NGUVU YA HOJAFr. P. Haule...

Misaada haikutumika ipasavyo

HIVI karibuni kuna mtaalamu mmoja wa kutoka nje ya nchi yetu amesema kwamba inasikitisha sana kuona Tanzania imepewa misaada mingi sana hasa ile ya maendeleo, lakini kazi iliyofanyika ni kidogo sana. Huo ni ukweli ambao hatuwezi tukaukana, kwani mambo ndivyo yalivyo hapa nchini petu.

Kama kuna nchi katika bara hili la Afrika ambayo imefanikiwa kupata marafiki na wahisani, Tanzania ni kati ya nchi za kwanza. Mwenyezi Mungu tokea tumepata Uhuru alitujalia wafadhili na wahisani wengi sana. Tumepata misaada ya hali na mali kutoka huko ng’ambo, Ulaya, Marekani, Uchina, Ujapan na kwingineko. Kumekuwa na wafadhili ambao wamegharamia miradi mbalimbali; kuna wale ambao wamegharamia miradi ya elimu, wengine miradi ya afya, wengine miradi ya maji, wengine miradi ya usafiri kama vile mabarabara. Kuna wafadhili wengine ambao wametusaidia katika mambo ya kilimo, uvuvi na hata mambo ya viwanda. Kwa kifupi tumesaidiwa sana.

Swali la kujiuliza ni je, misaada hiyo imetumika kama ilivyokusudiwa ama sivyo? Jibu la swali hilo ni kuangalia hali halisi ilivyo katika sehemu mbalimbali za nchi yetu. Mtu akipita hasa kule vijijini atashangaa sana kuona jinsi wananchi wanavyoishi bado katika hali ya umaskini. Ingawaje kulikuwa na misaada iliyotolewa kwa ajili ya huduma ya maji, lakini akina mama wanahangaika kila siku katika kutafuta maji. Ingawaje kumekuwa na wafadhili ambao walitoa misaada kwa ajili elimu, lakini inasikitisha sana kuona jinsi majengo ya shule, hasa madarasa yalivyo katika hali duni sana. Kulikuwa na wafadhili ambao wametoa misaada kwa ajili ya huduma za afya, lakini majengo yake ni mabovu, na ndani ya zahanati au hospitali hizo hamna dawa kabisa. Kumekuwa na wafadhili ambao wamekuwa wakitoa misaada kwa ajili ya barabara zetu, lakini hizo barabarani au haziishi, au hutengenezwa kwa kulipualipua na hivyo hali huzidi kuwa mbaya sana.

Tatizo kubwa lililoko kwa Watanzania wengi, na hasa wale ambao wana madaraka katika Serikali na katika Mashirika ni ile tabia ya ubinafsi.

Kutokana na hali hiyo ya ubinafsi , viongozi wengi wamekuwa wevi wa mali ya umma. Misaada mingi sana imeingia katika mifuko ya viongozi bila kufanya maendeleo yaliyokusudiwa. Inatosha mtu utembelee sehemu za Mbezi Beach na ukayaone yale mahekalu yaliyojengwa kule. Jaribu kuuliza ni nani anaweza kujenga majengo kama hayo kwa mshahara wake au kwa shughuli azifanyazo. Hatuna mashaka kwamba ni misaada ya wahisani wetu ambayo imetumika kujenga majengo hayo makubwa ambayo mengine hayamaliziki kwa sababu vyanzo vya pesa vimefungwa.

Serikali ya awamu ya tatu imetangaza kupiga vita rushwa, kwa hakika kabisa tunaipongeza. Lakini inaonekana kuwa ni kazi ngumu kutosha. Sisi tunasema hatua zinazochukuliwa sasa za kuzuia rushwa ingetakiwa kwanza kabisa kuanza na wale ambao wameshakula rushwa na mapato yake yanaonekana waziwazi. Hao wahusika waende kwanza kule Mbezi Beach na mahali pengine wakawaulize hao wenye majumba makubwa walipata hela wapi na hasa kama walikuwa ni watumishi wa Serikali. Vitendo vya kuwashika madaktari wetu na kuwaambia wamekula rushwa ya shilingi 30,000/= ni vya upuuzi kabisa. Kwanza tukawasake wale waliokula hela nyingi sana za wafadhili wetu, nasi tunabakia maskini na wachache wanaishi maisha ya anasa. Hao wanaofungua mashule ya kimataifa (international schools) watueleze pia hela hizo wamepata wapi na hivyo kuanza miradi mikubwa kama hiyo. Ni kweli kuwa kuna wale ambao wamefanya jitihada ya kujipatia hiyo mali, lakini tunasema hao ni wachache sana. Wengi wametumia nyadhifa walizokuwa nazo katika kujitajirisha binafsi kuliko kuwasaidia wananchi na taifa kwa ujumla.

Ni jambo la aibu sana mtu akiona jinsi viwanda vyetu mbalimbali vilivyo sasa hivi. Tunasema ni jambo la aibu kwani tumekuwa na Idara mbalimbali pamoja na Mawaziri na watendaji mbalimbali. Inashangaza kuona Waziri mzima, mwenye dhamana katika taifa hili, wizara yake inaporoka na yeye wala hashituki. Kwa wale waliokiona kile kiwanda cha Sungura Textile, Jijini Dar Es Salaam natumaini watakubaliana nasi kuwa kuna uzembe na kutokuwajibika kabisa kwa Mawaziri.

Ilikuwaje, kiwanda kifilisiwe wakati kuna Waziri wake wa Viwanda, pamoja na wasaidizi wake, wote wakilipwa mishahara mikubwa sana. Kiwanda kimeibiwa paa pamoja na mashine, lakini wahusika wanaendelea tu kula mali ya umma. Linaloshangaza ni kuona wadogo wakikosa tu jambo dogo hufukuzwa kazi, lakini hao wakubwa waliosababisha kiwanda kiibiwe wanaendelea kupanua na kutanua huko na huko.

Wafadhili wengi wamekuwa wakitoa misaada yao hasa kwa mashirika ya kidini kwani wanaamini kuwa itatumika ipasavyo. Na ndivyo ilivyo hadi sasa. Kutokana na ile dhamiri sana ya kutenda kwa haki bila kudanganya, mashirika mengi ya kidini hupata misaada ambayo hutumika vizuri. Hapo tunaweza kusema kuwa kama Serikali ingekuwa imeyashirikisha mashirka ya kidini katika huduma mbalimbali ambazo wahisani walikuwa wameng’aramia, tunadhani kuwa mambo yangekuwa katika hali tofauti.

Hatusemi hivyo kwa vile sisi wenyewe tunahusika na mashirika hayo ya kidini, bali ni kutokana na hali halisi ilivyo. Kuna watendaji wengi ambao dhamiri zao ni kama vile zimekufa au zimesinzia na hivyo hawaoni vibaya kutumia vibaya misaada inayotoka kwa wafadhili.

Huo ni ukosefu wa maadili na uadilifu. Tunataraji kwamba wale ambao wanapokea misaada kutoka kwa wafadhili na wahisani wetu wataitumia vizuri na hivyo kuweza kutoa hesabu yake sawa sawa. Lakini mambo yalivyo sasa hivi yamejaa udanganyifu na ubinafsi mno.

Kutokuwa mwaminifu pamoja na kuwa na ubinafsi, hiyo ni hali ya kutokustaarabika.Mtu asiye mstaarabu hana uaminifu wala uadilifu, licha ya kutokuwa mcha-Mungu.Yule aliye mwaminifu, huogopa kuchukua mali ya umma na kutumia kama ya kwake.

Kwa bahati njema bado kuna wafadhili ambao wako tayari kutusaidia, lakini wanazidi kukatishwa tamaa kwa jinsi tunavyoitumia misaada hiyo.

Hapo imetupasa tubadilike ikiwa tunataka hao wafadhili waendelee kutusaidia. Ni jambo la fedheha kuona mfadhili anafuatilia mwenyewe jinsi msaada wake ulivyotumika. Kwa upande fulani ni vema wakafanya hivyo kwani sisi Watanzania tumezidi mno kudanganya na hata kuiba haki za watu wengine.

Nakumbuka mara moja jinsi wahisani walivyomfurahia Padri mmoja katika Jimbo moja hapa kwetu. Huyo Padri alipewa hela na hao wahisani kwa ajili ya mradi wa maji.

Kwa mipango aliyokuwa nayo yule Padri aliweza kufanikisha mradi huo kwa muda mfupi, tena vizuri sana. Basi wahisani walipofika na kuangalia jinsi mradi huo ulivyofanikiwa, walifurahi na hivyo wakatoa hela nyingine kwa ajili ya mradi mwingine na pia wakampa zawadi ya kwenda kupumzika kule Ulaya. Je, ni wangapi wanafanya hivyo hasa kwa upande wa mashirika ya umma?