Make your own free website on Tripod.com

NGUVU YA HOJA Fr. P. Haule...

Malezi ya watoto wetu yasiwe lelemama

SIKU hizi kuna mjadala mkubwa sana kuhusu malezi ya watoto, na hasa juu ya adhabu za viboko. Kumekuwa na viongozi na watu mbalimbali wenye kulaani kabisa adhabu za vikobo kwa watoto na pia kuna viongozi na watu wengine binafsi wenye kusisitiza kuhusu adhabu hiyo ya viboko. Kila watu wamejitahidi kutoa hoja mbalimbali kuhusu suala hilo la malezi ya watoto wetu.

Kwa kuwa suala hilo linahusu jamii na wananchi kwa ujumla, sisi nasi tumeona ni wajibu wetu kusema machache juu ya jambo hilo. Kwa kuwa sisi ni Wakristo, basi tunapenda kuleta hoja yetu ambayo imo katika Maandiko Matakatifu. Tunasoma maneno yafuatayo kutoka katika Kitabu cha mwenye hekima Yoshua bin Sira, sura ya 30: "Ampendaye mwanawe atafululiza kumpiga, apate kumfurahia hatimaye...Amfundishaye mwnawe atamtia wivu adui yake, na mbele ya rafiki zake atamshangilia. Wenye kumtundua mwanawe na afunge jeraha zake, hata na moyo wake atafadhaika kwa kila kilio. Farasi asiyefungwa huwa mkaidi; na mwana aliyeachwa huwa mkorofi. Ukimkinaisha mtoto wako atakutia fadhaa, ukicheza naye atakuhuzunisha. Usicheke naye pamoja naye usije ukapata huzuni kwake; hatimaye ukasaga meno yako. Usimpe mamlaka yo yote wakati wa ujana wake, wala usiyaachilie mapumbavu yake. Uinamishe shingo yake maadamu yu kijana, umpige mbavuni wakati wa utoto wake; ili asije akawa mkaidi akakuasi, ikawamo huzuni moyoni mwake. Basi, umrudi mwanao na kujitahidi kwa ajili yake, ushupavu wake usije ukakuchukiza." (Yoshua bin Sira 30:1-13).

Hayo ni maneno ya mwenye hekima akiwa amefunuliwa na Mwenyezi Mungu na kwa hiyo ni maneno ambayo hayana ubishi. Hivyo pia ndivyo usemavyo ule msemo wa Kiingereza kuwa: ‘Spare the rod, spoil the child’. Maana yake yule asiyetaka kutumia fimbo atamharibu mtoto wake. Hayo mambo ndiyo tunayoyashuhudia siku hizi katika jamii yetu. Sote tunatambua kuwa watoto wetu na hasa vijana wetu wamo katika hali mbaya sana kitabia, kwani wamekosa malezi yanayotakiwa. Wazazi wengi wamewalea watoto wao katika hali ya kubembeleza na hivyo hawaogopi cho chote. Sasa hivi tuna matatizo makubwa sana na vijana wetu katika jamii yetu hii. Wazazi wengi hawako tayari kutoa adhabu kali kwa watoto na vijana wao na hivyo wana kiburi cha kupindukia na hawana adabu wala heshima kwa wakubwa na hata kwa wazazi wao.

Waswahili hutuambia kwamba majuto ni mjukuu, yaani mapato ya kutokuwa na hali ya ukali (kwa namna fulani) kwa watoto na vijana wetu baadaye hutuzalia majonzi tunayoyashuhudia siku hizi. Ni sharti tukumbuke kuwa kile tunachokipanda ni hicho ambacho tutakivuna. Ikiwa tunawalea watoto wetu kama mayai, tusishangae kabisa kuona baadaye wanatugeukia na hata kutufanya mambo ya ajabu. Mtoto hana budi kushikishwa adabu wakati akingali mdogo na papo hapo atambue kuwa adhabu anayopewa iwe ni viboko au kazi fulani, ni kwa ajili hasa ya kumjenga na kumsahihisha katika mambo yale mabaya aliyoyatenda. Adhabu haina budi kumrudi mtoto na kumwadibisha, yaani aache tabia au vitendo vibaya na kufanya mambo inavyopasika.

Kwa upande mwingine tunapaswa vile vile kuangalia namna ya kumwadhibu mtoto au kijana. Ni kweli kuwa kumetokea katika mashule na mahali pengine pa malezi, wale wenye kutoa adhabu wamefanya makosa hata ya kuwaua au kuharibu afya za wenye kuadhibiwa. Tunajua kuwa adhabu kama adhabu, kwanza inapaswa kuweka mwadhibiwa katika hali ya kutomchukia yule mwenye kumwadhibu, yaani atambue maana na umuhimu wa kuadhibiwa. Ikiwa mtoto au kijana baada ya kuadhibiwa anajenga chuki kwa ule aliyemwadhibu, hapo tuone kuwa huyo mwenye kuadhibiwa hajatambua maana ya adhabu. Kuna kiasi cha adhabu, na hivyo kumweka yule mwenye kupata adhabu kuendelea kumheshimu na kumpenda yule mwenye kumwadhibu. Lakini ikiwa adhabu itajenga chuki kati ya hao wawili, basi hapo lengo la adhabu litakuwa limepotoka.

Adhabu ya viboko imekuweko kutokea enzi za zamani kabisa. Tumesema kuwa yawezekana kwamba kukatumika adhabu nyingine badala ya mtoto au kijana kupigwa viboko. Lakini tunasema kuwa ni vema mtoto akapata adhabu ya kupigwa kwa makosa yale ambayo ni mabaya sana ili kuweza kutambua ubaya wa makosa hayo. Kuacha kuchapwa kwa watoto na vijana kutafanya jumuiya iwe na watu ambao hawatakuwa na woga wa kufanya mambo mabaya. Hatutaki kusema kuwa watoto wetu walelewe katika woga, lakini pale ambapo wanavunja sheria na kufanya mambo yasiyotakiwa inawapasa wapewe adhabu kali, na kati ya adhabu hizo kali mojawapo ni hiyo ya kuchapwa viboko.

Kwa hiyo tunapenda kutoa ushauri kwamba ni lazima watoto na vijana wetu waadhibiwe daima wanapokuwa wamekosa ili kuzisahihisha tabia na mienendo yao. Adhabu zitolewe kwa kulingana na makosa. Ni kweli kuwa kuna wazazi na walezi ambao wanatumia mdomo tu katika kuwaadhibu watoto na vijana wao, lakini hao ni wachache. Tunahitaji kabisa wazazi ambao wataw arudi watoto wao na siyo kuwalea kwa upole na kubeleza sana wakati wanapokuwa wamekosa.

Tunapoona kuna mmomonyoko katika jamii yetu tunapaswa kujiuliza kama kweli tunawalea watoto wetu vizuri ama sivyo. Njia mojawapo ya kuwalea watoto katika msingi mzuri, ni kuwadhibu pale wanapokuwa wamekosa, na hata ikiwezekana wapa adhabu ya viboko. Hatusemi kuwa kwa kila kosa mtoto apigwe viboko, bali pale linapotokea kosa kubwa. Adhabu hiyo sharti imfanye huyo mwadhibiwa asirudie tena kosa hilo kwa makusudi, labda iwe ni kwa bahati mbaya. Tunapaswa kutoa adhabu kwa watoto wetu katika kuwarudi tabia zao na pia kuwaadibisha, yaani wawe na tabia njema. Heshima ya watoto kwa wakubwa imefifia katika jamii yetu, na hivyo ni vema tukairudisha, hata kwa kutumia adhabu hii ya viboko. Ni dhahiri kuwa kumekuwa na malezi ya kilelemama kwa wazazi na walezi wengi katika jamii yetu, na hivyo tusishangae kuona kuna vijana wanowatukana watu hadharani, wanaodiriki hata kuwafanyia mambo mabaya wenzao.

Sisi tunasema kuwa mtoto akikosa aadhibiwe, na wala asiachwe kuadhibiwa au kukaripiwa. Ikiwa kosa ni kubwa, basi hapo anapaswa kupewa adhabu kubwa kulingana na ukubwa wa kosa hilo. Ikiwa mtoto au kijana amefanya kosa kubwa anapaswa kupewa adhabu ile ambayo itamkumbusha ubaya wa kosa hilo na hivyo kumfanya aogope kurudia tena kosa hilo. Kuto kumpa mtoto au kijana mhalifu adhabu yenye kulingana na kosa lake, hapo mambo yatakuwa mabaya kwa mzazi au mlezi mwenyewe, kwake yeye mwenyewe na pia kwa jamii. Adhabu zitolewe kulingana na makosa, na hivyo tunalaani kabisa ile tabia ya kumwadhibu mhalifu kupita kiasi.