NGUVU YA HOJA Fr. P. Haule...

Elimu hupatikana kwa jasho

KUNA mahitaji mengi sana kwa ajili ya binadamu ili aweze kuishi maisha ya furaha na pia maadilifu. Hitaji mojawapo kwa binadamu ni lile la kujipatia elimu na maarifa.

Binadamu anapasawa kujifunza mambo mbalimbali ili aweze kuishi vizuri.

Kuna mambo mengi ya kujifunza na pia kuna njia nyingi za kujifunza. Binadamu awapo mdogo kabisa hujifunza mambo mengi kutoka kwa wazazi wake na pia kwa majirani wanaomzunguka.

Kwa hiyo wazazi na majirani ni walimu wa kwanzakwanza kwa watoto.

Kadiri mtoto anavyokuwa na kuongezeka hivyo pia huzidi kupata mafunzo na maarifa kutoka kwa watu wengine.

Hapo zamani vijana wengi walifunzwa mambo ya ufundi kutoka au kwa wazazi wao au kwa wale waliokuwa karibu yao. Waliweza kujifunza jinsi ya kujenga nyumba, jinsi ya kuvua samaki kwa wale waliokuwa wanaishi karibu na bahari au maziwa. Walijifunza ufundi wa kufuma, kutengeneza vyungu, kupika pombe na kadhalika.

Baada ya kuingiliwa na ustaarabu wa kigeni tumekuwa na shule ambazo zimekuwa zikiwafundisha watoto na vijana na hata watu wazima maarifa mbalimbali. Kumekuwa na shule za awali ambamo watoto wanafundishwa jinsi ya kusoma na kuandika. Kumekuwa na shule za sekondari na vyuo pamoja na vyuo vikuu.

Vile vile kumekuwa na zile shule za ufundi na kilimo ambamo vijana wanafundishwa mambo hayo mbalimbali.

Elimu kama elimu ni kitu ambacho mtu hujipatia kwa kutumia akili na juhudi zake mwenyewe.

Haiwezekani mtu akasoma na kupata elimu kwa kutumia akili ya mtu mwingine. Ikiwa mtu anafanya hivyo, basi hapo tunaweza kusema kwamba huyo mtu haelewi maana halisi ya elimu.

Ni jambo la kusikitisha sana kusikia kuwa kuna wanafunzi ambao wanatumia vyeti vya wengine katika kuingia Chuo Kikuu.

Hivi karibu tumesikia kwamba kuna wanafunzi wenzi ambao wamekuwa wanaleta vyeti ambavyo si halali na wala siyo vya kwao ili kujiunga na Chuo Kikuu.

Tunasema jambo hilo ni la aibu kabisa na pia ni la hatari katika elimu kwa taifa letu.

Vitendo hivyo vinaweza kulinganishwa na kile kitendo cha mtu kuwa tayari kutimiza adhabu ambayo amepewa mtu mwingine, yaani kwa mfano kukubali kupigwa viboko kwa ajili ya kutimiza adhabu ya rafiki aliyeadhibiwa kupigwa viboko hivyo.

Adhabu hiyo haitamsaidia kamwe huyo mhalifu.

Hivyo pia kutumia cheti cha mwingine ambacho hakukitolea jasho ni jambo la udanganyifu mkubwa sana.

Lakini zaidi ni hasara kwake mhalifu mwenyewe na pia kwa taifa nzima. Tunaweza kujivuna kuwa tumekuwa na wasomi wengi kumbe ni akina "kihiyo" tu.

Hali hiyo imekuwa ikiota mizizi sana katika taifa letu hasa tunapokumbuka jinsi mitihani inavyovuja na kuibiwa.

Tunaamini kwamba yule mwenye kufanya ujeuri katika mitihani na katika masomo huliletea hasara kwanza taifa letu.

Tunafikiri kwamba tunao wataalamu ambao wamesoma vizuri kumbe wameibia hivyo vyeti.

Kwa kawaida watu wa namna hiyo kwa sababu wanajua kudanganya basi watadanganya hadi wanapewa madaraka makubwa sana katika taifa letu.

Mapato yake ni watu hao kutoweza kutekeleza wajibu wao na badala yake huwa wazembe, wakatili, hawataki kushauriwa kwa sababu si wanyofu na wala waadilifu.

Kwa kawaida mtu yule aliyepata elimu kwa jasho huwa ni mwadilifu na pia mwaminifu katika utendaji wake.

Taifa letu linao watu ambao wamedanganya sana katika kujipatia vyetu, bila kujipatia elimu na maarifa yenye kulingana na vyetu hivyo.

Pengine ni afadhali mtu akakosa cheti, lakini akawa na maarifa ya kufanyia kazi kwa ufanisi.

Tungependa kuwakanya kabisa wale vijana, hasa watoto wa wenye uwezo kutokutumia pesa kununua vyeti na baadaye kuleta hasara ya utendaji mbaya wa kazi zile ambazo wamekabidhiwa na umma.

Naupenda sana ule msemo usemao, soma ule, yaani lazima kwanza mtu atoke jasho na ndipo afurahie pato la jasho lake. Kwa wale waliosoma, wakajiandaa vizuri kwa mitihani yao, na kisha wakafaulu vizuri katika mitihani, huwa ni jambo la kufurahisha kweli kweli wapopokea vyeti vyao.Hilo linakuwa ni tenda la faraja kubwa mno, lakini hao wanaoiba mitihani au vyeti, nyoyo zao daima huwa katika hali ya wasi wasi.

Tunaposema kuwa katika taifa letu tunao wasomi, basi iwe kweli ni wasomi ambao wamatoka jasho katika masomo yao na wala siyo wale ambao wamakuwa nusu kwenye masomo na nusu kwenye starehe mbalimbali na hivyo kudanganya walimu wao. Vitendo hivyo vya wizi na udanganyifu katika mambo ya elimu vinatupunguzia hadhi yetu katika ulimwengu wa wasomi. Hatuna budi kuvikomesha kabisa kwa kila hali.

Tunasema kuwa elimu ni ufunguo wa maisha tuna maana kwamba sharti tuwe na elimu inayopatikana kwa njia ya kutoka jasho sisi wenyewe na wala ya kuiba kutoka kwa wengine.

Elimu kama elimu ni kitu ambacho kinakuwa ni sehemu ya binadamu, ni kama vile damu yetu sisi wenyewe.

Ingawaje kuna watu wanaweza kuishi kwa kutumia damu ya watu wengine, lakini mtu hawezi akafanya kazi kwa kutumia elimu ya mtu mwingine. Hivyo tunasema pia kuwa akili ni kama nywele na hivyo kila moja ana za kwake na hizo ndizo anapaswa kuzitumia. Wengi hatupenda kutumia nywele bandia, lakini zaidi vyeti bandia havifai kabisa.