Make your own free website on Tripod.com

NGUVU YA HOJA Fr. P. Haule...

Watoto wanahitaji michezo

KUMEKUWA na malalamiko makubwa sana hasa katika Miji na hasa katika Jiji letu la Dar Es Salaam kuhusu viwanja vya michezo kwa ajili ya watoto. Kuna sehemu nyingi ambazo hapo awali zilikuwa ni kwa ajili ya watoto waweze kucheza, sasa zimevamiwa na wakubwa ambao wamejenga nyumba na kunyang’anya viwanja hivyo vya michezo.

Tunaamini kwamba michezo ni kitu cha muhimu sana kwa ajili ya watoto, kwani mtoto asipopata nafasi ya kucheza maisha yake yatakuwa duni kabisa.Walezi wote wanatufundisha kwamba michezo kwa watoto ni muhimu sana kwa afya yao ya mwili na pia ya akili zao. Kwa hiyo tunaweza kusema kuwa michezo ni muhimu sana na hivyo ni lazima itiliwe mkazo kwa kila namna.

Hapo tungependa kutoa mwito katika nguvu ya hoja hii kwamba jumuiya inapaswa kuona umuhimu wa watoto kupata nafasi ya michezo. Hapo tungesema kuwa ni wajibu wa wajumbe wa mitaa, wa kata na hata taraja kuona kuwa watoto wanakuwa na mahali pazuri pa kuchezea. Inashangaza kuona sehemu nyingi za michezo kwa ajili ya watoto wamekuwa hasa ni sehemu za biashara mbalimbali. Tunavyofahamu ni kwamba wananchi wengi wanapenda michezo kama vile ile ya mpira wa miguu na ule wa vikapu. Lakini inashangaza kuona ni kwa jinsi gani watoto na vijana wadogo wanapewa misaada mbalimbali.

Ili kuweza kuwa na vijana wenye uwezo katika michezo jambo linalotakiwa ni kuwajenga wanamichezo hao kutoka wanapokuwa watoto. Na njia ya kuwajenga hao wanamichezo utotoni au ujanani mwao ni hasa katika kuwapatia sehemu za michezo zinazofaa. Ukipitapita mitaani utawaona watoto na vijana wanacheza katika viwanja ambavyo havikuandaliwa vizuri kwa michezo hiyo. Pia unashangaa kuona watoto wakichezea mipira iliyotengenezwa nao wenyewe bila utaalamu kabisa. Hapo lingekuwa ni jambo zuri kama wazazi na watu wazima wangewasaidia hao watoto kwa kuwapatia viwanja vizuri na pia kuwanunulia mipira inayofaa.

Watanzania tutaweza kuendeleza vijana wetu katika michezo ikiwa tunawahudumia hao watoto wetu. Wale watoto wenye vipaji vya michezo kama vile mpira wa miguu huonekana wakingali wadogo. Lakini tutawasaidia zaidi hasa ikiwa tunawapatia misaada ya hali na mali. Kwa hiyo tunapenda kutoa mwito kwa wale wenye uwezo kuangalia mahitaji ya michezo kwa watoto na vijana wetu. Tunafikia mahali na kunyang’anyana wachezaji kwa kuwa hatuchukui hatua za kufaa katika kuwaandaa watoto wetu kutokea umri mdogo tukiwapatia vifaa wanavyohitaji.

Ubingwa katika michezo hutokana na maandalizi ya kutoka utotoni na wala siyo katika ujana au utu uzima. Kwa hiyo tungependa kushauri kwamba timu za watoto na vijana ziimarishwe na wale watoto wenye kuonyesha vipaji vya pekee katika michezo fulani waendelezwe na kusaidiwa kwa hali na mali. Tukumbuke kuwa kushidwa kwa Watanzania katika michezo ya kitaifa na kimataifa, hutokana pia na maandalizi ya kutoka utotoni kwa wachezaji wetu. Tunapenda kupata matokea mazuri, na papo hapo hatuko tayari ‘kuinvesti’ katika michezo. Tunapenda kwenda kuangalia na kufurahia michezo huko viwanjani, lakini hatutoi michango kwa ajili ya uboreshaji wa viwanja vya michezo. Haiwezakani kuwapata wachezaji bora kutoka kwenye viwanja vibaya. Tusianze kuwafundisha watu wazima ikiwa hatukuwafunza wakati walipokuwa watoto.

Kwa hiyo tunaamini kwamba shule zetu zitazidi kuimarisha michezo na mahali pa michezo. Somo la michezo lisiwe la ziada bali ni la lazima katika ratiba ya shule. Watoto na wanafunzi sharti wapewe muda wa michezo na hivyo kugundua vipaji vya michezo kutoka utoto. Michezo sharti iwe ni sehemu muhimu sana kwa malezi kwani katika michezo mtoto hujifunza mambo mengi sana na hivyo hujenga tabia inayofaa. Kwa njia ya michezo watoto hujifunza jinsi ya kushirikiana, hujifunza namna kuvumiliana na pia jinsi ya kusaidiana. Ikiwa tabia hiyo imejengeka kutoka utotoni hapo tutaweza kuwa na matumaini kwamba vijana wetu watakuwa na ushirikiano ambao umejengeka kutokana na michezo, watakuwa na moyo wa kuvumilina kutokana na michezo na hiyo watakuwa na umoja katika shughuli zao za baadaye.

Sote tunatambua kuwa ni kwa njia ya michezo afya za watoto wetu huwa bora. Watoto wale ambao hawana michezo wanakuwa na afya mbaya kwa kawaida. Kwa hiyo kuna faida nyingi sana kutokana na michezo, na hiyo tunapaswa kuzingatia umuhimu wa michezo kwa watoto wetu kwani kukiwa na michezo nao watu wazima huburudika wakati wakiangalia. Tazama sasa ni kwa jinsi gani Jiji letu limepooza katika mambo ya michezo kwa sababu zile timu maarufu za Simba na Yanga hazichezi tena kwa ushindaji mkubwa na kuwa katika hali ya matatizo. Tunaweza kusema kuwa kwa namna moja au nyingine wetu wetu tumeshiriki katika kudhoofisha timu zetu hapa nchini kwa kutokuwa tayari kutoa misaada ya hali ya mali.

Ni jambo la kusikitisha kuona Watanzania wengi sasa hivi wamekuwa ni mashabiki wa michezo ya huko Ulaya, na kuacha kuwa mashabiki wa timu zetu hapa nchini kwa kuwa ziko katika hali duni sana. Lakini ukweli ni kwamba tunapaswa kujivunia chetu na siyo cha wenzetu. Na tukitaka kujivunia chetu imetupasa kabisa kukijenga kwa hali na mali. Ni fedheha kubwa sana kuona wengi wanakesha kwenye TV kuangalia mipira ya wenzetu huko Ulaya na penginepo na kudharau timu zetu badala ya kuzisaidia ili ziweze kuwa nzuri na za kujivunia. Tuwajenge watoto na vijana wetu ili nasi tuweze kujivunia timu zetu.

Kwetu sisi Watanzania tuna kila sababu ya kuweza kuandaa timu zetu za michezo na zikawa imara kabisa. Inakuwaje mataifa yale ambayo yamo siku zote katika hali ya machafuko na vita wanakuwa na timu nzuri za michezo, na sisi tunaoishi katika amani tunashindwa kuwa na timu nzuri za michezo. Taifa letu lina vijana wengi wenye nguvu, lakini huishia tu vijiweni na wangeweza kufanya shughuli hiyo ya michezo kwa kufanya mazoezi na kusaidiwa na jamii na hata tukawa na timu nyingi nzuri. Kuna Wilaya na hata Mikoa ambayo haina timu za maana za mpira wa miguu, wa mikono na hata riadha. Ni mambo ya aibu sana. Tumekuwa wavivu katika mambo ya kazi na pia hata katika mambo ya michezo. Tukumbuke kuwa ukiona kinaelea basi hapo ukumbuke kuwa kimeundwa, hivyo ukiona michezo ya wenzetu inapendeza basi ukumbuke kuwa wamefanya kazi ya kuandaa vijana wao kutokea utoto wao. Nasi hatuna budi kufanya hivyo!