NGUVU YA HOJA Fr. P. Haule...

Tunapaswa kujua tunakwenda wapi

KUNA msemo usemao kuwa kama mtu hajui anakokwenda, hataweza kufahamu kama ameshafika kule aendako au sivyo. Hivyo ndivyo inavyotakiwa kuwa katika shughuli zetu mbalimbali za maendeleo.

Yeyote anayetaka kufanya jambo la maendeleo hana budi kulifanyia mpango na kujua kwa dhati anataka nini, na hivyo anachokitarajia kitakuwa na faida gani kwake yeye binafsi, kwa familia yake na pia kwa jamii hasa ile inayomzunguka. Kwa maneno mengine ni kwamba daima inatupasa kuwa na malengo ya kunuiwa katika utendaji wetu. Bila kuweka malengo ya utendaji wetu, itakuwa ni kweli vigumu sana kuelewa kama tunafanikiwa ama sivyo.

Tumeanza mwaka mpya wa 2000, na tungetarajia kwamba kila mwananchi na kila binadamu mwenye akili na utashi atakuwa amejiwekea malengo yake. Tunaposema kuhusu malengo ya utendaji wetu, ni kwamba tunataka kusema kuwa tumeshaamua kufanya nini katika muda fulani wa mwaka huu. Yawezekana kuna baadhi yetu wameamua kwa mwaka huu kujenga na kukamilisha nyumba zao za kuishi. Hapo tunatumaini yatafanyika maandalizi mathubuti kulingana na muda walioupanga. Labda mwezi wa kwanza ni kuandaa bati, mwezi wa pili labda ni kununua simenti, mwezi unaofuata labda ni kununua mbao. Na baada ya hapo ni kuanza kujenga kabisa msingi wa nyumba. Hapo tunaweza kutaraji kwamba ifikapo mwezi fulani nyumba itakuwa tayari.

Yawezekana kuna mwingine ameamua kuanza biashara labda ya duka.

Naye huyu ataanza na maandalizi ya kutafuta mtaji labda kwa mkopo kutoka benki au mahali pengine.

Ataandaa nyumba ya kufanyia biashara, atanunua vitu kidogo kidogo, na kisha atakamilisha mambo ya liseni na tarehe iliyopangwa ataanza biashara hiyo. Jambo kubwa la kukumbuka ni kwamba tukitaka kufanikiwa katika mipango yetu au hasa katika mambo ya miradi, hatuna budi kuandaa vitu kwa taratibu. Tunapoandaa vifaa maana yake tunatekeleza mipango ambayo tumejiwekea ili kufikia lengo tulilokusudia.

Ni jambo la kusikitisha kuona wako wananchi wengi ambao hawafanyi maandalizi ya kutosha katika utendaji wao. Miradi yetu mingi inakwama na kushindwa kufikia mwisho wake kwa sababu ya kukosa maandalizi mazuri ambayo huenda pamoja na mipango thabiti. Kuna wengi wanaanza ujenzi wa nyumba, lakini hawafiki mwishoni na kukamilisha ujenzi huo kutokana hasa na kutofanya maandalizi kikamilifu. Daima tukishafanya maandalizi, tunapaswa kuwa na nidhamu ya kufuata hayo ambayo tumeyapanga. Ikiwa tumeamua kufanya biashara, tunapaswa kujinyima mambo fulani ili kuweza kukamilisha mpango wetu huo wa biashara. Haiwezekani kabisa tukaanza shughuli ya biashara na papo hapo tunaendelea na starehe.

Wale wataalamu wa maisha walisema kuwa ni vigumu sana kushughulikia vyuma vingi katika kazi ya utengenezaji wa hivyo vyuma ikiwa kuna vyuma vingi mno ndani ya moto. Kwa hiyo tuwe na vitu vichache vya kutenda kwa wakati mmoja.

Haifai kuwa na mipango mingi kwa wakati mmoja. Linalotakiwa ni kuwa na mpango mmoja na baada ya kuumaliza mpango huo, basi tunaweza kuanza mipango mwingine. Tunataraji kwamba wananchi wengi katika mwaka huu watajiwekea malengo ambayo siyo mengi, bali ni thabiti kabisa. Ni vema tukawa na mipango au miradi michache, kuliko kuanzisha miradi mingi na kuwa na mipango mingi ambayo haifikii mwisho wake kwa sababu tu nguvu kazi imetawanyika.

Uko msemo mwingine usemao kuwa kila mmoja anapaswa kushona nguo kwa kadiri ya kitambaa alicho nacho. Na hivyo katika mambo ya miradi au mambo yetu ya maendeleo. Tunapaswa kufanya miradi kulingana na mitaji au raslimali tulizo nazo. Tusifanye mipango mikubwa ambayo inapita uwezo wetu kifedha. Kuna watu waliamua kujenga majumba makubwa kabisa, lakini kumbe hawakuona mbele, na hivyo majumba hayo hayakuweza kumalizika na yamebakia kuwa kama magofi.

Ni jambo la aibu sana kuona nyumba kubwa ilianza vizuri lakini haikumalizika vizuri.

Tatizo ni kwamba kuna watu wengi ambao hujenga nyumba siyo kwa kutumia stoo, bali huenda mara kwa mara dukani na kununua vifaa wanavyohitaji kimoja kimoja.

Lakini kama wangetayarisha kila kitu na kufanya mahesabu vizuri, hawangeingia katika aibu hizo za kutoweza kumaliza miradi yao vizuri. Kuwa na mipango maana yake ni kufahamu wapi mtu anakwenda au amekusudia kwenda.

Binadamu mwenye akili na utashi anapaswa kuwa na mipango katika utendaji wake na wala kusiwe na tabia ya kubahatisha kama tulivyosema hapo juu. Mtu yule anayebahatisha katika utendaji, mara nyingi hafikii lengo lake na hapati mafanikio anayotarajia. Kuna wananchi wengi wamekuwa wakibahatisha katika utendaji na miradi yao, na mapato yake ni kwamba kumekuwa na mafanikio hafifu sana, na pengine hapakuwa na mafanikio yo yote yale. Katika kila mpango wa kimaendeleo inatakiwa kabisa kujifunga kibwebwe, yaani kuwa na ni thabiti na hivyo kufanya kila jitihada ili kukamilisha mpango huo.

Kwa kadiri ya mang’amuzi ya maisha tunaona kuwa watu wale ambao wanaishi kwa mipango na nidhamu, wanafanikiwa sana katika shughuli za maendeleo yao binafasi, lakini wale ambao hawana mipango au nidhamu ya maisha huwa ni vigumu sana kwao kuweza kufikia malengo yale ambao wangetamani kuyafikia. Katika mwaka huu wa 2000 tunataraji wengi watafikia malengo yao kwa kutenda kulingana hasa na utaratibu waliojiwekea. Hivyo cho chote kile ambacho kitatendeka.

Haitakiwi kabisa kufanya shughuli za maendeleo kwa mtindo wa kubuni mambo bali inahitajika kuwa na hali kuona mbele na kupanga mambo sawa sawa. Daima yatupasa kufanya tathmini katika utendaji wetu wa shughuli zetu mbalimbali. Mtu asipofanya tathimini ya kazi na shughuli zake, ni pia vigumu kuweza kuona kama amekwenda vizuri au hapana. Yafaa kufanya tathmini ya utendaji wetu kila mwezi, kila wiki na hata kila siku ikiwezekana. Katika kutathmini shughuli zetu hapo tutaweza kuwa na uhakika wa ufanisi wa shughuli hizo tulizokusudia kuzifanya.

Wengi hufanya shughuli kwa hasara kwa sababu hawafanyi thathimini ya mara kwa mara ya shughuli zao.

Kwa hiyo basi tunapaswa kuwa na mipango, yaani tuelewe tunakusudia kufanya nini, na baada ya hapo tuweke nia thabiti katika utendaji wetu. Lazima tuone mbele tunakotaka kufika. Daima yatupasa kufanya tathmini ya kile tulichokitenda na hivyo kuona ni wapi tumekwenda vizuri na wapi tumekwama. Ikiwa kuna mahali tulipokwama, basi inatupasa tufanye jitihada ya kusahihisha ili tufikie lengo lile tulilokusudia.

Tunamalizia kwa kutoa mwito kwa wananchi wote kuwa mwaka huu wa 2000 uwe ni kweli mwaka wa juhudi na mafanikio hasa katika shughuli za maendeleo ya kweli katika taifa letu na katika familia.