NGUVU YA HOJA Fr. P. Haule...

Tuwe na tahadhari katika maisha

BINADAMU ni kiumbe ambacho kina akili na utashi, yaani chenye kutumia akili katika utendaji wake wa kila siku. Kuwa vikubwa sana binadamu hataweza kamwe kujitetea daima na kusema kitu fulani kimetokea kwa bahati mbaya.

Ni kweli kuwa kuna bahati mbaya za hapa na pale. Hata hivyo wataalam bado watasema kama mtu akitumia akili yake na hivyo kufikiri kabla ya kutenda hawezi kamwe kuingia katika matatizo yaliyo mengi.

Tunaelekezwa kuwa katika maisha tunapaswa kuwa na tahadhari yaani ile hali ya kujiweka katika usalama daima. Ingawaje binadamu hukabiliwa na maadui wengi katika maisha yake, lakini kuna uadui fulani ambao angeweza kabisa kuushinda kama angekuwa na tahadhari. Kwa madereva wenye kuendesha magari, inapasa kuwa na tahadhari katika uendeshaji wao. Wanaambiwa kuwa kwa tahadhari inawapasa kwenda kwa mwendo ambao kukitokea kitu cho chote ghafla waweze kujisalimisha. Lakini kuna madreva ambao wanaendesha magari bila kujali kama katika mwendo huo kikitokea kitu ghafla wataweza kutawala gari ama sivyo.

Hivyo pia mtu anapoamuwa kujenga nyumba, ni sharti achukue tahadhari kwa kuona kuwa mazingira yanayoizunguka nyumba hiyo ni mazuri ama sivyo. Kwa nini mtu anaamua na kuwa mkaidi na hivyo kujenga nyumba yake kule bondeni. Na mvua zikija na hivyo kumletea madhara, atamnung’unikia nani kama siyo ujinga wake mwenyewe wa kutokuwa na tahadhari?

Tunafundishwa na kukumbushwa daima kwamba inatupasa tuzilinde afya zetu.Kwa maneno mengine tunaambiwa kwamba tunapaswa kuchukua tahadhari katika kuzitunza afya zetu. Mtu ambaye anaijali afya yake atahakikisha kuwa analala mahali pazuri, anakula chakula kizuri, anavuta hewa nzuri, anakunywa maji safi na salama na pia anakimbilia tiba daima anapoona kuwa afya yake iko katika mashaka. Lakini tunashuhudia jinsi watu wengine wanavyoishiri bila tahadhari ya afya zao. Mapato yake ni kupoteza maisha yao.

Binadamu ni kiumbe chenye kutafuta elimu kama tahadhari ya maisha yake ya hapo baadaye. Ili aweze kuwa maisha mazuri ya ushirikiano na walimwengu wengine, huchukua tahadhari ya kuwapeleka watoto wake shuleni ili waweze kuishi maisha mazuri hapo baadaye. Kwa hiyo mzazi ambaye hamsomeshi mtoto wake, tungeweza kusema hana tahadhari kwa ajili ya mtoto wake huyo. Licha ya kumpeleka shule huyo mtoto wake, anapaswa pia kuanza kumlea huyo mtoto pale nyumbani kama tahadhari kwa maisha ya watoto wake. Kwa tahadhari mzazi au mlezi atafanya kila linalowezekana kwa ajili ya kuhakikisha usalama na ustawi wa mtoto wake.

Katika maisha yetu tunapaswa kuwa na tahadhari nyingi sana. Kuna wengi wanafungua akaunti zao benki ili kujiwekea akiba kama tahadhari kwa maisha yao ya hapo baadaye. Kwa hiyo binadamu hujitofautisha na viumbe wengine hasa kwa kujiwekea akiba katika mambo mbalimbali kwa ajili ya wakati ujao. Ingawaje hatuwezi kujua tutaishi miaka mingapi zaidi, lakini ni sharti kuwa na tahadhari ya kila namna . Kutokuwa na tahadhari yo yote katika maisha yetu ni umaskini mbaya sana, kwani Mungu ametuumba akitupatia akili ili tuweze kuangalia mbele yetu kwa kila tendo tunalolitenda. Yeye hataki kabisa tuwe tunajitetea kwa kusema ni bahati mbaya kila wakati.

Ni kweli kuwa katika maisha yetu huwa tunapambana na vitendo ambavyo tunaviita bahati mbaya. Lakini hata hivyo kutakuwa na mmoja ambaye hakufanya tadhari. Kwa mfano kupata ajali ya kugongwa na gari kuumia. Hapo lazima tutambue kuwa kuna mtu au dereva ambaye hakufanya tahadhari katika uendeshaji wake na kusababisha hiyo ajali. Yawezekana kuwa hapakuwa na tahadhari ya kucheki gari lake kama lina breki sawasawa ama sivyo. Inawezekana hakuwa na tahadhari katika uendeshaji wake, kwa kutoshika sheria za barabarani. Kwa hiyo kwa vikubwa sana tunaona kwamba ajali nyingi hutokana na kutokuwa na tahadhari. Ni vigmu sana kusema kuwa ajali kama ajali hutokea tu, bali tunasema hasa ni ukosefu wa tahadhari.

Tungependa sana kusema hasa kuhusu tadhari ya kujiepusha na ajali mbalimbali za barabarani. Ajali nyingi hutokea kwa sababu ya kukosa tahadhari kutoka kwa watumiaji mbalimbali wa barabara.Ni jambo la kusikitisha sana kuona jinsi watumiaji wa barabara hapa Jijini wanavyohatarisha maisha yao bila kuchukua tahadhari yo yote kwa mfano wale ndugu wanaoendesha baskeli kati ya magari, au wale wanaovuka barabara bila kuchukua tahadhari yo yote ile. Lakini kama kila mmoja wetu angechukua daima hatua ya tahadhari kabla ya kuanza kutumia barabara, natumaini mambo yasingekuwa mabaya kiasi tulichofikia hivi sana.

Kuna baadhi ya madereva ambao hujiona kuwa wasipoovateki gari lililo mbele yao, basi hawajui kuendesha gari, kumbe sivyo. Hawachukua tahadhari katika kuovateki na hivyo kusababisha ajali ambayo huleta hasara siyo kwa magari yao tu, na pia kwa magari mengine yanayotumia barabarahiyo.

Hivyo pia kuhusu afya zetu ambazo huzidi kuwa mbaya siku hata siku. Tunaelezwa kila siku kwamba inatupasa tujikinge na magonjwa mabaya kama vile kipindupindu kwa kuishi katika mazingira safi na salama. Lakini wengi wetu hawako tayari kupokea tahadhari kutoka kwa wataalamu mbalimbali. Hakuna kitu kibaya katika maisha kama kwa mtu kupuuzia tahadhari anazozipokea kutoka kwa majirani. Na hivyo kwa mfano ugonjwa wa kipindupindu na hata ule wa ukimwi huzidi kumaliza watu wengi kwa sababu watu wengi hawako tayari kupokea tahadhari hizo. Tumekuwa nyuma katika maendeleo kutokana na kupuuzia tahadhari mbalimbali kutoka kwa viongozi wetu.

Wale Warumi, wataalamu wa hapo kale walikuwa na msema wa kilatine usemao: "Quid, quid agis, prudenter agas, et respice finem", maana yake ni kwamba cho chote ukifanyacho kifanye kwa busara, na kisha angalia mapato yake. Kwa hiyo binadamu mwenye kuumbwa na sura na mfano wa Mungu, mwenye akili timamu hana budi kuwa na tahadhari katika maisha yake ili kuepukana na balaa mbalimbali. Hakuna sababu ya kufanya mambo kwa kubahatisha, bali lazima kutumia akili timamu. Wengi wamepoteza bahati na maisha kwa sababu ya kutokuwa na tahadhari. Tuwe na tahadhari katika maisha yetu ya kila siku.