Make your own free website on Tripod.com

NGUVU YA HOJA Fr. P. Haule...

Tutafute chanzo halisi cha matatizo yetu

SISI Watanzania tunakabiliwa na matatizo mengi mno katika taifa letu. Kwa mfano kuna matatizo ya ujambazi, kuna matatizo ya rushwa, tun a matatizo ya vijana wanaovuta bangi na kubugia madawa ya kulevya. Tuna matatizo ya ukosefu wa maadili kwa vijana na hata kwa watu wazima.

Pia tunayo matatizo ya magonjwa mbalimbali kama vile ukimwi, kipindupindu, nk.

Swali la kujiuliza ni hili, je, tunayatafutia uvumbuzi sahihi matatizo yetu hayo. Tunaonavyo sisi mara kwa mara wahusika au viongozi hutoa suluhisho la matatizo mbalimbali bila kuondoa kitu kinachoitwa "root-cause" ya hayo matatizo. Jambo linalotakiwa kufanya ni daima kutafuta hasa sababu msingi za matatizo yetu hayo. Tunapaswa kujiuliza kwa mfano kwa nini kuna majambazi mengi sana katika nchi yetu siku hizi? Je, ni jambo au hali gani ambayo inasababisha tuwe na wezi wenye kutumia nguvu, silaha, ujanja na ujeuri? Je, ni kwa nini vijana wetu wanavuta bangi, wanabugia madawa ya kulevya? Tunapaswa pia kujiuliza, je, ni kwa nini watu wanafanya vitendo vya udanganyifu katika maofisi na katika shughuli mbalimbali? Pia tunapaswa kujiuliza, je, ni kwa nini katika taifa letu maadili yanazidi kuporomoka siku kwa siku? Je, ni kwa nini tunazidi kukabiliwa na magonjwa sugu na yenye hatari kubwa sana kwa maisha yetu, kama vile ukimwi?

Hayo ni baadhi ya maswali ambayo tunapaswa kujiuliza sana ili tuweze kuondokana, na hata walao kupunguza matatizo hayo. Kwa haraka kabisa tunaweza kusema kuwa matatizo yetu mengi kwa vikubwa hutokana na uchumi wetu mbovu yaani umaskini. Kwa hiyo "root-cause" ya matatizo yetu sisi Watanzania ya kwanza kabisa ni umaskini tulio nao. Hakuna asiyetambua kuwa nchi yetu ni kati ya nchi zile zenye umaskini wa kutupwa katika ulimwengu huu. Na je, huo umaskini unatokana na nini hasa? Hapo tunaona kuwa "root-cause" ya umaskini wetu kwa wengi ni kutokana na umaskini pamoja na ukosefu wa nyenzo za kutendea kazi. Nchi yetu kwa vikubwa hutegemea sana kilimo, lakini ni kwa kiasi gani kilimo kinatiliwa mkazo siyo kwa maneno tu bali kwa vitendo. Ni kwa jinsi gani wakulima wanasaidiwa kwa hali na mali ili waweze kuzalisha sana huko mashambani na vijijini.

Ni kweli kuwa kuna jitihada kubwa sana ya kusaidia vikundi mbalimbali vya uzalishaji, lakini mambo huwa si kwa vikubwa sana kama hela zinavyotumiaka katika mambo ya siasa. Nchi yetu bado inawathamini sana wanasiasa wenye kupigapiga maneno na kutowahudumia vilivyo wakulima na wazalishaji wengine. Je, ni marupurupu kiasi gani wanapewa wanasiasa kwa sababu ya kusemasema huko bungeni, na papo hapo wakulima hawahudumiwi vilivyo. Hatusemi kuwa wanasiasa wetu hawana maana, lakini tunachotaka kusema ni kwamba ingekuwa nzuri zaidi kuwasaidia na kuwapa mikopo ya kueleweka hao wakulima na wenye shughuli mbalimbali katika vikundi.

Ni kutokana na umaskini vijana wetu wanajiingiza katika mambo yasiyo na maadili yaani vitendo vichafu. Akina dada zetu wanaingia katika mambo ya ukahaba kutokana na umasikini, na hivyo wanaona njia rahisi ni kuwa akina changudoa na hivyo kuiuza miili yao. Mapato yake ni kueneza magonjwa ya zinaa pamoja na gonjwa baya sana la ukimwi. Kama umaskini ungeondoka, au walao ungepungua, na magonjwa mengi yangepungua. Watu wengi wanaingia katika vishwawishi vya kupokea au kutoa rushwa kutokana na umaskini tulio nao. Kuna mwenye kutoa rushwa ili aweze kupata chochote zaidi, na hivyo kuna mwenye kupokea rushwa ili aweze kuwa na kitu zaidi. Hayo yote husababishwa na umaskini, na hivyo pale ambapo hakuna rushwa ni kwamba kuna hali ya uchumi yenye unafuu.

Lakini tena tunapaswa kujiuliza, je, umaskini wetu huo tutauondoaje? Kwanza kabisa wananchi wanapaswa kufanya kazi kufa na kupona ili kuweza kuinua hali hiyo ya uchumi pamoja na serikali kutoa misaada ya vitendea kazi kama vile nyenzo na pembejeo. Kwa upande mwingine serikali hapa na pale ilikuwa imejitahidi sana kuwasaidia wakulima lakini kwa bahati mbaya misaada hiyo haikutumika ipasavyo na mapato yake hali zikazidi kuwa duni. Kumbe jambo jingine linalotakiwa ni kwamba lazima kutumia mambo yale tuliyo nayo ipasasavyo.

Jambo jingine ambalo ni kweli msingi wa matatizo yetu ni tabia mbaya ya uzembe katika utendaji wetu wa shughuli mbalimbali. Sisi Watanzania hatutaweza kumwe kuondokana na tatizo la umaskini ikiwa hatutakuwa na moyo wa kujituma na kufanya kazi kwa bidii. Kama tulivyokwisha kusema katika safu yetu hapo awali, ni kwamba Watanzania wengi ni "wavivu" pindukia. Wananchi wengi sana hawapendi kujituma na kufanya kazi kwa bidii. Nchi yetu tunaambiwa ina vijana wengi sana, lakini asili mia kubwa hawatumii kabisa nguvu kazi kwa ajili ya kujiendeleza. Badala yake tunaona jinsi wanavyojiingiza katika vitendo vichafu vya unyang’anyi, ujambazi na wizi wa kila aina. Kumbe tena chanzo asili cha umaskini ni uvivu wa kupindukia.

Mambo yamedhihirika hasa katika zoezi la ubinafsishaji wa mashiraka yetu. Wale ambao wameyachukua mashika hayo wame waajiri watu wao ambao wanafanya kazi kwa bidii kabisa. Na kwa sababu ya bidii yao katika utendaji, tunaona ni kwa jinsi gani wanalipwa mishahara mizuri, na hivyo kuondokana na umaskini. Wananchi wengi wanakuwa ni wategaji katika kazi na hivyo kusababisha mashirika mengi kuzidi kuzorota na hata kuanguka. Kwa sababu ya kukosa uaminifu na kuwa na usimamizi mbovu, pamoja na uvivu viwanda vyetu vingi vimepasika kufungwa na hivyo kuleta ukosefu wa ajira kwa wananchi wengi.

Tunaweza kusema kuwa sababu nyingine ya msingi katika hali duni ya maisha ya Watanzania wengi hutokana na ukosefu wa misingi ya maadili. Ukosefu wa maadili hutokana na ukosefu wa malezi na mafundisho ya kidini ndani ya familia, ndani ya jamii na ndani ya taifa letu. Vijana wengi na hata watu wazima wanakosa ile dhamiri ya kweli, yaani hakuna kitu kinachowahangaisha ndani mioyo yao na hivyo kufanya mambo hata yaliyo kinyume cha ubinadamu.Malezi ya kimaadili hudai hasa kuwa na dhamiri ambayo ni kilio cha moyo chenye kulia daima mtu anapotenda jambo baya, na papo hapo ni chenye kumsifu na kumwondolea mahangaika wakati akitenda jambo jema. Kwa hiyo kwa sasa hivi watu wengi wamefisha dhamiri zao na hivyo hawaoni vibaya kutenda mambo machafu na tena ya aibu kwa siri na hata hadharani. Kila siku tunasikia na kusoma kutoka vyombo vya habari jinsi watu wanavyofanya maovu bila aibu.

Hatuwezi kutarajia kwamba yule mtu ambaye anamcha Mungu, kila siku ya ibada anakwenda mahali pa ibada takatifu na kulishwa Neno la Mungu au kupokea mawaidha ya kidini, atakuwa kweli mzembe na mchafu. Lakini wengi wanakuwa na tabia chafu kutokana hasa na kutomwogopa Mungu na hivyo kuwa na dhamiri iliyokufa ambayo haiwezi tena kuona uchungu kwa sababu ya makosa mbalimbali anayoyafanya binadamu.

Tunapenda kumalizia Nguvu yetu hii ya Hoja kwa kurudia tena kuwasihi wananchi kwamba maendeleo ni kitu cha kukazania. Hatuweze kamwe kupata maendeleo ya kweli na ufanisi katika shughuli zetu mbalimbali ikiwa hatufanyi kazi kwa bidii. Na kwa upande wa viongozi daima wakumbuke kuwa ni wajibu wao kuwahangaikia raia wao hasa wale walioko kuli vijijini. Tutaweza kutoa adhabu kwa wahalifu kwa kadiri tuwezavyo, lakini hatutakomiesha uhalifu bila kuinua hali ya maisha ya kila mwananchi kiuchumi na kidhamiri.