Tanzania inatekeleza ipasavyo Haki za Watoto?

 

TANZANIA ni miongoni mwa  nchi zilizotia  saini Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto.Tangu Mkataba huo usainiwe takribani miaka 12 sasa, kumekuwepo na mafanikio kiasi. Pamoja na mafanikio hayo kwa Tanzania baadhi ya vipengele vya Mkataba huo vimekuwa vikiyumba. Katika makala haya Dalphina Rubyema anaeleza zaidi.

HUWA ni furaha kwa wazazi na ndugu karibu wote mtoto wao ama wa kiume au wa kike, anapompata mwenzi na kutangaza posa kulingana na taratibu za kabila husika.

Furaha huongezeka wachumba hao wanapofunga pingu za maisha kwa taratibu za Kanisa.

Haishii kwa wazazi na ndugu pekee, bali furaha hiyo husambaa kwa kiasi kikubwa zaidi kwa wachumba hao ambao wengi wao huiona siku ya harusi kama ndoto isiyotarajiwa kuwa ingetimia.

Furaha hiyo sasa huwa mara dufu baada ya ndoa hiyo takatifu kushuhudiwa kanisani ikiwa imefuata taratibu za kijamii na kikubwa zaidi, taratibu za Kanisa kuanzia kwa wanandoa wenyewe kila mmoja kuahidi moyoni kuishi ndoa takatifu, kisha ikapata matunda ya watoto ambao ni ZAWADI TOKA kwa Mungu.

Ni wazi zawadi ya mtoto si kwamba huongeza furaha na upendo kwa wazazi pekee, bali hata kwa kanisa na hata jamii nyingine inayowazunguka.

Bila shaka hakuna ubishi kuwa hali ndani ya familia huonekana ni ya kuhuzunisha pale inapotokea mwanamke ameolewa na kupita kipindi cha miaka mitano bila kupata mtoto.

Mara nyingi mama hujisikia mpweke sana, wakati mwinginie hufikia hatua ya kujiona hafai mbele ya mumewe na ndugu ama jamii inayomzunguka.

Hata akiomba kitu fulani kutoka kwa mume wake, kinapokosekana hata kama ni kwa sababu nyingine za msingi, mwanamke huyo hujishuku kuwa pengine anaadhibiwa kwa mtindo huo kwa vile hajajaliwa kupata mtoto, na kwamba labda hafai.

Pia, baadhi ya wanaume kimakosa huona kuwa hicho ndicho kigezo sahihi cha kutafuta nyumba ndogo ama kuhalalisha ndoa za mitala bila kuzingatia kuwa wanakwenda kinyume na Yesu Kristo kwani hakuagiza mume kuwa na wake wawili au mke kuwa na waume wawili.

Bahati mbaya zaidi, baadhi ya wanaume wa namna hiyo, huchukua uamuzi huo mbovu kukimbilia nyumba ndogo au ndoa za mitala kwa kisingizia cha mwanamke kutozaa kabla hata ya uthibitisho wa kitaalamu ili kujua kwamba matatizo yapo kwa nani kwa mwanaume, au kwa mwanamke.

Hata hivyo, inasikitisha kuona kuwa ukosefu au kuchelewa kupata mtoto kunaleta mtafaruku kwa baadhi ya wanajamii, lakini eti wapo wanawake wengine wanaoza na kisha kuwatelekeza watoto wao chooni, jalalani na hata kwenye mifuko ya rambo mitaroni na vichochoroni.

Wazazi wengine wanadiriki kuwanyanyasa watoto wao kwa adhabu kali, kuwanyika haki ya elimu, chakula, maradhi na kibaya zaidi, kuwahusisha katika ajira mbaya za watoto.

Hali hii ni hatari sana kwani licha ya kuwaathiri kisaikolijia na kiafya, inaongeza tatizo la kasi ya ongezeko la watoto wa mitaani sambamba na ongezeko la uhalifu.

Uchunguzi unabaini kuwa chanzo cha watoto wa mitaani mara nyingi ni umaskini, uhamiaji, kuyumba kwa msimamo wa uhusiano thabiti wa ndoa, unyanyasaji ama ukatiri dhidi ya mtoto na tabia za kibinadamu.

 

Umaskini

 

Umaskini ukikidhiri kwenye jamii, baadhi ya watoto hukimbia nyumba zao ili kutafuta unafuu wa maisha na matokeo yake, wanaangukia katika mazingira magumu yasiyo na uhakika wa kula, kulala wala kuvaa.

Mfano, baadhi ya familia zisizo na uhakika wa kupata mlo kwa siku. Hali hii inawafanya wazazi wawe nje ya familia zao kwa lengo la kutafuta riziki.

Inapotokea wazazi hao wakapata kidogo, baadhi yao wanakuwa na tabia ya kukitumia hicho kidogo walichopata kwa ajili ya starehe na kusahau adha wanayoipata watoto huko nyumbani.

 

Uhamiaji:

 

Suala la uhamiaji zaidi linazihusu zile familia zitokazo maeneo ya vijijini kwenda mijini kwa matumaini ya kupata kazi na maisha mazuri.

Familia hizo zikisha fika mjini, mara nyingi mategemeo yake huwa tofauti. Badala ya kupata kazi, hujikuta wakihangaika mjini na matokeo yake, hukosa hata chakula na kujibanza kwenye vijumba duni. Hali inapozidi kuwa mbaya, wazazi huingia katika hatua ya kuwa ombaomba kazi ambayo huwashirikisha hata watoto.

Familia zisizo na msimamo:

Zipo pia familia ambazo maelewano baina ya baba na mama huwa mabaya na hali hiyo, inasababisha kutengana. Matokeo yake, wazazi hao sasa hujikuta wanaoa au kuolewa na watu wengine.

Watoto hujikuta wakilelewa ama na baba, au mama wa kambo na kwa vile walishazoea upendo wa wazazi wa pande zote, hujiona wakinyanyaswa na walezi wapya.

Watoto hao wanaadhibiwa bila sababu na ama baba, au mama wa kambo wakisimangwa kwa mambo na vitu vingi vikiwamo vyakula.

Katika kuepukana na adha hiyo, watoto hao huamua kukimbilia mjini na hivyo, kuwa ombaomba mitaani na matokeo yake ni kuishia huko huko mitaani.

 

Ukatiri dhidi wa watoto

 

Kuna baadhi ya wazazi ama walezi wenye tabia ya kutoa adhabu kali pindi mtoto anapofanya kosa. Eti mzazi ama mlezi anadiliki kumfunga kamba mtoto na kumtupa darini ama kumchalaza fimbo huku akiwa amening’iniza kichwa chini miguu juu eti kwa sababu tu, kaiba shilingi 500 ama pengine hata pungufu ya hapo.

Wazazi wengine pia hujaribu hata kuwachoma moto watoto wao na katika kuepuka adha kama hizo, watoto hujikuta wakizikimbia familia zao.

 

Tabia za binadamu

 

Baadhi ya wazazi ama walezi wengine, wanatabia za ajabu ambazo watoto hushindwa kuzivumilia na kujikuta wakikimbilia mitaani.

Mfano mzuri katika mkoa mmoja hapa nchini, baba mmoja alikuwa na tabia ya ulevi na uvutaji bangi. Baba huyo alijikuta akitengana na mkewe na kumwachia mtoto wa kiume.

Katika nyumba hiyo ambayo sasa baba alibaki na mtoto wake, alikuwa anaishi vile vile dada wa huyo baba ambaye pia naye ni mlevi wa kupindukia.

Siku moja baba huyo na dada yake (shangazi yake mtoto), walikunywa pombe na kulewa na katika hali ya ulevi walifikia hatua ya kuingiliana kimwili.

Katika hali isiyo ya kawaida, mtoto bila kufahamu nini kilichokuwa kikiendelea, aliingia ndani ghafla na kukuta wawili hawa wakiwa wanaendelea kufanya dhambi zao.

Kwa woga na aibu, mtoto alitoka nje na ghafla shangazi yake alimfuata na kuanza kumkalipia eti kwa vile aliingia ndani pasi kubisha hodi.

Katika hali ya kupunguza aibu, shangazi mtu alimtaka mtoto huyo asimwambie mtu yoyote kuhusu tukio hilo na alimtishia kuwa akisikia kwa mtu, mtoto huyo angechinjwa.

Mtoto baada ya kutishiwa hivyo, aliona maisha yake sasa yamo hatarini, akaona heri atoe taarifa kwa balozi wa eneo hilo.

Balozi akamtaka huyo mtoto angozane naye hadi kwa wazazi wake (baba na shangazi yake) ili apate uhakika.

Kwa kuzingatia jinsi alivyoambiwa na shangazi yake kwamba “Ukimwambia mtu utachinjwa,” mtoto aliona sasa wakati wa kuchinjwa umefika na katika kuepuka balaa hilo, akaona heri akimbie eneo la nyumbani na kuishia zake mitaani.

Kufuatia mfano huo, ni dhairi kuwa mbali na baadhi ya watoto kukimbilia mitaani,pia hata wale ambao hubaki nyumbani kwa wazazi ama walezi wao, baadhi yao hukumbwa na matatizo mbalimbali.

Moja ya matatizo haya ni yale ya unyanyaswaji wa kijinsia likiwemo suala la ubakaji.

Uchunguzi umebaini kuwa vitendo vya ubakaji kwa watoto ni siri na  mara nyingi hufanywa na  ndugu wa karibu.

Umebaini pia kuwa, kutokana na wazazi kutokuwa karibu na watoto wao, watoto wanaofanyiwa vitendo hivyo hukosa nafasi ya kuwaelezea masuala yao ya ndani.

Katika kuhakikisha kila mtoto anatendewa haki, nchi nyingi duniani ziliona kuna haja ya kuweka Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto.

Mkataba huo wenye kubeba mawazo na imani za jamii, kabila na dini mbalimbali kuhusu watoto na jinsi gani wanatakiwa kulelewa, uliidhinishwa Novemba 20, mwaka 1989.

Tanzania ilitia saini Mkataba huo wenye kuidhinishwa na nchi 190. Ilitia saini yake Juni Mosi, 1990 na kuuridhia Juni 10,1991.

Kituo cha Kutetea Haki za Watoto nchini (KULEANA), kinabainisha kuwa ingawa Tanzania na nchi nyingine nyingi zimeridhia Mkataba huo, watoto wengi bado hawana haki.

Kituo hicho kinazidi kubainisha kuwa, kwa nchi maskini kama Tanzania ni vigumu kwa Serikali kutimiza haki zote zilizotajwa katika Mkataba huo.

Afisa Uhusiano wa Kituo hicho tawi la Dar es Salaam, Bw. Abdalah Ibrahimu, anasema kuwa Mkataba unatambua kuwa watoto wanahitaji kukua katika familia ambamo kuna furaha, upendo na maelewano.

“Watoto wanahitaji amani, heshima, kukubalika, uhuru, usawa na msaada. Wanahitaji haki hizo zote ili wakikua , waweze kuchangia katika ujenzi wa jamii bora,” anasema Ibrahimu.

Bw. Ibrahimu anaongeza kuwa, ili Mkataba huo utekelezwa ipasavyo, Serikali ya Tanzania haina budi kwanza kubadili baadhi ya vipengele vya sheria ili vitosheleze Mkataba huo.

Anatoa wito kwa Mashrika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs), na asasi mbalimbali kuweka kampeni ili Serikali ione umuhimu wa kuweka miundombinu madhubuti katika kutekeleza sawia Mkataba huo wa watoto nchini.

Kuhusu haki ya watoto kupata elimu na afya, Bw. Ibrahamu, anasema kuwa kwa kiasi kikubwa Serikali imefanikiwa kutekeleza masuala hayo zaidi kwa kufuata shule za Msingi.

Alisema, “Tunachoishauri Serikali ni kwamba, watoto washirikishwe kutoa ushauri wao kuhusu suala la ufundishaji na mazingira ya kufundishia.”

Anasema licha ya Serikali kutoa mwongozo kwamba mipango yote ya shule lazima iwashirikishe watoto wawili, akiwemo wa kike mmoja na wa kiume, lakini bado namba ya wawakilishi wa wanafunzi hao ni ndogo na uwezo wao wa kushiriki pia ni mdogo.

“Katika mpango huo unaojulikana kama Mpango wa Jumla wa Maendeleo ya Shule, sina uhakika kama wanafunzi wawakilishi kama wanajengewa uwezo wa kushiriki katika vikao hivyo, achia mbali suala la namba yao kuwa ndogo,” anasema.

Miongoni mwa vipengele vya Mkataba huo ambavyo kwa upande wa Tanzania bado havitekelezwi ipasavyo, ni pamoja na haki ya mtoto kupata hifadhi ya jamii.

Katika kipengele hicho, Mkataba unasema kuwa mtoto ana haki ya kupata hifadhi ya jamii kutoka Serikalini. Hifadhi ya jamii inaweza kuwa fedha taslimu au huduma zitolewazo na Serikali ili kukidhi mahitaji ya mtoto.

Kipengele hicho, pia kinaeleza kuwa kama wazazi au walezi wa mtoto hawana uwezo, Serikali ina wajibu wa kumsaidia mtoto huyo chini ya utaratibu wa hifadhi ya jamii iliyopo.

Kuongezeka kwa watoto wa mitaani kila kukicha, kunaonesha jinsi gani Tanzania isivyoutekeleza ipasavyo Mkataba huo wa Kimataifa juu ya Haki za Watoto.

Aidha, suala la kipengele kinachohusu Haki ya mtoto kulindwa dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia likiwemo suala la kujamiiana, bado kwa upande wa Tanzania linaleta utata.

Wakati mwaka 1998, Bunge la Tanzania lilipitisha Sheria Maalum inayomlinda mtoto dhidi asibakwe au kunajisiwa. Hata hivyo, bado idadi kubwa ya watoto wanabakwa na wahusika wa vitendo hivyo ni ndugu wa karibu wa mtoto.

Inasikitisha kuona kuwa, vitendo hivi vimekuwa vikimalizwa kimya kimya bila mtoto aliyebakwa ama kunajisiwa, kupewa fursa na uhuru wa kujieleza.

Mtoto aliyebakwa hubaki na kidonda kisichofutika ndani ya roho yake.

Hii ni kutokana na kashfa ya kubakwa kubaki pale pale huku mhusika (mbakaji), akiwa huru kwani kesi yake inaishia katika jamii inayomzunguka.

Umefika wakati sasa jamii ikaunganisha nguvu kukemea vitendo vya ubakaji na unajisi wa watoto wadogo kwani ni hatari kimwili na kiroho kwa mtenda na mtendewa.

Vatican yachambua Mkutano wa Maendeleo Endelevu (3)

Na Mwandishi Wetu

Katika mwaka 1995, Papa Yohane Paulo wa Pili aliongelea upyaisho wa roho ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa: “Umoja wa Mataifa, unahitaji kuinuka zaidi na zaidi. kupita hadhi ya taasisi ya utawala na kuwa kitovu cha maadili ambapo mataifa yote ya ulimwengu hujisikia nyumbani na kujenga utambuzi shirikishi wa kuwa, kama ilivyokuwa, ‘familia ya mataifa’. Dhana ya ‘familia’ mara moja inaamsha kitu zaidi ya uhusiano wa kikazi au mkusanyiko wa maslahi. Familia kwa asili ni jumuiya iliyojengeka katika misingi ya kuaminiana, kusaidiana na kuheshimiana. Katika familia halisi wenye nguvu hawatawali; badala yake wale wadhaifu kwa sababu ya udhaifu wao wanakaribishwa na kuhudumiwa.”

Katika ulimwengu wetu wa kutegemeana na utandawazi, ni roho hii ya “familia” ambayo ni lazima ikuzwe iwapo maendeleo ya kweli kuelekea malengo na mawazo ya maendeleo endelevu yanatakiwa kufikiwa. Ni pale tu ambapo kuna kuelewa mahitaji na mafanikio ya pamoja ndipo binadamu wanaweza kufikia ukamilifu wa maisha bora kwa watu wote wa ulimwengu, watu wote wa “familia ya mataifa.” Kwa kuunganisha dhana za mahitaji na mafanikio pamoja na dhana za kuaminiana, msaada na heshima, mchakato wa maendeleo endelevu hautaendelea tu mbele lakini utaimarishwa katika juhudi zake kuelekea uondoaji wa umaskini, utunzaji wa mazingira, ukuzaji wa haki za binadamu na heshima kamili kwa usawa shiriki wa binadamu.

Matokeo ya Mkutano huu ni lazima uweke lengo sahihi ili kufikia maendeleo ya watu kiuchumi na kijamii, mambo ambayo huunda msingi wa maendeleo endelevu.

Vatican inayatakia maazimio ya Mkutano huu kuwa hayatakuwa tu ya mafanikio lakini pia ya ugunduzi na kuangalia mbele na kwamba ahadi ambazo zitaibuka zitausukuma ulimwengu na watu mbele ili kuchangia kikweli katika maslahi ya kiroho na kimwili ya watu wote, familia na jumuiya zao.

Kusaidia katika ukamilifu wa matumaini haya, katika mazingira ya Mkutano huu wa Dunia wa Maendeleo Endelevu Vatican inatoa wito wa “Paji la Nafsi”, kwa kuwa binadamu hawezi kujua vipaji vyake alivyo navyo isipokuwa tu katika kujitoa.

 Katika kukabiliana na ubinafsi na kutojali, “Paji la Nafsi” hatimaye huhakikisha maslahi ya wengine na ya vizazi vijavyo na hivi huchangia kwenye maendeleo endelevu. Dhana hii ni msingi wa aina nyingine za mashirika ya hiari na mwamko ambao Mkutano wa Dunia wa Maendeleo Endelevu unapenda kuendeleza na kukuza.

“Paji la Nafsi” ni matumizi bora ya uhuru wa binadamu na msingi wa matendo kuelekea maendeleo mazima ya binadamu.

Msimamo huu wa Vatican juu ya kuhifadhi mazingira, unakuja huku Marekani mchafuzi mkubwa wa mazingira duniani ikiwa imegoma kuridhia itifaki ya Kyoto kuusu kuongezeka kwa joto duniani (The Kyoto Protocal on Global Warming).

Itifaki hiyo iliyofikiwa mwaka 2000 mjini Kyoto, Japan na kusainiwa na nchi zote zenye viwanda vingi duniani ikiwemo Marekani wakati huo ikiwa chini ya utawala wa Rais Bill Clinton.

Hata hivyo mkataba huo ulikumbana na kigingi baada ya Rais wa sasa wa Marekani George Bush kusema serikali yake isingeridhia itifaki hiyo na wala kuitekeleza kwa vile ina didimiza uchumi wake. Itifaki hiyo inahitaji kuridhiwa na angalau nchi 55 zenye viwanda vingi ambazo huchangia uharibifu katika utando wa Ozone ambao huikinga dunia kutopigwa na miali  ya jua ya moja kwa moja.

Kwa kuwa utando huo aidha umedhoofika au umetoboka sehemu fulanifalani, ndiyo maana kiwango cha joto duniani kimeripotiwa kuongezeka. Kutokana na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na gesi kutoka viwandani ambazo pia husababisha mabadiliko ya hali ya hewa, dunia imekuwa ikikumbwa na majanga mbalimbali kama vile ukama, mafuriko baa la njaa na mengine.

Huku Marekani ikiwa imegoma kutekeleza itifaki hiyo washirika wake katika Ulaya kupitia Umoja wa Ulaya walijitahidi kupunguza kiasi cha gesi hatari zinazoingia angani kwa robotatu ya kiwango ambacho walichotakiwa kupunguza.

Pia Japan mshirika wa Marekani kibiashara inaripotiwa kuwa ilijitahidi kupunguza kiasi hicho kwa kiwango cha kuridhisha.

Marekani kwa upande wake ilitakiwa kupunguza kiwango cha hadi asilimia saba ya gesi ambazo huzalishwa na viwanda mbalimbali nchini humo. Nchi hiyo yenye uchumi mkubwa duniani ikifuatiwa na Japan, peke yake huzalisha hadi asilimia 25 ya gesi hatari kwa mazingira ya dunia.

Ili kuwepa hata kuzungumzia suala hilo Marekani imekuwa ikitafuta visingizio mbalimbali vya hata kutozungumzia suala hilo. itakumbukwa kwamba huku mjadala juu ya suala hilo ukiwa umepamba moto, Marekani iliibua suala la kujenga mfumo wa ngao ya kujilinda kiusalama dhidi ya makombora. hatua hiyo ilikuwa ni ukiukwaji wa wazi wa mkataba dhidi ya silaha za nyukilia wa mwaka 1976 (The Anti-Baltic Missiles Treaty)

Wakati ikiwa katika ujenzi wa mfumo huo wa kujilinda na tayari imefanya jaribio moja lililodaiwa kufanikiwa nchi hiyo kubwa duniani ilishambuliwa kigaidi hapo Septemba 11 mwaka jana, shambulizi hilo lilisababisha upotevu mkubwa wa maisha na uharibifu wa mali. Shambulizi hilo lilithibitisha kwamba hakuna nchi inayoweza usimama peke yake duniani hata kama ina silaha kiasi gani, kuwa salama.

Huku ikijua kuwa Mkutano wa Maendeleo Endelevu ambao mazingira ilikiwa ni moja ya mada zake kuu Marekani iliiibua suala la Iraq ili kuepa mada hiyo ya mazingira. Si tu Marekani iliepa mada hiyo bali hata Rais Bush hakuhudhuria mkutano huo muhimu kwa maendeleo ya haki duniani uliofanyika Johanesburg Afrika Kusini.

Katika Mkutano huo, Bush alimtuma Waziri wake wa Kigeni Jenerali Collin Powell aliyekuja na kejeli dhidi ya hatua mwafaka za kutunza mazingira na kuishia kuzomewa pale alipokuwa akitoa hotuba.

UCHAMBUZI WA KITABU

Tamthilia na Ulimwengu Ulivyo Sasa

 

Kitabu:   Kivuli Kinaishi

Mwandishi:                  Said A. Mohamed

Mhakiki: Projest M. Christopher

 

Utangulizi

 

Ukisoma Tamthiliya hi,i utaona kuwa hakuna marefu yasiyo na ncha na kwamba, wakati ukishawadia umewadia. Bi. Kirembwe anayejiita mungu wa miungu, mfalme wa wafalme na malkia anayetazamia kukalia kiti cha uongozi daima na dawamu.

Kama nilivyokwisha kusema kuwa, haki ikishindana na dhuluma mara nyingi haki hushinda. Mtolewa na Wazi wanashirikiana na kuuangusha uongozi wa Bi. Kirembwe anayetawala Giningi kwa imani ya kichawi.

Uongozi mbaya: Waandishi wa Fasihi ya Kiswahili wamejihusisha mno na suala hili na huku kila mmoja akilinyooshea kidole. Bi. Kirembwe aliyejifanya Giningi himaya yake na kujitwalia madaraka yasiyosemeka mara mchawi, hakimu, malkia na pia mfalme kama msanii anavyosema:

“Mama … baba…. Mama upande mmoja na baba upande mwingine mama  na baba wakati mmoja” (Uk. 33).

“…..Mimi malkia wa wachawi…..” (Uk 42)

“Nimechukua umbo la uhakimu kwa sababu hakuna hakimu atakayenizidi mimi mkuu wa mahakimu….” (Uk. 66).

Bi. Kirembwe ana uchu wa madaraka na anajiita Kiongozi wa milele wa Giningi, anawaangamiza wale wote wanaojaribu kumshauri au kumhoji kuhusu madaraka hayo.

“Mmelaaniwa na wazee wetu… walinzi! Tusiwaone hawa…” Uk. 76. kwa Wanaginingi kama vile dawa, trekta, mbolea na chaki. Msanii anasema: “Lakini tuliambiwa tutapewa matrekta… tutaletewa mbolea za Kizungu hatukuletwa kumwagilia…” (Uk. 18).

“…Viti vya kukalia wanafunzi wala meza … pia hakuna vitabu… hakuna chaki za kuandika….” (Uk. 21-22)

“…Dawa nyingine hazipatikani hapa… (Uk. 23).

Mara ngapi katika jamii zetu wananchi wanalia na uongozi mbaya, nchi ngapi za ulimwengu huu zinapigana vita ili kuuangusha utawala wa ki-dikteta mfano Madagascar, Angola, Iraq, Nigeria na kwingineko?

Viongozi wa namna hii tunao wengi katika jamii zetu wenye vyeo vya maajabu; mara yeye waziri mara mkuu wa idara fulani wakati huo huo, ana kofia ya ualimu au udaktari.

Hivi kweli katika mfumo huu wa uongozi kazi zinaweza kutekelezeka? Vile vile, tunao viongozi wakorofi na wakatiliki.

Wengineni wakatili sana hasa unapojaribu kuwapa ushauri kama afanyavyo Bi. Kirembwe kwa wazee  na pale anapowaadhibu mwalimu, mtibabu na daktari: “…Adhabu kali ya kukatwa ulimi unaoringia unapokuwa darasani (Uk. 68).

Ingekuwa heri sana Tamathiliya hii iwapashe viongozi wetu wanaong’ang’ania madaraka kabla wakati haujawadia na kabla ya kelele za wakati hazijaanza: “….Ni kelele za wakati na kelele za wakati hazizuiliki…” (Uk. 119).

 

Rushwa:

 

Inaonekana rushwa ni matokeo ya uongozi mbovu, la sivyo utakuwa uongo mpevu. Kulegalega kwa Bi. Kirembwe, kunawapa fursa viongozi wengine kula rushwa.

Bawabu anapokea rushwa wazi wazi toka kwa wafanyabiashara ili ayafiche maovu yao na wale wanaokosa kutoa rushwa, wanaandikwa kwenye kitabu cheusi kama wahalifu.

Msanii anasoma “…Nimekuletea vinono… vifaa vya nyumbani … nguo za watoto, sabuni … Uk. 29) .

Aidha, Mtolewa anatoa rushwa ya shilingi 5000/- ili aingie Giningi baada ya kupuuzwa na bawabu ll kwa hodi zake zisizo na kitu chochote.

Baada ya kutoa rushwa hiyo, bawabu anazinduka na kumpokea kwa sifa kedekede na kumsihi asijaribu kuwa dhaifu kwani: “Chini kuna udhia” (Uk. 30).

Giningi ni jamii ya kuthamini wenye nacho. Wasio nacho ndio watumwa. Wafanyabiashara wanapokewa kwa shangwe na bawabu II. Hii ni kwa sababu wanacho.

Lakini, sauti za wasio nacho zinasikika zikimpasha Bi. Kirembwe katika  Uk. 69. kuwa:

“Na iwapo mfanyabiashara anakuwa mghushi…na iwapo malkia wa Giningi anageuka mbwa mwitu nani atawalinda kondoo na kuwafuga”.

Sasa kama viongozi waliopewa dhamana ya kuwalinda kondoo wanageuka mbwa mwitu, nani atamfunga paka kengele. Ni wazi kabisa rushwa inahalisika katika jamii zetu.

Vyombo vya habari, mashirika na tume mbalimbali vimejitahidi kupambana na wala rushwa, kuwepo kwa Tume ya kupambana na rushwa nchini (PCB) kunatudhihirishia wazi kuwa, rushwa ipo katika nchi yetu. Kama isingekuwepo, basi na Tume hii isingeundwa.

Rushwa ni ya aina nyingi. Ipo rushwa ya pesa, mali au bidhaa na hata wengine wanadiriki kutoa miili yao kama rushwa!

Mara ngapi madaktari wameomba rushwa ili wagonjwa watibiwe, pia ureje wimbo wa ‘Wagosi Wa Kaya’ ‘Wauguzi’ hii inatupa hali halisi ilivyo katika jamii yetu.

Tuepukane kwa kupambana na wala rushwa kwani tunanunua haki zetu wenyewe. Mfano, Mtolewa ilikuwa haki yake kuingia Giningi bila kutoa chochote kwani mtihani wa Giningi alishafaulu.

 

Uchawi na ushirikina:

 

Dhana hii inajitokeza katika Tamthiliya hii kwani Giningi na hadithi yake ni ya kiuchawi tu. Watu wanageuzwa mazuzu ili wasijue linaloendelea. Nyeusi iwe nyeupe na nyeupe iwe nyeus,i pia nyekundu ni manjano daima. Watu wanapoonza kubaini maovu hayo wanaambiwa : “…mzugo wako unaanza kwisha…” (Uk.18).

Bi. Kirembwe anatumia unga wa ndere kuwazuga watu. Anafanya mazingaombwe ili hapana iwe ndiyo na ndiyo iwe hapana. Msanii anasema

“…Mimi Malkia wa wachawi” (Uk. 42)

“Haya leteni unga wa ndere”…(Uk 46)

“Unga wa ndere mziba kauli na mfungua kauli” (Uk 46).

“.. ndiye mchawi mkuu, ndiye mwenye kustahili kukalia kiti…” (Uk. 71).

“Wanatumia uchawi wa maneno kuwazuga wengine na wanatumia nguvu kuwadidimiza na kuwaangamiza wasiozugika…” (Uk. 80).

“…Kwa hiyo uchawi wowote una miko…” (Uk. 80)

“…. Mwenye uwezo wake bado uwezo wa kichawi …” (Uk. 82).

Dokezo, dondoo na nukuu hizi zinatuonesha wazi wazi lile lililokuwa linajiri katika jamii ya Giningi.

Itaendelea toleo lijalo

 

It is prepared by Miss. Christina Nyambo. Authorised and run by Rev. Fr. Revocatus Makonge, Exec. Sec. of the Communications Department of TEC.

 

Please visit the TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE WEB SITE