Make your own free website on Tripod.com

NGUVU YA HOJA Fr. P. Haule

Madereva wawajibike zaidi

NAKUMBUKA sana mara moja mzee mmoja mmisionari alimwambia kijana dreva mpya kuwa kila anapoendesha gari akumbuke kuwa ni kama vile anatembea na simba ambaye wakati wo wote anaweza kumshambulia na kupoteza uhai wake mwenyewe au uhai wa watu wengine.

Hivyo ndivyo ingepasa kila dreva akumbuke kuwa gari analoliendesha ni kama vile simba mkali anayeua.

Lakini kwa bahati mbaya madreva wengi wanaona kuwa gari ni kitu cha kuchezea tu na hivyo wanaweza kukiendesha wanavyotaka kwa hasara yao wenyewe na ya wengine.

Pia mara moja niliingia katika gari moja na kuona mbele yangu pameandikwa maneno ya kiingereza ‘you ride on your own risk’ maana yake unapanda gari hili kwa kujihatarisha mwenyewe. Na ndivyo ilivyo katika magari mengi siku ya leo. Madreva wengi wanacheza na magari na kuhatarisha maisha ya watu kama vile mtu mjinga anavyocheza na simba. Itakuwa dreva na akili yake anaovateki mahali ambapo hana uhakika kabisa wa kupita salama akiwa amebeba watu wengi ndani ya basi. Inashangaza kuona ni kwa jinsi gani madreva wetu wanavyothamini spidi kubwa na hivyo kuonekana ni dreva wa maana kwa sababu ya kukimbiza gari na kusabisha ajali mbaya sana. Kusema kweli abiri wengi wanapanda magari kwa kujihatarisha wenyewe, lakini wafanyeje ikiwa hakuna namna nyingine ya usafiri.

Hivi karibuni nilisimuliwa na rafiki yangu ambaye alikuwa kule Israel kwa Hija. Alisema kuwa jambo la kushangaza ni kuona kule wenzetu hawana mtindo wa kuovateki magari na hivyo karibu hakuna ajali , hasa hizi zetu za kijinga na kiwendawazimu. Tunasema ni za kijinga kwa vile kama mtu angekuwa anatumia akili zingeweza kuepukika kabisa, lakini kwa vile madreva wetu wanatumia tu mabavu ya kutaka kujionyesha kama anaweza kukimbia sana na kumpita mwingine aliye mbele yake.

Huwa inanishangaza sana ninapoona gari lililo nyuma yangu likifanya jitihada ya kuovateki na kuwa tu mbele yangu na siyo zaidi. Madreva wengi wanaona ni fahali kubwa sana kuovateki na hivyo kusabisha ajali nyingi na mbaya.

Kama tulivyosema hapo awali kwamba dreva yampasa akumbuke daima kuwa anayo dhamana ya maisha ya watu na hivyo inampasa kabisa kuwa mwangalifu.

Hakuna sababu ya kufanya mashindano katika kukimbiza magari ambayo yana watu. Magari ya mashindano kwa kawaida hayana abiria, na hivyo madreva wanapoamua kukimbizana na huku wamebeba abiria hao ni wendawazimu na ni vichaa. Madreva hao tunasema kwanza hawana ubinadamu wala akili ya kiutu.

Tunapenda kuwaonya na wale abiria ambao wanawahimiza madreva kuongeza mwendo ili wakafike haraka. Nao tungeweza kusema ni kama wendawazimu kwani mara nyingi ajali zimetokea kutokana na hao abiria ambao wanataka magari yakimbie wakawahi shughuli zao.

Mapato yake ni kwamba, badala ya kuwai shughulini wanawahi kaburini.

Mara moja niliambiwa kuwa sisi Waafrika wengi tunakufa mapema kutokana hasa na uzembe pamoja na ujinga.

Ni kweli kuwa siku hizi tunasikia juu ya ajali mbalimbali huko na huko.

Lakini hizo tunasema ni ajali katika maana halisi, na siyo hasa kutokana na uzembe au ujinga wa kutojalia sheria.

Kwa kuwa dreva ndiye mwenye dhamana kwa abiria na pia kwa gari lake, itakuwaje aondoke na kuanza safari bila kujua kama gari lake liko katika hali gani.

Kuna vitu ambavyo dreva anapaswa kuviangalia kwa makini kabla ya safari yake kuanza, na hivyo pia anapokuwa ametembea mwendo wa kutosha.

Ni lazima kabisa matairi yachekiwe mara kwa mara hasa kama ni safari ndefu. Tunaposikia kuwa gari limeanguka kutoka na kupasuka tairi, ni lazima tumwulize dreva kama upepo katika tairi ulikuwa sawa sawa ama sivyo? Wako wale madreva bora ambao huwa wanacheki mara kwa mara kama matairi yako sawa sawa kwa kuwa wanajua kuwa wana dhamana kubwa sana mbele ya abiria.

Watanzia tutapunguza vifo vya ajali ya magari ikiwa madreva wetu watapunguza spidi na kuwa waangalifu zaidi.

Ajali za magari zitapungua ikiwa madreva wetu watakuwa waangalifu sana katika vitendo vya kuovateki na pia kucheki magari yao mara kwa mara. Madreva wengi hasa wa Daladala huthamini zaidi ukusanyaji wa pesa kuliko usalamu wa abiria na hivyo huendesha bila nidhamu.

Mara nyingi tunashuhudia magari hayo yakiwa yamepata ajali na hivyo wao wenyewe hukosa kazi, na wanaingiza hasara kubwa sana kwa matajiri pamoja na kuhatarisha maisha ya abiria.

Tunapenda kumalizia makala yetu hii kwa kurudia hayo tuliyoyasema kuhusu spindi na kuvateki kwa madreva wetu.

Wakienda kwa mwendo mzuri maisha ya abiria yatasalimika.

Mtu anaposafiri anapaswa kuwa katika utulivu wa moyo, lakini akisafiri na roho mkononi, hapo safari siyo nzuri.

Mapka sasa tunapenda kuyapongeza mashirika mawili ya magari yaendayao huko mikoani, nayo ni "Scandinavia na lile la Fresh ya Shamba". Wasafiri wale wanathamini maisha yao huyatumia mabasi hayo, licha ya kuchelewa kidogo kufika kule waendako. Hilo siyo kitu kwani kuna usalama.