Make your own free website on Tripod.com

NGUVU YA HOJAFr. P. Haule...

Tudumishe Amani

Wataalamu hutuambia kuwa zawadi ni kitu ambacho mtu hupewa bila mastahili yake mwenyewe bali ni kutokana na wema au huruma ya yule mwenye kutoa.

Mtu ye yote mstaarabu akishapewa zawadi kwa kawaidi huwa anashukuru kwa kusema asante. Lakini pia kuna wakati ambao hupasika kutoa ahadi ya kuitumia na kuitunza zawadi hiyo ikitengemea sana thamani ya hiyo zawadi.

Sisi Watanzania tunaambiwa kwamba licha ya kupewa nchi hii nzuri na ya kupendeza, Mwenyezi Mungu katujalia bahati nyingine kama zawadi nayo ni bahati au zawadi ya kuwa na ‘AMANI’.Tunasema kuwa tumepewa bahati na zawadi ya kuwa na amani katika nchi yetu na hivyo jambo la kwanza hatuna budi ya kushukuru bahati na zawadi hii. Jambo la pili tunalodaiwa ni la kuitunza hiyo amani. Siku kwa siku viongozi wetu na wale wote wenye kututakia mema sisi Watanzania, hawakosi kutukumbusha juu ya zawadi hiyo na pia kutuhimiza kuhusu utunzaji wa hiyo zawadi. Wengi wanatuambia kwamba tusichezee zawadi hii ya amani kwani hasara yake kama itapotea ni kubwa mno.

Daima hao viongozi wanatuambia bayana kuhusu zawadi yetu hiyo na hasara inayoweza kutokea wakituletea mifano ya nchi jirani ambazo hazina amani, na badala yake ni mapigano tu.

Je, ni nani kati yetu ambaye angependa atengane na wazazi wake, atengane na mke wake, atengane na watoto wake, au atengane na marafiki zake? Ni kwa masikitiko gani tunaona wale wenzetu ambao hulazimika kutengana na ndugu zao na hivyo kuwa wakimbizi kwenye nchi jirani wakiwa wameacha karibu kila kitu nyuma yao.

Ni dhahiri kuwa hao wamepoteza ile zawadi kubwa na bora sana ya amani.

Na kwa nini mtu mzima mwenye akili aweze kutamka kuhusu umwagaji damu, au kwa maneno mengine kuhusu kudharau hiyo zawadi tuliyopewa. Papo hapo tunatambua kweli kuwa madhara yake ni mabaya.

Tunawapongeza na kuwasifu viongozi wetu wenye uchungu na nchi hii kwa kuwa tayari kuwakemea wale wote wanaotaka kuichezea zawadi yetu hii kubwa na ya thamani. Tunapenda kuona kama ilivyokuwa kawaida yetu kwamba tunazimaliza tofauti zetu ziwe za kiuchumi, za kisiasa na za kijamii kwa njia ya mazungumzo na wale siyo kwa njia ya umwagaji damu. Tunazidi kuomba kwamba mshikamano tulio nao katika Taifa letu udumu.

Pale penye tofauti tuwe tayari kuleta uelewano na hivyo tudumishe umoja, upendo na amani. Tunambiwa tupingane bila kupigana, tuzungumze bila kugombana, tujadiliane na kufikia mwafaka ambao utatudumishia amani.

Wataalamu wa Kirumi na Kiyunani walisema kuwa pale penye vita na machafuko, hapo miungu ya maendeleo haifanyi kazi. Kwa maneno mengine ni kwamba hakuna maendeleo ya kweli ikiwa watu wanapigana na kukimbia kimbia huko na huko ovyo ovyo.

Ebu, angalia kule Angola, kule Congo, Burundi na Rwanda, ni kweli kwa muda huo wa vita watu wamefanya kazi za maendeleo ya nchi zao? Jibu ni kwamba kumekuwa na hali ya kurudi nyuma kabisa.

Kama kusingekuwa na vita, tunaamini kwamba hao ndugu zetu wangekuwa katika hali bora sana, lakini kutokana na ubinafsi wa hasa viongozi hali ya nchi hizo ni mbaya sana.

Tunapenda kusema kuwa tofauti zetu za kisiasa zisitufanye tupoteze zawadi yetu hii.

Daima sisi Watanzani tumehimizwa kuhusu vikao mbalimbali. Kwa njia ya vikao tumeweza kumaliza matatizo na tofauti zetu nyingi sana.

Kwa njia ya vikao ni kweli kuwa sisi Watanzania tutaweza kuitunza zawadi yetu hii kubwa na ya thamani. Tukumbuke kuwa kuna watu wengi na nchi nyingi sana ambazo zinatuonea wivu kwa zawadi hii kubwa tuliyojaliwa na Mwenyezi Mungu.

Kwa bahati mbaya wapo baadhi ya wananchi ambao bado hawatambui kabisa zawadi hii tuliyojaliwa.

Tunatumaini kwamba kama wangetambua, basi wasingekuwa wanaroporopa maneno ya kuidharau zawadi hiyo ya amani.

Tunaambiwa kuwa amani ni zawadi na kwa hiyo tunapaswa kuitunza kwa hali na mali. Tunaweza kusema kuwa ingawaje nchi yetu kiuchumi ni maskini, lakini kwa sababu ya amani tuko ‘matajiri’. Katika maana hii ni kwamba tukiwa na amani tunaweza kufanya mambo mengi sana ya uzalishaji wa mali, lakini kama kuna choko choko za hapa na pale siyo rahisi kuzalisha mali.

Hapo tunawaomba viongozi wetu wasikose kuwakemea wale wote wanataka umaarufu kwa njia ya kuturugia zawadi yetu ya amani. Tunapenda wale wenye kutaka umaarufu katika taifa letu, wautafute kwa njia zinazojenga amani, na siyo zile zenye kuleta vurugu na kuharibu amani yetu.

Pia kwa kuwa amani kama tulivyosema ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi, basi hatuna budi kukumbushana kuhusu kumshukuru huyo Mwenyezi kwa zawadi hiyo, lakini hasa kuzidi kumwomba azidi kutudumishia hiyo amani. Tunamwomba Mwenyezi adumishe amani katika taifa letu hasa nyakati hizi ambapo kuna hewa isiyo nzuri katika taifa letu.

Ni Mungu mweza yote ndiye mwenye kuzidi kutudumisha katika amani na umoja.

Tunachoomba ni amani idumu katika wanasiasa wetu ili wazidi kutuunganisha licha ya kuwa na vyama vingi. Wingi wa vyama utuletee uelewano zaidi kwa njia ya utajiri wa mawazo.

Lakini hasa tunapenda kuwa na uelewano tukiachilia mbali kabisa tofauti zetu za kidini na kikabila.

Wananchi wamwabudu Mungu katika amani na isitokee kwamba kuna kudharauliwa au kubaguana kidini. Huo umekuwa ni msimamo wa nchi yetu tokea tumejipatia uhuru. Tumeishi kwa kushirikiana bila kubaguana wala kunung’unikiana. Pale palipotokea kutoelewana, tumekuwa tukizungumza na kumaliza tofauti zetu. Siyo kawaida ya nchi yetu kikundi fulani kuishi kwa manung’uniko yawayo yote yale, bali tunataka kila mmoja aishi katika haki na usawa.

Kwa kumalizia tunapenda kuwakumbusha yale maneno ya yule Mtaalamu, kwa kumwomba Mwenyezi atufanye sote tuwe vyombo vya amani ili tuweze kuleta upendo pale penye chuki, kupatanisha pale ambapo watu wanagombana, kuleta uelewano na kupatana pale ambao watu wanafarakana, kujenga uvumilivu na moyo wa kusameheana pale ambapo binadamu wanakoseana.