Kabila aruhusu Umoja wa Mataifa kuingiza walinzi nchini kwake

LUSAKA, Zambia

RAIS wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Laurent Desire Kabila, amebadili uamuzi wake juu ya mpango wa amani wa Kongo na amekubali kuwaruhusu walinda amani wa Umoja wa Mataifa kuingia nchini mwake.

Kwa mujibu wa Rais wa Zambia Fredrick Chiluba wakati akitoa ujumbe kwa waandishi wa habari katika ikulu ya nchini Zambia, amesema baada ya kushindwa kwa kikao cha Lusaka juu ya mgogoro wa DRC, hatimaye Rais Kabila amehakikisha ulinzi kwa vikosi vya Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo, Rais Chiluba hakueleza ni lini Rais Kabila alitoa uamuzi huo.

Jumanne iliyopita, Rais Kabila alikiacha kikao kikiwa kinaendelea kikiwa na viongozi wa mataifa 11 na viongozi wa waasi baada ya kutokubaliana na mpango wa kuvipeleka vikosi vya Umoja wa Mataifa kwenye maeneo yanayomilikiwa na serikali huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Rais Chiluba alisisitiza kuwa Rais Kabila hakujitenga na mkutano huo kwani alikuwa mchovu na alipoondoka alimuacha Waziri wake wa Mambo ya Nje.

Alisema pamoja na kwamba Rais Kabila amekubali kubadili uamuzi wake, hii haimaanishi kuwa amani imefikiwa na akautaka Umoja wa Mataifa kuelewa kuwa, suala kama hili si pekee kutokea barani Afrika baada ya makubaliano kutiwa saini kwani hata Mashariki ya Kati ama Timor ya Mashariki, ingawa makubaliano yamefikiwa, lakini mpigano bado yanaendelea.

Waasi wa Sudan kuwaachia mateka

KARTHOUM,Sudan

WAASI wa Sudan Peoples Labaration Front (FPLA) wamesema chama chao kitawachia huru mateka tisa wa vita katika mkoa wa Blue Nile unaoshikiliwa na waasi.

Kwa mujibu wa redio ya wapinzani hao wa Serikali ya Sudan, wafungwa hao wa kivita wataachiwa huru katika misingi ya kuheshimu haki za binadamu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka redio hiyo waasi wa FPLA, wamekwisha wasiliana na Shirika la Msalaba Mwekundu ili waweze kuwasilina na kuwajulisha ndugu na familia za mateka hao na kwamba usafiri kwa ajili ya kusafirisha, umekwisha andaliwa.

Kiongozi wa FPLA, Dk, John, aliagiza kuachiliwa kwa wafungwa hao wa kisiasa mapema wiki iliyopita.