MICHUANO YA KOMBE LA MATAIFA AFRIKA:

Taifa Stars kigugumizi kikubwa kwa Wasudan

l Sudan kuwasili nchini Jumatano ijayo

  Na Lilian Timbuka

KIGUGUMIZI bado kingali kikiwakabili wachezaji na makocha wa Timu ya Taifa kuhusiana na pambano lao na Timu ya Taifa ya Sudan linalotarajiwa kufanyika nchini hapa Oktoba 12, mwaka huu jijini Mwanza.

Baadhi ya wachezaji waliozungumza na Gazeti hili kwa njia ya simu kutoka Mwanza ambako timu hiyo imeweka kambi tayari kwa pambano hilo, walisema ni vigumu kutabiri ushindi wa mechi hiyo.

Wachezaji hao walisema kuwa, maandalizi duni na ukosefu wa mechi kubwa za majaribio, ni miongoni mwa matatizo makubwa yanayotatanisha klabu na kuifanya ishindwe kujiamini kuwa itafanya vizuri.

“Mechi ni ngumu na haitabiriki kabisa labda tusubiri kwani mpira ni dakika 90 kule ndani ya Uwanja wa Kirumba. Suala la msingi washabiki na Watanzania kwa jumla, nikukubaliana na matokeo ya mechi hiyo,” alisema Steven Mapunda ambaye pia ni mchezaji wa Timu ya Simba ya jijini Dar es Salaam.

 Naye mshambuliaji machachari wa Timu ya Soka ya Yanga ya Dar es Salaam, Edibily Jonath Lunyamila, aliyeongezwa hivi karibuni katika kikosi cha Timu ya Taifa Stars, alisema ugumu uliopo ni kwamba Taifa Stars haifahamu mbinu za uchezaji kutoka kwa wapinzni wao.

  “Ni vigumu kutabiri au kulizungumzia pambano hilo kutokana na kutofahamu mbinu wanazotumia wapinzani wetu, hivyo hali hiyo inajenga mazingira magumu ya ushindi japokuwa hata wenzetu pia walifungwa katika mchezo wao na Timu ya Taifa ya Zambia kwa bao 1-0,” alitanabaisha winga huyo.

 Lunyamila alisema mchezo ni mashindano ambayo yanatakiwa apatikane mshindi na mshindwa, “Tunaenda kushindana, hivyo lazima awepo mtu atakayetoka akicheka na mwingine akiwa amenuna, kwa kufungwa au kufunga. Hali hiyo kwa upande wa Watanzania hatuwezi kuitabiri kutokana na maandalizi tuliyonayo,” alisema Lunyamila.

Mechi hiyo ambayo ni ya kusaka nafasi ya kushiriki mashindano ya kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika Mwaka 2004, katika michuano itakayofanyika nchini Tunisia, inatarajiwa kufanyika katika Uwanja wa C.C.M. Kirumba jijini Mwanza.

 Naye Dalphina Rubyema anaripoti kuwa; Timu ya Taifa ya Sudan inawasili Jijini Dar es Salaam Jumatano hii tayari kupambana na Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), katika kinyanga’anyiro cha  kuwania Kombe la Mataifa Afrika.

 Akizungumza na KIONGOZi jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Chama cha Soka nchini (FAT), Michael Wambura, alisema kuwa baada ya kuwasili jijini Da es Salaam, Timu hiyo ya Sudan itaondoka kesho yake kuelekea jijini Mwanza ambapo itaungana na timu ya Taifa Stars iliyoko Mwanza kwa takribani wiki mbili sasa.

Taifa Stars iko chini ya Kocha Mkuu, Salum Madadu na Msaidizi wake, Hafidh Badru. Taifa Stars ambayo bado inakumbuka kipigo cha kutisha kutoka kwa timu ya Taifa ya Benin hivi karibuni cha mabao 4-0, inatakiwa ishinde mechi hiyo ili iweze kuwafariji Watanzania na kujiwekea mazingira mazuri ya kusonga mbele.

Taifa Stars katika kundi lake, inaungana na timu za Benin, Sudan na Zambia na kati ya timu hizo nne, inatakiwa ipatikane timu moja ambayo itashiriki katika Fainali za Kombe la Mataifa Afrika zinazotarajiwa kufanyika nchini Tunisia.

Mechi hizo zinaendeshwa kwa mtindo wa ligi na timu inayoongoza katika kundi hilo ni Benin kwa kuwa na pointi 3 na magoli 4 ya kufunga.

Nafasi ya pili inachukuliwa na Timu ya Zambia ambayo nayo ina pointi 3 na goli moja la kufunga ikifuatiwa na Timu za Sudan na Tanzania ambazo zote hazina pointi wala magoli ya kufunga zaidi ya kufungwa. 

Wachezaji wa zamani wataka washirikishwe katika michezo

Na Thadeo Malashala, DSJ

VIONGOZI wa Vyama vya Michezo mbalimbali nchini wameshauriwa kuwashirikisha wachezaji wa zamani katika kutoa maoni juu ya namna bora ya kuendeleza michezo hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Kocha wa zamani wa timu ya Yanga , Mkwavi Majimengi, wakati akizungumza na KIONGOZI jijini Dar es Salaam.

Majimengi ambaye pia aliwahi kuichezea timu ya Mkoa wa Dar es Salaam na Tanga, alisema kuwa, kuwashirikisha wachezaji wa zamani katika masuala mbalimbali, ni sehemu ya kuwaenzi wachezaji hao na kupata mchango wao katika kuboresha michezo nchini.

“Mimi ningoeomba Serikali iliweke wazi suala hili kama sehemu ya  kuwaenzi wachezaji wa zamani yaani maveterani na hata kufaidi mchango wao hata wa kimawazo,” alisema.  Aidha, Majimengi alisema kuwa timu za mavetereni zimeandaa mechi ya kirafiki itakayofanyika hivi karibuni huko Rufiji.

Alizitaja timu hizo kuwa ni Tanzania Legands, itakayomenyana na Timu ya Ijumaa Sports Club.   

 Majimengi aliyataja majina ya maveterani watakaoshiriki mechi hiyo ya kirafika kuwa ni Maulidi Dilunga, Rasuendee, Maulidi Abedi, Fundi   Magota, Lukas  Nkondoa,  Sunday Juma, James Kisaka na Rajabu  Rashidi.

Wengine ni Said Mwamba Kizota, Sebastian Nkoma, Mhidin Siso, Yasin Napili, Jumanne Shengo, Malota  Soma, Abubakari Salum, Juma  Mkambi, Makumbi Juma, Omary  Hussein na Ramadhani Nkumba.

Serikali yatakiwa iendeleze soka si kuitelekeza

Na Godwin Kaijage, DSJ

IMEELEZWA kuwa moja ya sababu zinazochangia kufungwa kwa Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Satars,) katika michuano ya Kimataifa,ni maandalizi hafifu.

Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa juma na mchezaji wa zamani wa soka nchini, Omari Pazi wakati akizungumza na Mwandishi wa habari hizi jijini Dar es Salaam.

Pazi alisema kuwa timu ya Taifa inapaswa kuandaliwa katika kipindi kirefu kabla ya mashindano na si vingine kwani kinume na hivyo, ndipo hutokea hatari ya kufungiwa rundo la magoli.

“Si kama inavyoendeshwa hivi sasa ambapo timu hupewa maandalizi ya muda mfupi ya   wiki mbili tu, hali aliyosema inasababisha jahazi la soka kuzama,” alisema.

Vile vile, alitoa changamoto kwa Serikali kulivalia njuga suala la kuunua mchezo wa kambumbu badala ya kuutelekeza. “Kwanini jamani hata sisi Tanzania tusisikike katika mataifa mbalimbali kwamba nasi ni vinara wa soka?” Alihoji.

Aliongeza, “Angalia soka linalochezwa na wachezaji wa Afrika ya Kusini, Senegal, Nigeria na nchi nyingine Afrika. Wanasakata kambumbu safi”.

 Alisema hivi sasa kuna vilabu vingi tofauti na zamani ambapo mtu kupata nafasi ya kuchezea timu fulani, ilitakiwa mchezaji huyo afanye kazi ngumu kweli kweli, lakini akasema pamoja na wingi wa vilabu hivyo, bado soka linazidi kushuka kila kukicha.

“Zamani ili upate kuichezea timu ya Simba ama Yanga, ilibidi ufanye kazi ya ziada tofauti na wakati huu ambapo timu  ni nyigi na viongozi  wa soka hutembelea katika viwanja   mbalimbali na pale wanapovutiwa na wachezaji hao huwasajili moja kwa mojakatika timu zao,” alisema.                   

Pazi katika  mchango  wa kuleta maendeleo ya  soka nchini, alifundisha timu za Mogo na Black  People zilizoko Ukonga  jijini Dar  es  Salaam.

Matumizi mabaya ya fedha, chanzo cha wadhamini kutodhamini michezo-Rais Yanga

MATUMIZI mabaya ya fedha za wadhamini ni moja ya vikwazo vya wadhamini kukwepa udhamini wa vilabu vya michezo nchini, anaripoti Lilian Timbuka.

Rais wa Klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam, Abbas Tarimba, alisema wakati akizungumza na Mwandishi wa habari yalipo Makao Makuu ya Yanga, Jangwani jijin Dar es Salaam.

Alisema imekuwa kawaida kwa viongozi wa vilabu mbalimbali vya michezo na vyama vya michezo, kutumia vibaya fedha wanazopewa na wafadhili wanaojitokeza kudhamini michezo.

“Viongozi waliopo madarakani wanapungukiwa na sifa za kuwa viongozi kwa sababu wanavunja mikataba ya awali, kwa mfano hivi sasa FAT tayari wamekiuka na tayari wamekwisha tumia pesa za vilabu kwa ajili ya nauli kwa matumizi mengine ambayo yako nje ya mkataba na VODACOM,” alisema.

Alisema Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ambayo awali ilidhamini Ligi Kuu Tanzania Bara, iliamua kuvunja mkataba huo baada ya FAT kushindwa kutimiza masharti ya mkataba katika Ligi Kuu mwaka jana ya Hatua ya Sita Bora, ambapo FAT iliongeza timu 8 badala ya sita bila kuwaarifu wadhamini hao.

“FAT walipewa fedha na wadhamini wa ligi hiyo ambao ni VODACOM kwa mujibu wa mkataba, lakini wao wamezitumia fedha hizo kinyume,” alisema.

Alisema katika hali kama hii, Tanzania isitegemee kuendelea katika soka kwa kuwa inao baadhi ya viongozi ambao ni wababaishaji na wasiojua matumizi ya fedha na wasiothamini mikataba hata siku moja.

“Mimi naungana na Waziri Mkuu kuwa viongozi wetu wana ubinafsi na wanaopenda kugonganisha vilabu na wadhamini,” alisema Rais huyo ya Yanga.

Hivi  karibuni FAT ilikiri kutumia pesa za nauli za vilabu zilizotolewa na VODACOM kwa matumizi mengine ambayo hayakubainishwa na Chama hicho, ambapo Katibu Mkuu wa chama hicho, Michael Wambura aliahidi kuzirejesha pesa hizo kwa vilabu shiriki kabla ya Ligi hiyo kuendelea tena hapo Oktoba 16.

Kwa hivi sasa Ligi hiyo imesimamishwa kutokana na kuipa nafasi Timu ya Taifa ambayo inakabiliwa na mechi ya Kimataifa inayotarajiwa kufanyika Oktoba 12, dhidi ya timu ya Taifa ya Sudan.

 

It is prepared by Miss. Christina Nyambo. Authorised and run by Rev. Fr. Revocatus Makonge, Exec. Sec. of the Communications Department of TEC.

 

Please visit the TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE WEB SITE