KAULI YETU

SERIKALI: Hivi Sekondari ya Shauritanga kuna nini?

 

MWISHONI mwa juma, Watanzania walikumbwa na mshituko mwingine mkubwa baada ya vyombo vya habari kuripoti juu ya ajali ya moto iliyotokea katika shule ya Sekondari ya Wasichana ya Shauritanga iliyopo Tarafa ya Mashati, wilayani Rombo katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Tukio hilo la Jumatano jioni, liliongeza simanzi kwa Watanzania na kikubwa zaidi, kwa wanafunzi wa shule hiyo walionusurika kufa kufuatia mabweni sita kuteketezwa katika ajali hiyo ya moto.

Tukio hili limekuja wakati hata machozi ya Watanzania yaliyotokana na ajali nyingine kama hiyo iliyotokea katika shule hiyohiyo mwaka 1994, hayajakauka.

Tunasema hivyo kwani, katika tukio hilo la mwaka 1994, wanafunzi 43 walifariki dunia.

Kwa mtazamo wa haraka, ni wazi kila mtu anaona kuwa huenda ajali ya 1994, ilikuwa na wingu la utata kwani licha ya Serikali kuunda tume ya kuchunguza tukio hilo, hadi sasa hakuna taarifa sahihi zilizotolewa na hii inatia shaka.

Tunasema inatia shaka kwani licha ya miili iliyogundulika kufa katika mabweni yaliyoteketea kwa moto katika tukio hilo kuwa 43,  bado wanafunzi wa shule hiyo waliotambuliwa walikuwa 41; wawili hadi sasa bado ni kitendawili.

Tukio la wiki iliyopita lililowafanya wanafunzi kukosa mahali pa kulala na kupoteza mali zao zikiwamo pesa, na kuwafanya wabaki na nguo walizokuwa nazo wakati wa tukio walipokuwa katika masomo ya jioni. Inasikitisha mno.

Tunasema linasikitisha mno kwani hivi sasa wanafunzi hao wamehifadhiwa katika ukumbi wa mikutano wa shule hiyo uliozinduliwa hivi karibuni na Rais Benjamin Mkapa huku wakiimba nyimbo za kumsifu Mwenyezi Mungu kwa kuzinusuru roho zao.

Wanafunzi hao wanakesha na kushinda kwa nyimbo hizo huku wakiwa wamevaa nguo pekee walizobaki nazo na ambazo ndizo pekee walizokuwa wamevaa wakati janga hilo linatokea. Hii ni kusema kuwa sasa hawana nguo hata moja ya kubadili.

Kinachotia wingu la utata katika tukio hilo, ni taarifa ya Mkuu wa Shule hiyo aliyekaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa ni vigumu kuamini kuwa tukio hilo limetokana na hitilafu ya umeme.

Mkuu huyo alisema kuwa kasi ya moto iliyokuwapo, kutokuwapo kwa wanafunzi mabwenini wakati wa tukio, pamoja na mabweni kutokuwa na swichi hata moja, ni mambo yanayoashiria kuwa tukio hilo sio la kawaida kwani uwashaji na uzimaji wa taa hudhibitiwa katika ofisi ya mwalimu wa zamu.

Kama hivyo ndivyo, ni vigumu kufikiri kuwa pengine kulikuwa na mwanafunzi aliyejaribu kufanya utundu wowote na hivyo, kugusa waya au kusababisha hitilafu yoyote ya kiufundi.

Sisi tunasema, kama hivyo ndivyo, tatizo liko wapi katika shule hiyo na habari za moto kuunguza mabweni ya Shauritanga, zitakoma lini kusikika masikioni mwa Watanzania?

Huku tukimshukuru Mungu kwa kutumia nguvu na mapenzi yake kuwaepusha wanafunzi wote kutoteketea hata mmoja katika moto huo, tunasema, tunajua upo uwezekano wa Serikali kuunda tume nyingine kuchunguza ajali hiyo, hatukatai lakini, wingi wa tume za uchunguzi zisizotoa taarifa sahihi na njia za kukomesha majanga kama hayo, unawasaidije Watanzania?

Tunatoa wito kwa Serikali  asasi mbalimbali za kidini, kibinafsi na watu wote wenye mapenzi mema, kuwapa misaada mbalimbali vijana hao ambao sasa wanaishi katika mazingira magumu. Kila mmoja ajue kuwa kutoa ni moyo na wala si utajiri.

Pia, tunatoa wito kwa Serikali kuzingatia usemi kuwa, dalili ya mvua, ni mawingu. Hii yaweza kuwa ni ishara za mwanzo za janga kubwa zaidi kutokea katika shule hiyo.

Ni vema uchunguzi wa kina ufanywe ili kubaini asili ya ajali za moto katika shule hiyo. Uchunguzi ufanywe kuanzia kwa masuala ya kiufundi na pia, uchunguzi wa kina wa kihistoria ufanywe ili kubaini uhusiano wa shule hiyo na jamii nyingine tangu siku za nyuma.

Sisi tunasema, tukio hili lisipotoa fundisho kubwa na kuifanya Serikali kuchambua toka matandu hadi makoko ya ukweli juu ya shule hiyo, tujue kuwa hii ni rasharasha, masika inakuja.

Serikali ijiulize, kwanini Shauritanga iwe kisima cha historia ya majanga ya moto katika shule za sekondari?

Hatusemi kuwa juhudi zielekezwe kwa shule hiyo ya Shauritanga pekee katika kuchukua tahadhari, bali pia Watanzania wazingatie kuwa mwenzio akinyolewa, wewe tia maji, hivyo shule nyingine zote nchini zizinduke na kuwa macho zaidi.

Hata hivyo, tumshukuru Mungu kwa kuzinusuru roho za vijana wetu ingawa bado tunaiuliza Serikali, HIVI SHAURITANGA KUNA NINI?

MUNGU IBARIKI TANZANIA.

BARUA

FAT msitake kumnenepesha ng'ombe siku ya mnada

Ndugu Mhariri,

 

Napenda kujitokeza katika Gazeti lako, ambalo sasa linaibuka kwa kasi kuingia katika ushindani wa kibiashara ili nilitumie kutoa maoni yangu.

Timu yetu ya  Soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Oktoba 12, mwaka huu, inatarajia kujitupa katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, ili kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.

Taifa Stars imepangwa katika kundi la tatu pamoja na Sudan, Benin na Zambia huku kila moja ikiwania kushiriki michezo ya Fainali itakayofanyika Tunisia mwaka 2004.

Mchezo wa Taifa Stars na Sudan utakuwa wa pili kwa timu hizo ambazo zilipoteza michezo yao iliyofanyika Septamba 8, mwaka huu.

Katika mchezo huo, Taifa Stars ilifungwa na Benin mabao 4-0 mjini Cotonou, wakati Sudan ilipata kipigo cha bao 1-0 na Zambia.

Kutokana na kufungwa mabao 4-0, uongozi wa Chama cha Soka nchini (FAT) ulikutana na Kocha Mkuu Salum Madadi ambaye aliongeza wachezaji kadhaa Taifa Stars.

Kuna baadhi ya wachezaji ambao walipunguzwa na wengine kuongezwa na kuifanya timu hiyo, sasa kuwa na wachezaji 29.

Timu hiyo imeweka kambi mjini Mwanza ikijiandaa na pambano hilo linalotarajiwa kuwa gumu, ingawa kwa upande mwingine Taifa Stars ina faida zaidi kwani itakuwa nyumbani.

Wasiwasi wangu ni kwamba, maandalizi ya timu hiyo yamekuwa ya mashaka na sijui kama kweli ina lengo la kushinda mchezo huo ama inakusudia kusindikiza katika staili ya Life Goes On yaani, bora maisha?

Ninasema hivyo kwani hadi sasa ninashangaa kuona kuwa, FAT imetangaza kwamba timu hiyo itasafiri mpaka Uganda kwa ajili ya kucheza mechi ya kirafiki na timu ya Taifa hilo ‘The Cranes’.

Pambano hilo kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa FAT Michael Wambura, limepangwa kufanyika Oktoba 9. Kinachonishangaza zaidi ni kwamba, mechi hiyo ya kirafiki itafanyika Jumatano ya Oktoba 9 na pambano dhidi  ya Sudan litafanyika siku ya tatu baadaye yaani, Jumapili ya Oktoba 13.

Hatuelewi kwa nini imekubali mwaliko huo bila kwanza kutafakari faida na hasara ambazo zitapatikana kwa wachezaji kucheza mechi hiyo ya kirafiki ambayo hatuamini kama ina faida yoyote kwa sasa.

Ikumbukwe kuwa Uganda ilikataa kucheza na Taifa Stars katika mechi za majaribio kwa madai imebanwa na ratiba, hivyo isingekuwa tayari kucheza.

Inashangaza kuona FAT imekubali haraka kwenda Uganda  huku ikijua kuwa Taifa Stars itakuwa na siku tatu tu, kabla ya kucheza na Sudan.

Mimi ninasema mechi kama hizo hazina tofauti na mwanafunzi anayekesha siku ya mtihani bila maandalizi bora ya awali hali ambayo ni sawa na kutaka kumnenepesha ng’ombe siku ya mnada.

 Ninasema hivyo nikijua kuwa ingawa siombei baya kwa timu yetu lakini, safari ni safari. Lolote laweza kutokea wakati wowote ikiwa ni pamoja na kuchelewa kunakoweza kusababishwa na tatizo la usafiri.

Kuna hatari ya kuwachosha wachezaji katika siku yenyewe hasa na kibaya zaidi, hata kama mchezaji kaumia, muda huo uliobaki  hautoshi kumpa matibabu na mazoezi ili ashiriki vema katika Uwanja wa CCM-Kirumba kuvaana na Sudan!

Ni vizuri kujiandaa kwa mazoezi kama hayo, lakini muda wote timu inakuwa wapi isifanye michezo ya kirafiki hadi dakika za mwisho za kuingia katika pambano kubwa?

Ninashindwa kujua kama mpango huo unalenga kujenga na utetezi na visingizio mara ikitokea timu yetu ikafungwa au la.

Hivi kucheza mechi hiyo na Uganda kutaipa mazoezi timu yetu badala ya kuwapa wachezaji uchovu zaidi na hatimaye kushindwa kumudu pambano?

Lengo langu si kuipinga Taifa Stars kupata mechi za majaribio la hasha isipokuwa, wasiwasi wangu ni muda wa mechi hiyo.

Tukumbuke kuwa ng’ombe hanenepi siku ya mnada, hivyo tulitakiwa tuanze mapema zaidi?

Kama tunataka mechi za majaribio ni vema zikafanyika wiki moja kabla ya kupambana na Sudan, lakini si kusubiri siku tatu kabla ya pambano hilo kwani madhara yanaweza kutokea.

Tuaamini kuwa kikosi kizuri cha Taifa Stars hakiwezi kujengwa kwa kutegemea pambano la Uganda, hivyo ikiwezekana ni bora Stars isiende Uganda.

Ninaomba wahusika kuwa makini na maamuzi wanayoyatoa katika kipindi hiki.

 

 

Tinner Paul

S.L.P. 6202

Dar es Salaam

 

                               TAFAKARI YA WIKI

Walakini kwa habari ya mtu maskini uwe mvumilivu, na kumwongezea siku kwa huruma.

Umsaidie maskini kwa ajili ya amri; na kadiri ulivyo ukata wake usimfukuze mikono mitupu.

Poteza fedha zako kwa ajili ya ndugu yako na rafiki yako, zisiharibike kwa kutu chini ya jiwe

                                                                        Yoshua Bin Sira 29: 8-10.

Mambo mema mbele ya kinywa kilichofumbwa ni kama vyakula vilivyowekwa juu ya kaburi

                                                                                  Yoshua Bin Sira 30: 18

 

 

It is prepared by Miss. Christina Nyambo. Authorised and run by Rev. Fr. Revocatus Makonge, Exec. Sec. of the Communications Department of TEC.

 

Please visit the TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE WEB SITE