Make your own free website on Tripod.com

NGUVU YA HOJA Fr. P. Haule...

Watanzania tuko Maskini

WANAUCHUMI wa kimataifa hueleza kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi maskini ulimwenguni. Huo ni ukweli kwa namna fulani. Lakini ikiwa mgeni atafika na kuzuru Jiji la Da Es Salaam atashangaa kuona ni magari mangapi yanayotembea barabarani. Kama kuna shida katika Jiji hili ni wingi wa magari yanayosabisha watu kuchelewa kule waendako kwani barabara za Jiji karibu haziwezi kuhimili wingi wa magari.

Jiji lina magari mengi sana. Kuna magari mengi sana madogo madogo na tena ya fahari. Kuna wale wenye uwezo ambao wana zaidi ya magari mawili. Siku kwa siku magari huzidi kuongezeka hapa nchini. Kuna sehemu nyingi za maonyesho ya magari mapya na hata yale yaliyotumika kidogo ambayo huuzwa hapa na pale. Kuna pia magari makubwa mengi sana yenye kubeba mizingo mbalimbali katika makontena na hata katika magari yenyewe. Kuna matenka mengi yenye kubeba mafuta na kupeleka kule mikoani. Ni vigumu sana kwa mtu kuamini kama kweli nchi hii ni maskini akiona jinsi magari yanavyosongamana. Kuna magari hayo yanayosafirisha abiria hapa Jijini yajulikanayo Daladala na Vipaya. Hayo hayako tu hapa Jijini, bali karibu katika kila mjini.

Ukweli wa mambo ni kwamba kuna baadhi ya Watanzania ambao wana hela nyingi sana, na hivyo wana magari mengi sana. Licha ya kuwa na magari wanajenga nyumba kubwa sana za kifahari na papo hapo kuna Watanzania walio wengi ambao hali zao ni duni kabisa. Wako Watanzania ambao hawana uhakika wa chakula cha kila siku, lakini papo hapo kuna wengine ambao wanacheza na pesa. Tunaweza kusema kuwa kuna tofauti kubwa mno kati ya wale wenye uwezo na wale ambao hawana uwezo.

Mara kwa mara mtu anakuambia ninakwenda kuhangaika, yaani ninakwenda kujishughulisha. Jiji la Dar Es Salaam tunaambiwa kuwa ni mahali pa kutumia akili, ubongo. Hivyo Dar huitwa ni ‘bongo land’, yaani hapa wanaishi watu wanaotumia akili. Na hivyo ndivyo ilivyo kwamba bila kutumia akili siyo rahisi kuishi vizuri katika Jiji hili. Wale wenye kuhangaika au kuchakarika ndiyo wenye kuwa na nafuu katika maisha yao. Kuna watu ambao hufanya mahesabu kila siku ya mapato na matumizi, lakini pia kuna watu ambao hawafanyi hivyo na maisha yao huzidi kuwa duni. Wako wale ambao wanatumia akili na utashi wao katika kutenda kazi za kujipatia na kujiongezea kipato chao. Jambo linalotakiwa ni kwa mtu kutumia ubongo au akili yake pamoja na juhudi ili kuboresha maisha yake.

Kuna watu ambao wanajipatia utajiri kwa njia halali, lakini wako pia ambao hutumia njia ambazo si halali katika kujipatia utajiri. Neno kubwa ni kwamba kila mwananchi anapaswa kujihangaisha katika kujipatia cho chote. Yule mwenye kufanya kazi ofisini anapaswa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kukuza mapato katika ofisi yake. Lakini kwa kuwa siyo kila mmoja anaweza akaajiriwa, basi linalotakiwa ni katika kujiajiri. Yule mwenye kujiajiri anayo miiko ya utendaji katika kazi yake hiyo. Tunaweza kusema kuwa katika utendaji na kufanikiwa katika utendaji huo tunahitaji kuwa na nidhamu licha ya kutumia ubongo wetu.

Wako baadhi ya wananchi ambao hupenda sana kutumia njia rahisi katika kuboresha na kupata mahitaji yao ya kila siku. Nimewahi kushuhudia jinsi vijana wanavyokimbiza matenka na kujaribu kuchota mafuta kwa ajili ya kuwauzia madreva barabarani. Vitendo hivyo kusema kweli ni vya hatari sana kwa maisha. Hivyo pia kuna vitendo vingi vya aina hiyo wafanyavyo vijana katika kujipatia riziki zao za maisha kama vile ujambazi na uporaji wa mali za watu. Kuna vijana ambao hupoteza maisha yao kutokana njia rahisi wanazotumia katika kujipatia riziki zao.

Watanzania tumefikia mahali na kusema kuwa pesa ni ngumu sana na hivyo yataka mtu mwenye akili na juhudi kuipata. Hivyo ndivyo mambo yalivyo hapa nchini, kwani hatuwezi kusema kuwa hali ni mbaya sana kwa vile wako wale ambao wana hali nzuri sana na kila siku wanatembelea magari ya fahari, wanakula vizuri na hata kunywa vizuri. Lakini kwa hakika watu hao wanafanya kazi kwa bidii na maarifa.Kila siku wana mipango ya kuongeza na kuzalisha zaidi.

Ni jambo la kufurahisha sana kuona hata akina mama wanajishughulisha katika kazi mbalimbali za kujiongezea kipato. Wako wale ambao wanashughulika na mambo ya biashara wakiwa tayari hata kusafiri huko na huko ili kutafuta bidhaa za kuwafaa wateja hapa na pale. Wako akina baba ambao hawaoni vibaya kufanya kazi hata ya kupika chakula na kuuza. Katika kufanya hivyo hujipatia mahitaji yao ya kila siku na hata kuweza kumudu mambo mengi kama vile kuwasomesha watoto. Wananchi wengi wamefikia mahali ambapo husema kuwa hakuna kazi ya aibu mradi huleta kipato.

Kulikuwa wakati ambapo watu walikuwa wanachagua kazi, lakini siku ya leo sivyo. Watu hufanya kila kazi inayoweza kuleta kipato. Kwa hiyo tunapoona kuna nyumba nyingi za fahari kama vile kule Mbezi Beach na penginepo na kwamba watu hao wamekubali kufanya kaza za aina mbali mbali na hivyo zimewaletea kipato hicho. Tatizo lililopo ni kwamba kuna wananchi wengi ambao hawako tayari kuiga mifano ya wengine katika utendaji na utafutaji wa maisha nafuu. Bila kufungua macho na masikio katika kupata maarifa kutoka kwa wenzetu si rahisi tukaendelea.

Kwa upande fulani tumechelewa katika maendeleo ya nchi yetu kutokana na kuwa na hali ya uvivu. Wengi wetu tumepata misaada kutoka kwa wafadhili, lakini hatukuitumia misaada hiyo katika uzalishaji, na badala yake tumekula tu bila kufanyia cho chote cha maana. Kumekuwa na baadhi ya wananchi ambao wamefanikiwa kutumia misaada ya wahisani vizuri na hivyo hali zao siku ya leo ni njema kabisa. Kuna wengi ambao siku hizi wanastaafu kutokana na muujibu wa umri wao kazini. Lakini inashangaza sana kuona hali zao ni mbaya, kwa kuwa hawakutumia vizuri kile walichokuwa wakikipata katika kazi zao. Hao wamekuwa ni watu wa ‘kutoka mkononi kwenda mdomoni’ tu. Jambo hilo siyo zuri na hivyo maisha yao huzidi kuwa duni katika uzee wao.

Basi tunapenda kusema kuwa tunapaswa kutumia akili na nguvu zetu katika kujiongezea vipato vyetu ili maisha yetu yaweze kuwa mazuri. Hatuna sababu ya kuwa na hali mbaya ikiwa majirani zetu wako katika hali nzuri. Daima tuone wivu wa kimaendeleo tukuchukue hatua za kujiendeleza. Wale Warumi walikuwa na msemo: ‘Potuerunt hae, et potuerunt hi, quare non ego?’ Maana yake ni kwamba wamefaulu wao akina mama, wamefaulu wao akina baba, kwa nini na mimi nisifaulu?.