Malawi yapata ziada ya tani milioni 1.8 za mahindi

BLANTYRE, Malawi

NCHI ya Malawi imevuka lengo la mavuno baada ya kupata tani milioni 2.5 za mahindi ikiwa ni matunda ya juhudi zake baada ya kuanzisha mpango wa kuwasaidia wakulima wadogowadogo kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Kwa mujibu wa maofisa wa kilimo wa nchini Malawi, mavuno katika kipindi cha miaka miwili yalikuwa yamevuka lengo lililowekwa la tani milioni 1.7.

Serikali ya Malawi imeuelezea mpango huo kama mwanzo mzuri wa wakulima wapya katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ambapo wakulima hao walipewa mbegu za kupanda, mbolea, madawa na ushauri wa kilimo.

IMF yaanza kuikopesha Kenya

NEWYORK, Marekani

BAADA ya kuzuia mikopo kwa muda wa miaka mitatu sasa, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF)limeanza kuikopesha tena nchi ya Kenya, likiidhinisha mkopo wa dola milioni 198 na kutoa zaidi ya dola milioni 14 kwa matumizi ya kuleta mageuzi.

Habari zinasema mkopo wa IFM, utachangia na kutasaidia kufungua milango ya nchi hiyo kupata mikopo mingine kutoka kwa wafadhili wengine wa kimataifa.

Baraza la Benki Kuu ya Dunia linatarajiwa kukutana wiki ijayo kuamua ikiwa lianzishe mfuko wa dola milioni 150 kwa mageuzi makuu ya kiuchumi.

Kwa mujibu wa msemaji wa IMF, lengo la mfuko wa miaka mitatu unaotolewa kwa Kenya ni kusaidia mageuzi ya kiuchumi.

Shirika la IMF, lilizuia mikopo ya Kenya tangu mwaka 1997 likilalamika kuwa Kenya ilitumia pesa hizo kinyume

'House girl' wenye Ukimwi Misri warudishwa makwao

CAIRO,Misri

MWANAMKE mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Jenifa, amerudishwa nchini kwao Ethiopia baada ya kugundulika kuwa ameathirika na virusi vya HIV, aliyeingia nchini humo kufanya kazi za ndani kwenye familia moja.

wiki iliyopita yaliripoti magazeti ya nchini Misri, kuwa wanawake 16 wenye virusi vya ugonjwa huo wasiojulikana uraia wao ambao wamekuwa wakifanya kazi nchini misri, walifunguliwa milango ya kutokea ili warudi katika nchi zao.

Wakizungumza juu ya mwanamke huyo, maofisa kadhaa wa Uwanja wa Ndege, wamesema, mwanamke huyo alirudishwa nyumbani kwao baada ya vipimo vya damu alivyofanyiwa kuonesha kuwa ana virusi vya ugonjwa hatari wa ukimwi.

Umoja wa Mataifa washangaa maafisa wake kuzuiliwa Kongo

NEWYORK Marekani

UMOJA wa Mataifa unatetea shughuli za maafisa wake katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Taarifa zilizotolewa na maafisa wa umoja huo walioko nchini Kongo, zinasema kuwa uamuzi huo unafuatia kitendo cha Serikali ya Rais Laurante Kabila kuzuia upelekwaji wa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa.

Msemaji wa umoja huo, Said El Hord, amesema watumishi wa Serikali ya Kongo wameunyima umoja huo haki ya kupeleka wanajeshi wake wenye silaha katika nchi hiyo.

Kufuatia uamuzi wa Serikali ya Kongo kuyakataa majeshi ya Umoja wa Mataifa yenye silaha, Umoja huo umesitisha upelekaji wake wa vikosi vya Tunisia ambavyo vingekuwa ni vya kwanza kuingizwa nchini humo.

Uamuzi huo pia unafuatia hotuba ya Rais Kabila kwa taifa lake kwamba Umoja wa Mataifa hautakiwi kuagiza wanajeshi wenye silaha katika mji ulioko Magharibi Kaskazini pamoja na Kinshasa.

Aidha habari za hivi karibuni zinasema kuna wasiwasi wa majeshi ya Rwanda na Uganda kupambana tena mjini Kisagani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Nchi hizo mbili zinawaunga mkono waasi kwa nia ya kufuata waasi wanaoyapinga mataifa hayo mawili.