HEADLINES

Walokole wawazingua Wakatoliki

Wamisionari wataka amani Congo

 

Walokole wawazingua Wakatoliki

lPadri aamua kufanya utafiti wa kina

Nairobi Kenya

PADRI mmoja wa Kanisa Katoliki Kenya, Padri Patrick Wachegge amesema kwamba amedhamiria kufanya utafiti wa kina juu ya watu wengi kuondoka katika madhehebu yao ya asili na kuingia katika madhehebu mapya, hasa kutoka kanisa katoliki.

Padri huyo wa kanisa la Holy Family (familia Takatifu) nairobi ambalo ni Kanisa kuu (Kathedrali) na mwalimu wa mafunzo ya dini Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya amesema kwamba suala hilo ni nyeti na kanisa halitakiwi kuendelea kulidharau.

Katika mahojiano yake na AllAfrican News Agency, AANA, Padri Wachegge amesema kwamba utafiti wake utazamia katika nadharia mbili nazo kuhusu imani na wokovu na utabibu wa kiimani.

Amesema masuala hayo mawili ndiyo yamekuwa yakielezwa na kila mtu ambaye amechomoka katika dini yake ya awali na kufuata dhehebu jingine jipya.

Alipoulizwa kufafanua zaidi yeye anafikira nini kuhusiana na suala hilo la watu kuondoka katika makanisa yao ya asili, Padri Wachegge amesema kwamba ni uhai mkubwa katika ibada zao.

Amesema mengi ya makanisa ya zamani ibada zao hazina uhai wa kumfanya mtu ajisikie na hivyo kutafuta dhehebu jingine ambalo linaweza kuweka uhai wa kutosha.

Amesema makanisa mengi makuu ya asili hayana uhai wa kutosha. Amesema utafiti atakaofanya utasaidia sana kujua tatizo halisi, kiini chake na pasi shaka kujaribu kutoa baadhi ya majibu kwa ajili ya kanisa.

Amesema kwamba suala kubwa ni kujaribu kutoa nafuu kwa waumini wa kanisa ambao wanaweza kuwa wanahangaika bila yasababu. Wakati Padri huyo wa Kikatoliki anatafuta majibu kwa ajili ya kanisa lake Katoliki Kanisa la Kiinjili lenyewe limesema kwamba ni kawaida watu kutafuta eneo ambalo wanadhani linawapatia nafuu zaidi katika imani yao kwa Mungu.

Kiongozi huyo wa Kanisa la Kiinjili alisema kwamba binadamu ana haki ya kuchagua njia anayoitaka ili kuboresha roho yake na upendo kwa mwenyezi Mungu.

 

Wamisionari wataka amani Congo

WAMISIONARI nchini Kongo wametoa rai ya kurejesha amani ya kudumu kwenye Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nchi ambayo tangu Agosti 2 mwaka huu imekumbwa na machafuko.

"Nchi hiyo ikiwa inakabiliwa na mauaji ya raia, uporaji na mateso, Wamisionari hawapaswi kukaa kimya," inasema taarifa iliyotolewa na ofisi ya habari ya Vatican.

Taarifa hiyo imenukuu maneno ya Maaskofu wakuu wa Kinshasa, Kisangani na Bukavu kuwa Wamisionari wanapaswa kuwa sauti ya wale wasio na sauti na kutaka kumaliza mapigano, chuki na kisasi.

Taasisi za Kimisionari zimeutaka Umoja wa Mataifa, OAU, Umoja wa Ulaya kuingilia kati ili kuhakikisha kuwa mapigano yanasitishwa karibuni.