NGUVU YA HOJA Fr. P. Haule...

Mwaka 2000 uwe ni mwaka wa namna gani?

MAMBO mengi sana yamebashiriwa kwa mwaka huu tunaouanza hivi leo. Wako watu ambao wameubashiria kuwa utakuwa ni mwaka wa maafa mengi sana na hata ukawa ndio mwisho wa dunia.

Wako watu ambao wanakatishwa tamaa kabisa kwa mwaka huo kwa vile wanafikiri kuwa hautakuwa ni mwaka wa bahati njema kwao na hivyo husema kwamba ni wakati wa mwisho kabisa kwa uhai wao. Hata hivyo kuna wengine wenye kuuangalia mwaka huo kama ni mwaka wa bahati mbalimbali katika maisha yao.

Kwa hiyo kwa hao Watanzania wenye mtazamo huo wa matumaini na wenye faraja, mwaka huu utakuwa ni kweli wa maendeleo, ukitilia maanani kwamba tumetangaziwa kuwa tunaingizwa katika karne ya sayansi na tekinolojia. Jambo hilo ni lenye kutia moyo kwa wale wote wapenda maendeleo na wenye juhudi ya kujiendeleza. Hao ndugu wanamshukuru Mungu kwa kuwawezesha kuvuka kutoka karne ya 20 na kuingia katika karne hii mpya ya 21. Kwao siyo mwaka wa kuketi na kulalamika, bali ni mwaka wa kazi hasa kwa kutumia juhudi na maarifa.

Ni jambo la kusikitisha sana kwa Watanzania wengi kuwa wavivu na kukosa kabisa ari ya kufanya kazi za kujiendeleza na hivyo kuwa na maisha mazuri. Watanzania wengi wana ile sifa ya UVIVU na UZEMBE katika kazi na hivyo kuwa na maisha duni kabisa. Misahafu yote na walimu wote wa maendeleo ya binadamu huhimiza kuhusu utendaji wa kazi. Ni jambo la kusikitisha mno kuona Wananchi wengi hawana hamu ya maendeleo, bali wanapoteza nguvu zao na hata muda wao kwa kupiga domo na kulala usingizi.

Tunavyoelewa ni kwamba hata kama mtu unafunga kufuatana na dini yako inavyodai, lakini kamwe hakuna dini inayofundisha kwamba wakati wa mfungo ukae tu chini ya kivuli ukisubiri kufuturu na kupata futari. Mfungo wa kweli ni ule unaoendana na kufanya kazi kwa bidii.

Lakini kinyume chake ni jambo baya sana la kushinda bila kazi wakati wa mfungo.

Tokea tumepata UHURU tuliambiwa kuwa ilitupasa sisi tukimbie, wakati wenzetu wanatembea mwendo wa kawaida. Lakini kumbe sisi tunatembea, tena pole pole sana na wenzetu wanapozidi kukaza mwendo wa maendeleo. Watanzania walio wengi wameridhika mno na maisha duni, na hivyo hawataki kabisa kujiendeleza. Kwa hiyo tunatumaini kwamba mwaka huu wa 2000 utakuwa ni mwaka wa mwamko kwa Watanzania walio wengi.

Tunatumaini kwamba mwaka huu ustakuwa ni mwaka kwa ajili ya kujenga hamu na ari kubwa ya maendeleo yetu binafsi na ya jamii.

Hakuna kitu kibaya katika shughuli za maendeleo ziwazo zo zote zile kama mtu kuridhika na hali aliyo nayo. Kuna wananchi ambao wameridhika kabisa kuishi katika vibanda duni, na papo hapo wana nguvu, wana muda, lakini hawana ari. Wako pia wananchi ambao wameridhika kabisa kuvaa nguo duni, chafu, na hawataki kabisa kubadilika na kuwaiga wengine. Wako vile vile Watanzania ambao wanapenda kuwaelemea ndugu zao, hawataki kujitegemea na kufanya kazi, bali wanapiga uvivu na kuridhika na hali hiyo.

Licha ya kujinyima wao wenyewe maendeleo, wanawakwamisha pia hao ndugu wanaowaelemea. Tungependa tabia hiyo ikome kabisa katika mwaka huu wa 2000 na kuendelea. Hivyo pia tungependa kuona Watanzania wote wanajenga ule utamaduni wa kuona aibu ya kukaa bila kazi na bila kuzalisha cho chote kile pale tulipo.

Tungependa kuona Watanzania wote wanakuwa na wivu wa maendeleo badala ya kuwa na uvivu wa maendeleo.

Wanasiasa wetu tokea awali tunapata Uhuru walitufundisha kusema na kuishi kwa msemo, "UHURU NA KAZI". Lakini kumbe siku hizi wengi wanataka kuishi kwa uhuru BILA kazi.

Je, hali hiyo itatupeleka wapi sisi Watanzania? Inashangaza sana kushuhudia jinsi Watanzania tunavyojiaibisha kwa wageni wafikao na kutoka katika nchi yetu. Tunazungumza mno na kutenda kidogo mno na hata pengine, hakuna kinachofanyika na mtu anakaa tu wala hakuna anachokizalisha siku nzima, wiki nzima na hata mwezi mzima. Kidini jambo hilo ni dhambi, tena dhambi kubwa .

Binadamu tuliagizwa kufanya kazi ya kuutawala na kuuendeleza ulimwengu huu. Kuna wenzetu wengi ambao wameelewa maana ya kufanya kazi ya kuutiisha ulimwengu huu.

Wenye hekima hutuambia kwamba mtu anaweza akamlazimisha punda kwenda mtoni au kisimani, lakini kamwe hawezi kumlazimisha kunywa maji.

Hivyo nao viongozi wetu wamejitahidi kutuhimiza na hata kutulazimisha katika kufanya kazi za kimaendeleo, lakini Watanzania walio wengi hawataki kabisa kupokea mashauri hayo ya maendeleo.

Hivyo wengi wanaingia katika karne hii mpya na vibanda vinavyovuja, na nguo zenye viraka, wanaingia wakiwa hawana mahali pazuri pa kulala, wala chakula cha kutosha.

Wengi wanaingia karne ya 21 wakiwa na magonjwa yanayotokana na kutozingatia sheria na kanuni ya afya.

Watanzania wengi wanaingia katika karne mpya wakiwa wamezungukwa na ujinga mwingi sana kutokana na uvivu na uzembe wao wenyewe.

Ama kwa hakika ni jambo la fedheha mno kuona baada ya miaka 38 ya Uhuru, bado hali zetu ni duni mno.

Hatuna mtu wa kumlaumu bali tunapaswa kujilaumu sisi wenye kwa kutokuwa na hamu ya maendeleo na hivyo kupiga uvivu mchana kutwa, bila kufanya kazi ya kuzalisha cho chote kile. Hivyo tusipobadilika kimaendeleo, tunataka mwaka 2000 uwe ni mwaka wa namna gani?