Make your own free website on Tripod.com

NGUVU YA HOJA Fr. P. Haule...

Wabunge fanyeni tathmini

MPAKA sasa imebakia miezi michache sana na tutakuwa na uchaguzi wa Rais na Wabunge wetu. Kwa muda wa takriban mika mitano ndugu zetu Wabunge wamekuwa wakuhudhuria vikao vyao vingi kule Makao Makuu ya Serikali, Dodoma.

Wabunge wetu walijadiliana mambo mengi sana kwa faida ya taifa zima na hasa Majimbo yao ya uchaguzi. Tumekuwa na wabunge wasemaji na watoaji hoja nzuri sana na pia tumekuwa na wabunge ambao ni wa kimya kule bungeni, lakini watendaji na wahamasishaji katika Majimbo yao uchaguzi.

Tungeweza kusema kuwa huu ni wakati wa kufanya tathmini ya dhati kwa Wabunge wetu. Je, ni kweli kuwa hao Waheshimiwa kwanza kabisa wamekuwa ni wawakilishi wa wananchi ama sivyo? Kitu ambacho mwananchi anataka kutoka kwa Mbunge wake ni kutetewa na kuelekezwa katika shughuli za maendeleo.

Hivyo Waheshimiwa Wabunge wetu wanapaswa kujibu maswali mengi sana kwa Wananchi ambao waliwapa kura zao licha ya ile "kula". Je, Mheshimiwa Mbunge umetembelea vijiji vyako vyote katika Jimbo lako la uchaguzi na umeshiriki katika shughuli za maendeleo huko vijijini? Je, Mheshimiwa Mbunge umeshirikiana namna gani na serikali ya Wilaya pamoja na ile ya Mkoa katika kutatua matatizo ya wananchi wa Wilaya yako ya uchaguzi kama vile matatizo ya ujenzi wa shule, ujenzi wa zahanati, uondoaji wa tatizo la maji, uhimizaji wa elimu nk.? Je, Mheshimiwa Mbunge umekuwa ukiishi zaidi kwenye Jimbo lako la uchaguzi ama katika Jiji zuri la Dar Es Salaam? Je, Mheshimiwa Mbunge umekamilisha miradi mingapi katika Jimbo lako la uchaguzi?

Kwa makusudi kabisa Serikali yetu imejitahidi kuwapatia Waheshimiwa Wabunge wetu magari ya uhakika kusudi hasa waweze kufika huko vijijini bila wasiwasi. Gari la Mheshimiwa Mbunge lina dhamana kubwa sana kwa wananchi, na hivyo tunaweza kusema kuwa kwa namna fulani ni chombo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. Inatakiwa kila mwananchi alifahamu gari la Mheshimiwa Mbunge wake kwa vile linapita huko vijiji likuwa katika shughuli za kuhudumia maendeleo ya wananchi.

Na hata kama Mheshimiwa Mbunge kalikomboa kabisa gari hilo, hubakia ni kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. Hicho ni kitendea kazi cha Mbunge kwa Jimbo lake la uchaguzi na wananchi wa sehemu hiyo.

Kwa hiyo tunapenda kuungana na yule ndugu ambaye aliomba wakati wa kufanya kampeni za uchaguzi, Waheshimiwa Wabunge waende na ripoti ya utendaji huko kwenye kuomba kura.

Kwanza waeleze ni mambo gani waliyofanikiwa kuyafanya katika kipindi kilichopita na kisha ndipo watoe hizo ahadi nyingine. Watu wanapenda kufahamu kwanza ni kitu gani kimefanyika, na kisha nini mtu ananuia kufanya hapo baadaye.

Miaka mitano ni mingi kutosha kwa kuweza kufanya jambo la maendeleo kwa yule mwenye nia ya kufanya hivyo.

Kuna Waheshimiwa Wabunge ambao kusema kweli wamefanya mambo mazuri sana majimboni mwao.

Tungeweza kusema hao ni wachache sana kwani utashangaa kuona katika sehemu mbalimbali kuna shule ambazo hazijamalizika, kuna zahanati ambazo ziko katika hali mbaya sana. Bado watoto wetu wanasoma katika mazingira mabovu na Wabunge wenye kuhimiza maendeleo wako.

Hali za majimbo hudhihirisha utendaji wa Wabunge wetu kwa namna moja au nyingine. Ikiwa Jimbo fulani la uchaguzi limechangamka kimaendeleo, hapo tunaweza kutambua ule ushirikiano ulioko baina ya Mheshimiwa Mbunge pamoja na viongozi wenzake.

Lakini tunapoona wananchi wanaishi katika mazingira duni, nyumba mbovu, wavivu katika shughuli za maendeleo, hapo tujue kuwa Mheshimiwa Mbunge hakutimiza wajibu wake ipasavyo.

Tunao Wabunge ambao ni kweli wako pamoja na watu katika shughuli za maendeleo.

Hao ni wabunifu katika kuendeleza sehemu zao. Kama kuna tatizo hufuatilia kwa makini kabisa ili kuweza kupata suluhisho.

Tunawataka zaidi Wabunge walio watendaji kuliko wale wasemaji na wenye kupiga blablaa tu. Pia maswali ambayo wanauliza Waheshimiwa Wabunge wetu yale ni hasa yale ambayo yanawakera wananchi, na siyo yale ya kutaka kufahamu tu.

Tunataka waulize maswali ambayo yanalenga majimbo yao ya uchaguzi, na baadaye kufuatilia utekelezaji wake. Tulishaambiwa kwamba kwetu sisi Watanzania, maneno yawe mafupi sana, lakini utendaji uwe mkubwa zaidi.

Tunamalizia Nguvu Yetu hii ya Hoja kwa kuwatakia Waheshimiwa wetu Wabunge kujadiliana mambo yale ya maendeleo ya Majimbo yao na siyo vinginevyo kwani wananchi hawakuwatuma wajadili kila kitu ambacho hakiwasaidii kamwe katika maisha na maendeleo yao. Ni jambo la kukumbuka kuwa Ubunge siyo utemi, bali ni kama kuajiriwa na wananchi wa Jimbo la uchaguzi na hivyo wananchi wanawapatia kura na ni haki yao kupata huduma inayostahili kutoka kwa hao Wabunge waliowachagua.