyo wa kanisa atakuwa huru mara tu baada ya mazungumzo yanayoendelea kakamilika.

Viongozi wa waasi hao wamesema mambo yanacheleweshwa kuhakikisha kuwa utaratibu mzuri wa kumrejesha Askofu huyo unaandaliwa.

Kwa mujibu wa Padre Bosco, Bahama, wa Kanisa Katoliki, amesema anaamini kuwa Askofu huyo ataachiwa na waasi kwa kuwa ni mtu safi.

Waasi hao walimteka na kumshikilia Askofu huyo hivi karibuni kwa tuhuma kuwa alikuwa miongoni mwa watu wanaowahujumu.

Umoja wa Mataifa wavalia njuganjaa Afrika

Washington, Umoja wa Mataifa

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, amepetuma mjumbe maalumu katika Pembe ya Afrika kupanga hatua zitakazochukuliwa kufuatia tishio la njaa linalotarajiwa kuliathiri eneo hilo pamoja na sehemu ya Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa habari hizo watu wapatao milioni 16 wanakabiliwa na upungufu wa chakula katika eneo hilo.

Mjumbe huyo Bibi Catherine, ambaye ni Mkurungenzi Mtendaji wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP), tayari ameshazitembelea nchi za Ethiopia, Djibout, Kenya na Eritrea kwa muda wa siku 10.

Umoja wa Mataifa umesema kuwa tatizo hilo la njaa linalotokana na ukame linatarajiwa kuwa kubwa kama lile lililotokea miaka 15 iliyopita.

Uhaba huo wa chakula pia unatarajiwa kuziathiri nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi.