NGUVU YA HOJA Fr. P. Haule...

Tutafanikiwa kwa matumaini na juhudi

VIONGOZI mbalimbali wa serikali na hata wa madhehebu ya kidini wamesema kuwa wanatakia raia na wananchi kwa ujumla mwaka huu uwe ni hasa mwaka wa matumaini.Wanasema kuwa wangependa kuweko na matumaini ya maendeleo katika mataifa. Wanapenda kuwe na matumaini ya amani kati ya mataifa na kati ya jumuiya na jumuiya. Pia wangependa kuona haki inadumishwa kati ya mataifa. Kwa kifupi ni kwamba viongozi hao wanapenda kuwasihi na kuwahimiza raia wote na hasa wale wenye mapenzi mema kuwa wanatakiwa wasikate tamaa licha ya magumu ambayo yamekuwa yakionekana katika siku za nyuma, au mwaka uliopita.

Sote tunakiri kwamba kumekuwa na matatizo mengi katika mwaka uliopita. Kulikuwa na matatizo ambayo yaliyokuwa nje ya uwezo wetu, na hivyo hatukuweza kuyashinda au kuyakwepa. Kulikuwa na matatizo ambayo yalikuwa ndani ya uwezo wetu, lakini kwa bahati mbaya kwa sababu ya kukosa ujasiri na juhudi tulishindwa kukabiliana nayo. Hivi mwaka huu tunaalikwa kukabiliana na matatizo mbalimbali ya maendeleo kwa juhudu pamoja na matumaini. Mtu mwenye matumaini hakati tamaa anapokabiliwa na upinzani uwao wote ule.

Tunapaswa kukumbuka kwamba hakuna shughuli yo yoyote ya maendeleo ambayo haina upinzani au hali ya kukatisha tamaa. Wataalam wa falsafa hutuambia kwamba kila jema hupatikana kwa juhudi kubwa kwa kuwa jema lo lote lile ni kitu bora na hivyo hakiwezi kupatikana kwa njia rahisi. Shughuli za maendeleo ni matokeo ya kazi ya jasho inayotokana na juhudi ya mtu binafsi au kikundi cha watu. Jema ambalo binadamu hulitafuta daima linapatikana kwa kufanya juhudi pamoja na matumaini.

Hivyo hao wenzetu tunaowaona wamesonga mbele katika shughuli za kimaendeleo na pia katika ustaarabu wa siku hizi ni kwamba wamekuwa na matumaini pamoja na juhudi katika kufanya kazi. Na tunaposhuhudia kazi mbalimbali kama majengo, mashine, mabarabara, mashamba makubwa na madogo, na mambo mengineyo tukumbuke kwamba hayo yametokana na mioyo ya watu iliyokuwa imejaa matumaini. Kwa sababu walikuwa na matumaini, basi waliongeza daima juhudi pale palipokuwa pakionekana kuwa na ugumu fulani. Hakuna kazi njema isiyo na vipingamizi kutoka ndani au kutoka nje. Kwa hiyo viongozi wetu wanapotutaka tuwe na matumaini, wanalotaka kwanza tuwe tayari kukiri kuwa kuna matatizo ambayo sharti tukabiliane nayo.

Maendeleo kwa kawaida hayafiki kwa njia rahisi, au wasemavyo wataalamu hayafiki kwa kuletewa kwenye sahani ya dhahabu, bali ni kwa kutenda kazi. Kwa hiyo licha ya kuwa na matumaini kuhusu maendeleo au cho chote kile tunachokihitaji katika maisha yetu inatupasa pia kuwa na bidii pamoja na ujasiri. Wengi wetu tunatamani kupata maendeleo au kupata kitu fulani kilicho chema. Lakini kumbe kwa bahati mbaya hatuna juhudi ya kutenda kazi na hivyo kukabiliana na shida mbalimbali. Wananchi wengi wanakosa kuwa na nyumba nzuri kwa sababu ya kukosa juhudi, ingawaje pengine wanatamani kuwa na nyumba. Wako wanaotamani kuwa na mali, lakini hawataki kufanya kazi kwa bidii na kwa juhudi. Tamaa yao ya kuwa na vitu kama hivyo hubakia tu katika mioyo na akili zao kwa sababu hawako tayari kukaliana na magumu, kama vile jua kali au baridi kali. Tamaa pekee yake bila juhudi haiwezi ikazaa lo lote lililo jema. Mtu anaweza akawa na tamaa au hamu ya kuwa na kitu, lakini asipokuwa na juhudi thabiti ya kukipata kitu hicho ni kazi bure kabisa.

Kila tunaposhuhudia kuna maendeleo fulani hapa na pale tukumbuke kwamba hao walioleta hayo maendeleo walikuwa kwanza na hiyo tamaa ya kujiendeleza. Baada ya kuwa na tamaa, lililofuata wakaweka juhudi katika jambo au kusudio hilo. Ikiwa walipambana na magumu, hawakukata tamaa, bali walitafuata suluhisho na wakaweza kufanikiwa. Ni jambo baya sana kwa mtu mwenye kutaka maendeleo kuwa na hali ya kukata tamaa au kutokuwa na ujasiri wa kukabiliana na vikwazo mbalimbali. Binadamu kwa vile ni kiumbe chenye kupenda kushirikiana na wengine, basi hapo anapokwama hujitahidi kuomba msaada kutoka kwa wale wanaomzunguka. Pengine huomba msaada wa kusaidiwa kimawazo, na pengine hata kimali.

Licha ya kutumia juhudi katika utendaji wetu, tunaambiwa kuwa inapasa pia kutumia maarifa katika utendaji wetu tukitaka kuendelea kweli kweli. Mara kwa mara tunaona kwamba kuna watu ambao wamekuwa na juhudi sana katika kutenda kazi za maendeleo, lakini wanashindwa kupata yale matunda yanayotamaniwa kwa sababu hakuna ule ufundi au maarifa yanayotakiwa. Kwa mfano kwa wakulima, wanaweza kulima maekari mengi sana, lakini kama hawatatumia maarifa ya kilimo kama vile kuweka mbolea, kupanda wakati wake, na kupalilia, hapo si rahisi kuvuna kile kinachotarajiwa. Tunahitji sana kuwa na matarajio au matumaini katika kazi yetu, na tunahitaji kuwa na juhudi katika utendaji wetu, lakini pia tunahitaji kutumia elimu na maarifa katika utendaji wetu.

Kwa hiyo tunaposema kuwa mwaka huu uwe ni mwaka wa matumaini na juhudi, ni kwamba kila mwananchi kwanza awe na malengo. Binadamu tu viumbe vyenye akili na utashi na hivyo tunapaswa kutumia akili zetu katika kufanya mipango ya mwaka. Haitoshi kutamani kitu, bali inatupasa kukiwekea mikakati ya kukipata kwa hali na mali. Kwa hiyo wiki hii ya kwanza ya mwaka ni kwa ajili ya kujiwekea mipango ya malengo yetu. Tunapaswa kuona waziwazi ni jambo gani tunalitaka kulifanikisha katika mwaka huu.Sisi binadamu tukiwa tofauti na wanyama tunajiwekea mipango ya kitu fulani na katika mwaka mzima tunaweka juhudi, matumaini pamoja na maarifa yetu ili kuweza kulifanikisha jambo hilo. Tunapaswa kuachana na ile tabia ya kusema mradi kumekucha.

Kila siku katika mwaka huu iwe ni kwa ajili ya kujiongezea tija, na hivyo kutuletea mafanikio ya namna falani. Mtu anayeridhika na hali aliyo nayo hawi tofauti na mnyama ambaye hata kama mwaka hata mwaka ananyeshewa mvua hafanyi jitihada ya kukabiliana na mvua kwa kujenga nyumba. Lakini tunatarajji kwamba binadamu kwa kuwa ana akili atafanya kila jitihada ya kukabiliana na mazingira magumu na hivyo kuwa na maisha bora zaidi. Jambo kubwa tunalodaiwa mwaka huu ni hasa katika kuboresha hali za maisha yetu, tukianzia hasa na maisha ya nyumbani. Tunapaswa kuwa na chakula cha kutosha, ili afya zetu ziweze kuwa bora. Pia itatupasa kuhakikisha kuwa tunakuwa na mahali pazuri pa kulala na vilele nguo bora za kujivika. Itatakiwa kila mwananchi atunze mazingira yanayomzunguka katika usafi unaotakiwa.

Na kwa upande wa elimu, kwa vile tumeambiwa kwamba huu ni mwaka wa sayansi na tekinolojia, tunatamani sana wananchi wawe na mwamko wa kujipatia elimu katika mambo mbalimbali. Ni jambo la kusikitisha sana kuona kwamba wananchi wengi wameridhika na hali duni waliyo nao hasa ile ya ukosefu wa elimu na maarifa. Tunapenda kuwaalika wote waone kwamba kwa kufikia mwaka huu wa 2000 wamebahatika sana na hivyo inawapasa kuwa na shukrani. Lakini shukrani kubwa itakuwa hasa ni ile ya utendaji katika matumaini, na pia ya kuwa na juhudi katika utendaji huo.