MAZISHI YA PADRE KIJA

Mamia ya watu wamzika Padre Kija

Na Charles Hililla, Shinyanga

MAMIA ya watu kutoka ndani na nje ya nchi wamejitokeza kwa wingi kumzika aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Idara ya Mawasiliano katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania,Padre Norbet Kija aliyefariki dunia Septemba 19 na kuzika Septemba 22 mwaka huu Jimboni kwake Shinyanga.

Akizungumza katika kwenye misa ya mazishi ya Padre huyo,Askofu wa Jimbo la Shinyanga,Askofu Aloysius Balina alisema kuwa Binadamu siku zote anatakiwa kuishi maisha yanayompendeza Mungu ili kuleta heshima na maana ya uwepo wake hapa duniani kwani hajui siku wala saa atakayoitwa kwa Mungu

"Uwepo wa binadamu hapa duniani ni pamoja na kumjua Mungu na kufanya mambo yanayoendana na mapenzi yake na siyo kuishi kwa vile ulijikuta upo duniani"alionya Askofu Balina.

Askofu Balina alimtaja marehemu padre Kija kuwa alikuwa na tabia ya upole na unyenyekevu tabia ambayo alisema ni mfano wa kuigwa na jamii.

Aliendelea kusema kuwa moyo wa marehemu wa kuwafikiria zaidi na kujitoa kwa ajili ya wengine kuliko kujifikiria mwenyewe ni moja ya sifa zilizompa mafanikio katika shughuli zake mahali pote alipofanya kazi au kuhudumia.

Misa hiyo ya kumuombea marehemu padre Kija ilitanguliwa na ibada fupi ya kupokea mwili huo iliyofanyika nje ya mlango wa Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Shinyanga ambapo iliongozwa na padre Norbert Ngussa.

Baada ya ibada hiyo jeneza lililokuwa limewekwa mwili wa marehemu liliingizwa kanisani kwa ajili ya watu mbalimbali kutoa heshima zao za mwisho.

Marehemu Padre Kija amezikwa kwenye makaburi ya mapadri yaliyopo nyuma ya Kanisa Kuu Jimbo Katoliki la Shinyanga.