Uamsho ni Ulokole katika Ukatoliki?

l   Karismatiki ilianzishwa na Walokole

l  Sasa Walokole hujichomeka katika Uamsho wa Kikatoliki

l  ASKOFU: Chama cha kitume kinachodharau kingine marufuku

ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Method Kilaini na Mratibu wa Karismatiki Katoliki iliyopo Tanzania, Joseph Mshiri, wameweka wazi kuhusu kikundi cha Wanauamsho baada ya watu kutokielewa na kukitazama kama Ulokole ndani ya Ukatoliki.

                                           

Novatus Magege, muumini wa Parokia ya Kurasini, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, alipoulizwa anaijua vipi Karismatiki, alisema, “Hawa si ni Wanauamsho wa Kikatoliki.”

Kuhusu tofauti zao na Waprotestanti (Walokole), alisema.

“Tofauti yao ni kwamba Wanauamsho wanalitii Kanisa Katoliki na Walokole wao wana yao tu, hilo ndilo mimi ninafahamu.”

Bw. Joseph Magabe, wa Parokia ya Kiagata, Jimbo Katoliki la Musoma, yeye alipoulizwa kwa simu toka Musoma, alisema, “Kwa kweli hiyo Karismatiki mimi ninaisikia tu, sijui ni nini. Ila, nasikia wanafanya mambo kama Walokole. Sasa sijui vizuri labda wewe (mwandishi) unieleweshe vizuri.”

Mmoja wa waamini waliokuwa katika Mkutano wa Injili wa hivi karibuni uilofanyika katika Kanisa La Pentekoste Tanzania (KLPT), katika Parish ya Keko,jijini Dar es Salaam, alisikika akisema baada ya mkutano huo, “Mikutano ina faida bwana si unaona siku hizi hata Waromani (Wakatoliki) nao wanaifanya tunaona.”

Katika kutafuta ufafanuzi juu ya jambo hili linaloonekana kutoeleweka kwa jamii, kwa nyakati tofauti Gazeti la KIONGOZI lilikutana na Mratibu wa Karismatiki Bw. Mshiri.

Mshiri alisema, “… Wakarismatiki sio Walokole. Unajua wanaojiita Walokole sio dini wala dhehebu, hao ni watu wachache tu, wanaojiona kuwa wao ni cream yaani safi kabisa mbele ya Mungu kuliko watu wengine. Lakini, Wakarismatiki, kazi yao ni kutangaza Habari Njema.

Wana karama ya Kuhubiri Injili kwa kutumia zawadi (karama) za Roho Mtakatifu ambazo ndizo nyenzo maana Kristo anamuita kila mtu kumtumikia kwa karama yake na katika nafasi yake. Kama ni dereva aendeshe kama ni daktari, atibu watu.”

Akaongeza kuwa, “ Hawa wana karama ya kuhubiri na kuombea watu wengine hata wagonjwa.. .. hapa ni lazima kila mtu atambue ameitiwa nini katika kutumikia Ukristo.”

Kuhusu suala la kunena kwa lugha, Bw. Mshiri alikuwa na haya, ”Mtu anaanza mwenyewe kunena na wala sio kwamba anapata mafunzo mahali popote na ni vema hata Wakarismatiki wanajua wazi kuwa wakati mwingine, kunena kunaweza kuwakwaza watu wengine. Ndiyo maana hilo halifanyiki kanisani.”

Hata hivyo, anaongeza kuwa, “Kwa bahati mbaya ipo kasumba inayowanyemelea baadhi ya Wanakanisa kudhani kuwa Karismatiki ndiyo safi kuliko wengine na wengine wanapotoka kwa kudhani kuwa, kama mtu haneni kwa lugha, huyo eti hana Roho Mtakatifu. Hiyo si kweli. Hapo ndipo linakuja tatizo la watu wengine wenye karama kujiona wa juu kuliko watu wengine na hivyo, kuvunja umoja wa Kanisa.

Alisema kila Mkristo safi, hana budi kutodharau huduma ya mwingine.

Kuhusu kusali nje ya Kanisa, Bw. Mshiri alisema, “…Hatuwezi kuwafikia watu wengine wakiwamo Waislamu na wale wa madhehebu mengine kama hatutatoka nje ya kanisa kwa sababu, kanisani watu hawa hawaingii.”

 Kuhusu suala hilo, yafuatayo ni maneno halisi ya Mhashamu Method Kilaini, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, juu ya Karismatiki Katoliki

 “ILI kuelewa hili, kwanza tujue kwamba Kanisa Katoliki ni pana; na Mungu ni mpana  ambaye kila wakati tunajifunza kitu kimoja na kingine kuona jinsi gani kinaweza kuleta msisimko. Katika mafundisho ya Kanisa yapo mambo mengi sana, na katika nyakati mbalimbali za kihistoria, mara unakuta kipengele fulani kameshikwa, kipengele kingine kimeingizwa sana.

 Vyote hivi ni vipengele tofauti vya Kanisa hilo hilo ambalo linahamasisha Wakristo.

Unakuta wakati mwingine Moyo Mtakatifu wa Yesu, uliingia sana. Moyo Mtakatifu wa Mama maria ukaingia sana, Mtakatifu Anna na karama zake, ikaingia sana.

Katika kuelewa ukweli wa namna hiyo, tunaweza tukaelewa na Karismatiki.Kwanini Karismatiki inakuja leo; likuwa wapi na ilikuwa inafanya nini?

Karismatiki ni mojawapo ya vyama vya kitume ambavyo msisitizo wake unakuwa juu ya karama zake Roho Mtakatifu. Hii ina mwanzo wake kwani tangu mwanzoni mwa Kanisa, Wakristo wa mwanzo walisisitiza sana juu ya karama za  Roho Mtakatifu.”

Anaendelea,”Kadri Kanisa lilipoanza liliweka mpango mmoja baada ya mwingine ili kuweka msisitizo wa karama ya kujitoa, kumbe misisimko ya haraka haraka ikapungua na kuwepo mipangilio ambayo inafanya vitu vilivyopangwa; kwamba tunaposali tufanye hivi, tufanye vile, hapa tuinue nikono, hapa tuiweke chini, ambapo sasa unaona katika Kanisa la mwanzo wakati wanafanya ule msisimko wa Roho Mtakatifu, ilikuwa ni ile hisia. Walitumia sana ile hali ya hisia.

Na kadiri muda  ulivyokwenda hisia zilipungua na kukawepo na mipangilio ambayo inaeleweka. Lakini mara nyingine kuna uhitaji, hivyo katika kipindi tulichoingia  na hasa baada ya Mtaguso wa Pili, ikatokea nafasi kwamba watu wenyewe vilevile waanze kuleta hisia zao katika namna wanavyofundisha na wanavyotoa msimamo wa dini.

Na katika hisia zao, zikaja karama zake Roho Mtakatifu ambazo ni kuhubiri; mtu akijisikia anahubiri, mtu anapoimba anaweza akaruka.

Zamani walikwambia hata mikono uifunge namna gani, na uifunge kwa kiasi gani.

Haya ni mambo ya kihistoria kwa sababu haya ni mambo ya binadamu anavyoitikia wito wa Mungu kufuatana na nyakati zake kufuatana na hali yake.

Itaendelea Toleo lijalo

Wakazi watatu wahukumiwa kunyongwa Tarime

l Wawili waliua wake zao

Na Mwandishi Wetu, Tarime

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imewahuku kifo wakazi watatu wa Wilaya ya Tarime kwa kipindi cha wiki tatu kutokana na makosa tofauti ya mauaji ikiwa ni pamoja na wawili kuwaua wake zao.

 

Katika tukio la hivi karibuni Mahakama hiyo iliyokutana katika ukumbi wa Mahakama ya Wilaya ya Tarime, Oranda Nyakua (35), mkazi wa Utegi, wilayani hapa, alihukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mkewe, Pamela Nyakua, kwa kumkata panga.

 Akisoma hukumu hiyo katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime Jumatano iliyopita, Jaji John Mtolela, alisema Mahakama Kuu imetoa hukumu hiyo chini ya Kifungu cha 197 cha Kanuni ya Adhabu Namba 322 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa mashitaka uliotolewa mahakamani hapo.

 Awali, Wanasheria wa Serikali, Feleshi Mbuki na Deo Mgengeli, walidai mahakamani hapo kuwa, Oktoba 11, 1995, Saa 5:00 asubuhi, katika Kijiji cha Masike wilayani Tarime, mshitakiwa kwa makusudi alimvizia kisimani na kumkata kwa panga kichwani na katika mkono wa kushoto, mkewe, Pamela Nyakua, shambulio hilo lilisababisha kifo baada ya dakika chache.

 Katika tukio jingine, Septemba 27, mwaka huu, Mahakama Kuu hiyo ilitoa hukumu ya kumyonga hadi kufa, mkazi wa Kijiji cha Nyamaharaga, Wilaya ya Kehancha katika nchi jirani ya Kenya, Samsoni Buruna Sibare (47), baada ya kuua kwa kukusudia.

Ilidaiwa mahakamani hapo na wanasheria hao wa Serikali kuwa, Februari 19, 1990 mchana, kwa kushirikiana na nduguye, Sagore Buruna Sibare ambaye alitoroka, kwa kudhamiria walimkata kwa panga mguu wa kushoto na mgongoni, mkazi wa kijiji cha Ketenga Wilayani Tarime, Chacha Bisase na kumsababishia kifo saa mbili baadaye.

Katika tukio jingine, Septamba 30 mwaka huu, Mahakama Kuu hiyo ilimhukumu kunyongwa hadi kufa, mkazi wa Kijiji cha Tagota Wilayani Tarime, Lucas Kimito (69), baada ya kupatikana na kosa la kumuua mkewe Wagesa Kimito.

Mbele ya Jaji Mtolela, wanasheria wa Serikali waliimbia Mahakama Kuu kuwa, Machi 12, 1995 wakiwa nyumbani, kwa makusudi mshitakiwa huyo alimshambulia kwa ngumi na fagio hadi kumuua mkewe Wegesa Kimito baada ya kuzuka ugomvi wa kifamilia. 

SINODI YA UCHAGUZI  NA KATIBA:

Wamoravian hatima ya Kanisa lenu imo mikononi mwenu, lioneeni huruma

lWachungaji matumbo yawaka moto; Kitendawili cha nani atakuwa nani kigumu

Na Waandishi Wetu, Dar na Tukuyu

TANGU mwishoni mwa juma, Kanisa la Moravian Tanzania (KMT), Jimbo la Kusini; mji wa Tukuyu umekuwa na wageni mbalimbali wanaohudhuria Mkutano wa Sinodi ya Katiba na ile ya Uchaguzi Katika Kituo cha Mikutano cha Rutengano mjini Tukuyu, inayofanyika Oktoba 7 hadi 1 2, mwaka huu.

Sinodi hiyo inayofanyika nje kidogo ya mji wa Tukuyu kuelekea Kyela inawahusisha wajumbe zaidi ya 310, wakiwa ni wachungaji wa shirika zote za Jimbo zipatazo 155 wakiwa na mjumbe mmoja mmoja kutoka kila ushirika.

Viongozi wakuu wa KMT, Jimbo la Kusini yaani Askofu Lusekelo Mwakafwila, Mwenykiti wa Jimbo, Mchungaji Angetile Musomba na Katibu Mkuu, Mchungaji Nelsen Mwaisango, kwa nyakati tofauti mwaka huu, waliliambia KIONGOZI kuwa Sinodi ya Uchaguzi hukutana kila baada ya miaka minne wakati ile ya marekebisho ya Katiba hukutana kila baada ya miaka sita.

“Mwaka huu Sinodi zote mbili zimeangukia pamoja, ila itaanza hii ya Katiba kisha ifuate ya Uchaguzi,” alisema Mchungaji Musomba wakati akizungumza na KIONGOZI katika Sikukuu ya Pasaka Mwaka huu.

“Huo ni Mkutano mkubwa unaowachagua viongozi wote wa Jimbo, wakiwamo Wenyeviti wa Wilaya,” alisema Askofu Mwakafwila alipozungumza jijini Dar es Salaam, miezi michache iliyopita.

Naye Katibu Mkuu, Mchungaji Mwaisango, alisema jijini kuwa, “Wanaochaguliwa katika Sinodi ni Mwenyekiti wa Jimbo, Makamu Mwenyenyekiti, Katibu Mkuu na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Jimbo.”

Hadi hivi sasa, kila mtu anajiuliza nani ataibuka kiongozi katika uchaguzi huo na atachaguliwa kuongoza katika ngazi gani.

Kwa mujibu wa taratibu za KMT, hakuna kugombea nafasi yoyote hususan Mwenyekiti wa Jimbo au Wilaya, Makamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu.

Wajumbe wa Mkutano kila mmoja huandika kwa siri jina la mchungaji anayemtaka kuongoza kwa ngazi fulani na kisha huangaliwa wenye kura nyingi ambao hupigiwa tena kura za siri hadi anapopatikana kiongozi.

Kutoka  Tukuyu Mwandishi Wetu anajaribu kuelezea mtazamo wake na kukumbusha kidogo historia muhimu ya KMT jimboni humo. Endelea.

HIVI karibuni, jina la KMT, hususan Jimbo la Kusini, limekuwa likitajwa mara kwa mara katika vyombo kadha vya habari.

Tunafurahi kuona hivyo, hasa tunaposikia, kuona au kusoma habari  hizo zikiwa zinalihusu Kanisa, zikielezea maendeleo na kutoa changamoto zaidi kwa jamii ili kuimarisha maendeleo ya kiroho na kimwili.

Hata hivyo, kwa upande mwingine wa shilingi, habari  hizo zimekuwa ni zile ambazo, yeyote mwenye nia njema na KMT, hatamani kuendelea kuzisikia au kusoma.

Hii haitokani na ukweli kuwa zimepotoshwa, bali kutokana na kile kinachoelezwa hasa tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya uongozi katika KMT, jimboni Kusini.

Mara kwa mara vyombo hivyo, vimeripoti mapendekezo ya waamini wa KMT, jimboni wakiwamo wachungaji wakimtaka Mwenyekiti wa Jimbo la Kusini, Mchungaji Angetile Musomba, apumzike nafasi  yake ya Uongozi.

Katika kutoa sababu za madai ya waamini hao, wanadai Mchungaji Musomba, akiwa Mwenyekiti wa Jimbo (KMT), amekuwa akitoa nafasi za uwakilishi wa Jimbo katika Mikutano ya nje ya nchi, kwa upendeleo, pamoja na mengine yanayopingana na maadili ya Utumishi wa Mungu.

Katika hili, mimi sio hakimu wa kutoa hukumu juu ya nani ana ukweli wote isipokuwa pia, ninakumbuka dhahiri kuwa madai hayo, yalikanushwa na Askofu wa Jimbo hilo, Lusekelo Mwakafwila, pamoja na Mwenyekiti mwenyewe.

Kama hivyo ndivyo, wakati huyu anasema ndivyo, na huyu anasema sivyo, kuna kuelewana? Kama hakuna kuelewana, matokeo yake ni nini kwa Kanisa? Linajengeka au linabomoka? Lakini, kama linabomoka, Wamoravian hawaoni kuwa kuruhusu nyufa katika Kanisa ni aibu kwa Wakristo?

Hivi kwa nini Wamoravian wote; walalamikaji na walalamikiwa, wasilionee huruma Kanisa wakatii ukweli, kwa manufaa ya Kanisa na Ukristo kwa jumla?

Labda kabla hatujaenda mbali, tukumbushane japo kwa ufupi tu, historia ya KMT jimboni, wakati tishio la kuwepo kwa nyufa lilipoanza kujitokeza.

Hii ilikuwa mwaka 1988, ilipojitokeza migogoro kadhaa wakati KMT Jimbo la Kusini likiwa chini ya uongozi wa Mwenyekiti, Mchungaji Musomba na Makamu akiwa Mchungaji Samweli Mwakijambile; Katibu Mkuu, alikuwa Mchungaji Nelsen Mwaisango.

Ni dhahiri kuwa migogoro hiyo ilitokana na tuhuma za matumizi mabaya ya pato la ofisi miongoni mwa viongozi.

Ni wazi kuwa hali hiyo, ilifanya kuwepo picha fulani ya kuwindana miongoni mwa viongozi ingawa hali hiyo haikuwekwa wazi na wahusika ambao wote ni wana Kamati ya Utendaji. Sakata moja wapo lilikuwa la mashine ya mbao, ambayo ilitoweka katika mazingira ya utata.

Sakata hilo, lilikuwa limemkalia vibaya Mwenyekiti. Kutokana na hali hiyo, ikabidi aliyekuwa Makamu, akalie kiti hicho katika kulishughulikia suala hilo.

Hata hivyo, ilitia faraja kwani baada ya mazungumzo ya busara kutumika, msamaha ndio ulioafikiwa na kuacha mambo yalivyo. Hii ilipangwa kuwa siri ingawa baadaye haikuwa siri tena.

Ukapita muda, janga la kutoeleweka vizuri katika mapato na matumizi ya pesa, likamgeukia Makamu. Safari hii aliyekalia kiti katika kushughulikia suala hilo, akawa Mwenyekiti wa Jimbo.

Katika kuyamaliza hayo, Makamu akakubali kubeba msalaba huo, Mwenyekiti hakukubaliana.

Kutokana na ama ujanja wa bahati mbaya au wa makusudi, suala la Makamu Mwenyekiti likawekwa wazi kuwa anatuhumiwa kwa ubadhilifu wa shilingi laki moja na nusu (150,000/=). Hali hii ikazua uelewano dhaifu katika Kanisa. Na hali ilikuwa ya kutisha.

Katika suala hili, kulikuwa na mgawanyiko. Wapo waliosema Makamu Mwenyekiti huyo alipe pesa hiyo ili aendelee na kazi, wapo waliosema aondoke kabisa. Pia, hawakukosekana waliotaka viongozi hao wote; Mwenyekiti na Makamu wake, waondoke katika nyadhifa zao.

Ikumbukwe kuwa ipo dhana ambayo kwa mtazamo wangu binafsi, ninaiona si nzuri ndani ya Kanisa na ni sumu katika umoja wa Kristo.

Hii ni dhana ya mapokeo kwamba, kati ya Mwenyekiti wa Jimbo, Makamu, na Katibu Mkuu, mmoja akitoka Kyela, Mwingine atoke Ileje na mwingine atoke Tukuyu.

Kwa mantiki hiyo, Mchungaji Musomba (Mwenyekiti), alikuwa mwakilishi wa Wandali (Ileje), Mchungaji Mwakijambile (Makamu), aliwakilisha Wanyakyusa wa Kyela; wakati Mchungaji Mwaisango (Katibu Mkuu), aliwakilisha Wanyakyusa wa Tukuyu.

Mimi ninadhani dhana na mapokeo ya uwakilishi wa namna hiyo si nzuri kwani ina hatari ya kumuweka kiongozi asiye na uwezo na kuwaacha wenye uwezo wa kuongoza katika nafasi husika, ili mradi tu, kuna mbegu hiyo mbaya ya ukabila.

 Wamoravin wanapaswa kujua kuwa Yesu anahimiza umoja katika Kanisa sio ukabila katika Kanisa.

Ieleweke kuwa Jimbo la Kusini, linazo wilaya nne (kwa mujibu wa KMT). Hizo ni Wilaya ya Kusini (Kyela), Wilaya ya Magharibi (Tukuyu), Wilaya ya Kati (Ileje) na Wilaya ya Mashariki (Dar es Salaam, Morogoro na Pwani).

Pia, dhana ya uwakilishi wa namna hii ni hatari kwa sababu, ipo hatari upande mmoja ukamfanya mtu mmoja ajione kama mungu-mtu ndani ya Kanisa na hata kuamini kuwa hakuna mwingine kama yeye.

Ninasema hali hiyo inadumaza Kanisa kimanedeleo kwani licha ya kumfanya mtu ajisahau, alale usingizi, pia haitoi mwanya wa kutosha kwa waamini wengine kutumia vipawa vyao kulitumikia Kanisa la Mungu.

Ni vema jamii ya Wamoravian wa Jimbo la Kusini, itambue kuwa, katika milenia hii ya tatu, miongoni mwa mambo yanayoweza kuhatarisha umoja, mshikamo na udugu katika Kanisa, ni upatikanaji wa viongozi kwa vigezo vya umaarufu wa kabila au ukoo.

Hivi umaarufu wa ukoo na mambo ya Mungu, wapi na wapi?

Sasa, itasikitisha zaidi kama waamini wa Moravian Jimbo la Kusini, wataendelea kuruhusu kuwapo tena kwa migogoro ndani ya Kanisa lao na wakasahau kuwa Mungu alisimama pamoja na Kanisa hadi likafika lilipo.

Inasikitisha kuwa licha ya neema hizo za Mungu, joto na fukuto la chuki, ukabila na mgawanyo linaanza kulinyemelea Kanisa huku waamini wapo; tena pengine wanashiriki kwa kuwa chanzo kwa namna moja ama nyingine; aibu.

Hivi Wamoravian kwa ujumla wenu,  mnalitakia nini Kanisa lenu; kwanini msilionee huruma na kulinusuru lisianguke kwenye janga la migogoro?

Hata hivyo, namna nzuri ya kulinusuru Kanisa, ni kuona kuwa, waamini wanakuwa wakweli. Penye kustahili pongezi, wampongeze Mwenyekiti (Mchungaji Musomba) kwani ni ukweli ulio wazi kuwa licha ya kumtuhumu kwa hili na lile, yapo mengi mazuri aliyayofanya ndani ya Kanisa. 

Uamuzi wa busara na unaojenga heshima ya kiongozi husika, na Kanisa kwa jumla.

Umefika wakati sasa, chuki zisizo na maana, zikaepukwa na kila mmoja hasa viongozi wawe mfano bora wa kuonesha na kulinda heshima ya Kanisa, kila mmoja ajue kuwa ukabila, ni sumu ndani ya Kanisa, ubinafsi, kwa kila mmoja awe muumini au kiongozi ni hatari.

Hata zama za kupuuza suala la watumishi wa Mungu kujiendeleza na hatimaye kuonekana kama anasa, zimepitwa na wakati.

Anayeona hakubaliki ndani ya Kanisa kiuongozi, aache wengine wajaribu kulisukuma gurudumu la maendeleo ya jamii kiroho na kimwili.

Pia, ni vema msamaha wa kweli utawale na aina yoyote ya ubaguzi iondolewe.

Kila mmoja ajue kuwa hatima ya Kanisa la leo na la kesho, ipo mikononi mwa waamini.

Kila mmoja ajue kuwa majungu kamwe hayajengi na ubinafsi unaolenga kujinufaisha au kunufaisha kikundi fulani cha watu kwa kutumia dhamana aliyonayo mtu, iepukwe sasa. Uchaguzi huu utumiwe kulijenga Kanisa sio kuliangamiza.

Wamoravian wajue kuwa, kosa lolote watakalolifanya sasa, linaweza kuwaliza kwa miaka minne ijayo na hata zaidi.

Wachungaji wa zamani nao watambue kuwa, mbele ya Mungu na mbele ya jamii, wanao wajibu mkubwa kutoa ushirikiano wa dhati baina yao na wachungaji vijana wa sasa, wasigeuze Kanisa kuwa uwanja wa ushabiki na upinzani wa kidini, kikabila na kiukoo.

Watoe ushauri kwa viongozi na wachungaji wengine wakilenga kulinufaisha Kanisa sio kumnufaisha wala kumpendeza mtu mmoja mmoja. Wasitoe ushauri wa kuliangamiza Kanisa na kuifanya jamii vikiwamo vizazi vijavyo, viwalilie.

Wamoravian wajue kuwa wametumwa ili wawe watumishi waaminifu shambani mwa Bwana; walihurumie Kanisa.

Sinodi ya Uchaguzi jimboni humo, iwe chachu ya kujenga upendo, ushirikiano na umoja ndani ya Kanisa. Itumike kumpata kiongozi ambaye ataliongoza vizuri Kanisa hata kama alikuwa madarakani katika kipindi kinachoisha.

Wamoravian Jimbo la Kusini hawana budi kujua kuwa kosa watakalolifanya katika Uchaguzi huu, litakuwa gharama ya mahangaiko yao kwa miaka minne ijayo.

CHAGUENI VIONGOZI WATAKAOLISAIDIA KANISA NA UKRISTO KWA JUMLA NA WENYE DHANA YA MAENDELEO.

Fanyeni hivyo mkijua kuwa mkikosea katika Sinodi hii ya Uchaguzi, msimlaumu mtu; mjilaumu wenyewe.

 

Kama hujijui, basi wewe na mwenzio mko hivi:

lWote hakuna hata mmoja aliyekamilika

Na Joseph Sabinus

 

MIGONGANO baina ya watu hutokea kwa kuwa tu, kila mmoja hataki kukubali kuwa yeye ni tofauti na kila mtu, kwa sura, jina, tabia, malezi, mzingira ya kuzaliwa na kukulia namna ya kupokea na kukabili taarifa na hata kuichambua.

Hivyo, marekebisho na uvumilivu mwingi huhitajika katika jamii kwani tofauti hizo husababisha migongano na kutoelewana hasa katika sehemu za kazi na makazini.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa, kadiri watu wanavyotofautiana kitabia, ndivyo kunavyokuwa na uwezekano mkubwa wa kupata migongano.

Ni muhimu kila mtu akatambua na kukubali kuwa namna alivyo ni tofauti kabisa na alivyo rafiki, mkewe au mmewe, wazazi na watu wengine kwani hata mapacha wanataofautiana kwa hili ama lile mradi tu, hawafanani kwa kila kitu.

Ni wazi kuwa ili kuishi na kushirikiana vema katika jamii  ya watu wanaokuzunguka, ni muhimu kwanza kabisa, kujua tabia yako mwenyewe ili uweze pia kujua namna ya kuwaongoza na kushirikiana na wengine katika jambo lolote hata kama wana tabia tofauti na yako.

Ujuzi wa tabia yako na za wengine utakupa wigo mpana wa kushughulikia jambo au kushirikiana na watu wengine wenye tabia tofauti kwa ufanisi na kwa amani.

Maarifa haya, yatakuwezesha hata kuchagua rafiki, mume au mke mshauri mzuri katika masuala ya kimaisha au kikazi ambaye tabia  yake na yako zinashabihiana au zinaweza kujirekebisha na kufanana kwa urahisi.

Marekebisho haya yatafanya pia watu  hao waepuke kufarakana kwa kuwa watafanya marekebisho yanayohitajika. Wakifahamu tofauti hizo, wanaweza kuishi ama kufanya kazi kwa amani zaidi.

Maarifa ya tabia za watu  mbalimbali ni muhimu katika uchaguzi wa kazi fulani zinazohitaji watu fulani. Kwa viongozi ni muhimu kujua tabia za unaowaongoza ili kujua namna ya kuwapangia kazi za kudumu kutokana na tabia zao.

Kwa mfano, mtu asiye na mpangilio mzuri wa mambo ni vugumu kufanya kazi za uhazili au uhasibu au  hata kuongoza vyombo kama treni au ndege.

Mtu ambaye ni mwepesi wa kuogopa hatari anaweza asifae kabisa kazi za uokoaji, upelelezi, uandishi wa habari, urubani au hata kuongoza jeshi katika vita.

Kadhalika, mtu asiyependa kutabasamu hafai kabisa katika kazi kama uuguzi, kuuza pombe au eneo la mapokezi ya watu.

Pia, mtu asiyependa kuzungumza mbele za watu anaweza asifae kabisa katika kazi za uhakimu, uhubiri, upelelezi na uendesha mashtaka.

Ni muhimu kujua watu hao kwa kuwa baadhi  hupenda kutumia nguvu na madaraka na wengine hushawishi wanapohitaji kitu au jambo fulani.

Wengine ni wasemaji sana na wengine ni wakimya. Pia, wengine ni wachoyo, wakatili, wenye wivu na wenye roho mbaya; wasiopenda kuona wenzao hasa wadogo wakinyanyuka na kupata unafuu katika hali fulani.

Ni dhahiri kuwa ni watu wachache wenye moyo wa huruma na wapenda haki wenye utu na wengine ni wale wenye msimamo sana, sio waoga, hawajikombi na hao, hawahitaji kumpendelea mkubwa hasa kwa mambo yaliyo nje ya sheria.

Watu wengine hupendelea kuuliza maswali mengi kabla  ya kufanya jambo na wengine hukubali kwa urahisi bila hata kuuliza swali. Hao ni rahisi kubadili msimamo.

Wengine mambo na sauti zao ni polepole wakati mwingine ni wepesi wa kutenda mambo bila hata uvumilivu wala uchunguzi na tafakari ya kutosha.

Tofauti hizo za watu zinatokana na tofauti za tabia zao.

Mtaalamu mmoja wa Kigiriki  wa tabia za watu Bw. Hipprocratus katika kitabu chake cha Hippocratus, alitenganisha na kujaribu kuzipanga tabia za binadamu katika makundi manne  yaani, “choleric” kama mtu mwepesi wa hasira; wakati “sunguine” alielezwa kama mtu mwenye furaha kwa wakati mwingi, mwenye kutumaini na kutazamia wema tu.

Anapenda watu na ni mwenye bidii.

Mtaalamu huyo alimtaja ‘Philegmatic’ kama mtu mtulivu, thabiti na asiyeshtuka na mwisho akamuelezea ‘Melancholy’ kuwa ni mtu ambaye ana tabia  ya kuhuzunika,  uchungu, mwepesi wa kukata tamaa na mzito wa kufanya jambo.

Mtaalamu mwingine wa Kiingereza yeye aliziweka tabia za watu katika makundi kama hao ila kwa majina tofauti. ‘Dominance’ alitajwa kama mtu mwenye tabia ya kupenda kutawala wengine na kutumia nguvu huyo alifananishwa na ‘Choleric’ kama alivyotajwa na mtaalamu wa tabia za watu wa Kigiriki.

‘Influencing’ yeye alitajwa kuwa ni yule mtu mwenye tabia ya kupenda kuongoza wengine huku akiwashawishi kwa kutumia mvuto wake.

Ni mtu mwenye furaha mara kwa mara na hupenda watu. Huyo ni sawa na ‘Sunguine’.

‘Compliance’ huyu ni mtu mwenye tabia ya kupenda kukubali kufuata, kutii na kuridhika. Anapenda kuwaacha wengine wafanye wanavyopenda ana tabia ya kuogopa kuingia kwenye migongano na hivyo, huogopa asikatae jambo analoambiwa ; ni sawa na ‘Melancholy’.

‘Steadness’ ambaye alifananishwa na  ‘Philegmatic’ yeye ni mtu mwenye tabia ya uthibiti, uadilifu, uaminifu na utaratibu. Ni mwenye tabia ya kupenda mambo yaende sawa ingawa kwa kawaida huwa hapendi kuongoza.

Ufafanuzi zaidi wa kila kundi la tabia za binadamu.

 Choleric au Dominance’ huyo ni mtawala jasiri. Anapenda kuongoza na kushawishi wengine ili kufanya malengo yaliyopo yatimie.

Msigeuze mabinti zenu kuwa mitaji- Askofu Balina

Na Charles Hilila, ShinyangaASKOFU wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Mhashamu Aloysius Balina, amekemea tabia ya baadhi ya wazazi  kuwatumia watoto wa kike kama mitaji yao huku wakiwanyima elimu ambayo ni paji la Roho Mtakatifu.

Mhashamu Balina alisema katika Ibada ya Sakramenti ya Kipaimara katika Parokia ya Bugisi jimboni kwake hivi karibuni kuwa, uduni wa elimu hususan kwa watoto wa kike mkoani Shinyanga, kwa kiasi kikubwa unatokana na wazazi kutowajibika vema kwa watoto hao kama wazazi wanavyowajibika kwa watoto wa kiume.

“Wazazi wengi wanawaonea sana watoto wa kike. Badala ya kuwasaidia na kuwaendeleza kama wanavyofanya kwa watoto wa kiume, wanawatumia kama mitaji na vitega uchumi vya familia. Tabia hii si nzuri kabisa,” alisema.

Alisema tamaa ya kupata mali ikiwa ni pamoja na ng’ombe,  imewafanya baadhi ya wazazi kuwaoza watoto wao wakingali wadogo  na hata kuwaachisha wengine masomo.

Alisema tamaa ya kupata mali na ng’ombe nyingi, haina manufaa zaidi ukilinganisha na elimu kwa mtoto ambayo ni mchango na nguzo kubwa katika kuboresha maisha ya mtu.

Mhashamu Balina aliwahimiza wazazi katika Parokia ya Bugisi, kuitumia shule ya sekondari iliyojengwa katika Parokia hiyo, badala ya kuiacha nafasi hiyo kutumiwa na wengine wanaotoka nje ya mkoa huo.

“Unaona sasa, Jimbo limejenga sekondari hapa, lakini ni watoto wangapi wanaosoma pale wanatoka katika Parokia hii…Kwani wazazi wa hapa hamzai; mbona hakuna watoto wenu hapa?” Alihoji.

Ili kuimarisha elimu Jimboni hapa na kupambana na ujinga, Jimbo limeweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuweka mpango wa Askofu Balina kuzungumza na wazazi wa watoto katika Parokia zote za Jimbo na kuwaeleza haki ya mtoto kupata  elimu bora katika mazingira bora, pamoja na manufaa ya elimu na madhara ya ujinga.

Katika Misa hiyo, Askofu Balina alitoa Sakramenti ya Kipaimara kwa waamini 195 wa Parokia ya Bugisi. Ilihudhuriwa na mamia ya waamini.

Askofu Ngalalekumtwa ataka waamini wasiwe bubu, vipofu kukemea uovu

 

Na Getrude Madembwe, Iringa

ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Iringa, Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa, ameitaka jamii kuepuka tabia ya kufanya maigizo kuwa wao ni viziwi na mabubu, na hivyo hawaoni maovu yanayotendeka na kuwataka wayakemee.

Aliyasema hayo katikati ya juma lililopita wakati akihubiri katika sherehe za Wanashirika wa Shirika la Teresia wa Mtoto Yesu zilizofanyika katika Parokia ya Tosamaganga na kuhudhuriwa na mapadre na masista wa mashirika mbalimbali, watawa wakiume na wakike pamoja na walei kutoka katika parokia mbalimbali jimboni humo.

Oktoba Mosi, kila mwaka, huwa ni maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu ambaye ni Somo wa Shirika hilo.

Alisema watu wengi wakiwamo waamini, wamekuwa na tabia isiyo nzuri ya kuona maovu yakitendeka katika jamii, lakini wanayafumbua macho kwa kujifanya vipofu ama viziwi wasioyaona au kuyasikia.

 “Ni heri mtu kipofu wa kweli asiyeona au kiziwi wa kweli kweli kwa kuwa yeye hasikii, kuliko anayejifanya kipofu au kiziwi ili asikemee mambo yanayokwenda kinyume na mapenzi ya Mungu,” alisema Mhashamu Ngalalekumtwa.

Akaongeza, “Mwenye macho haambiwi tazama; sasa kwanini wewe ujifanye kuwa huoni mpaka uambiwe kuwa tazama?”

Mhashamu Ngalalekumtwa alisema kuwa, katika mazingira hayo ya kiburi cha kujua na kufumbia makosa, wanadamu wanahitaji msaada wa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu ili wapate kuponywa na kwamba, wanaagizwa kuboresha maisha yao ili wafanywe kweli watoto wa Mungu.

Wanashirika hao pia wametakiwa kuwa na kiu na njaa ya kutimiza matakwa ya Mungu ambayo ni kuwa na moyo wa huruma, sera, katiba, kanuni inayohitaji kutumika kwa wanashirika.

Maendeleo sahihi yajali watu sio vitu- Sumaye

Na Eric Samba

MAENDELEO ya kweli na endelevu, ni lazima yawe maendeleo ya wanadamu badala ya vitu, amesema Waziri Mkuu, Fredrick Sumaye.

Sumaye aliyasema hayo juma lililopita katika hafla ya kuchangia Mfuko wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC), iliyofanyika katika ukumbi wa AMECEA uliopo Kurasini jijini Dar es Salaam.

Alisema maendeleo ya kweli na halisi ni mchakato wa kudumu usio kuwa na mwisho.

“Maendeleo ni ya kudumu hakuna hatua inayoweza kufikiwa na kusema kuwa sasa tunapumzika. Hata zile nchi tunazosema zimeendelea, bado hazijapumzika kutafuta maendeleo zaidi,” alisema.

Aliongeza, “Ili kufikia kiwango cha nchi zilizoendelea, lazima kuwekeza zaidi katika huduma za jamii, hasa elimu na afya.”

Alisema kwa kutambua hilo, Serikali inahamasisha wadau wote wa maendeleo ili waelewe na kushiriki katika kuboeresha juhudi za kuelekea maendeleo endelevu na sahihi.

Alisema Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025, ni mkakati wa makusudi unaolenga kupunguza umaskini kufikia 2010 na kuuondoa kabisa hadi mwaka 2025

Aidha, aliwataka Watanzania kujitahidi kusimamia maendeleo yao ili wafike huko wanapoelekea, vinginevyo wataachwa kando.

Alisema itakuwa ni kosa kubwa kwa Watanzania wakifikiri kwamba huko nje kuna waamini na watu fulani wanaosubiri kuwapa misaada yote wanayohitaji.

Waziri Mkuu alisema, njia nzuri ya kujitegemea ni kufanya kazi kwa bidii na ubora unaotakiwa. Alisema mbaya zaidi ni kwamba, Watanzania wengi hawafanyi kazi kwa bidii, ubora na kujituma.

Aliwashukuru Maaskofu kwa kukutana na viongozi wa serikali za Mitaa katika kanda mbalimbali ili kujadili maendeleo bila kujali tofauti zao.

Awali akimkaribisha Waziri Mkuu, Makamu Rais wa Tume hiyo ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severine NiweMugizi, alisema Tume hiyo iliundwa miaka kumi iliyopita ikiwa na malengo kadhaa ambayo ni pamoja na kuchangia maendeleo ya wanadamu kimwili na kiroho pamoja na kupanua na kuboresha huduma za elimu na afya kupitia miradi mbalimbali.

Alisema Tume yake imeamua kuandaa hafla ya kuchangia kutokana na wafadhili kupunguza misaada yake kwa taasisi za tume hiyo kwa asilimia 20, ambapo bajeti ya Tume hiyo ilikuwa ikitegemea wafadhili kwa alisimia 100.

Alisisitiza kuwa, ili kuziba pengo hilo, Tume inawajibika kutafuta kiasi cha shilingi milioni 110 kupitia hatua mbalimbali.

Aidha, alisema kuwa ni muhimu kuchangia huduma hizo kwani wapo Watanzania wengi wanaotegemea huduma za hospitali na shule zilizo chini ya uratibu wa Tume hiyo.

Alisema hadi sasa, Tume inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na kuendeleza huduma za jamii katika hospitali, kuinua kiwango cha elimu ambacho kimeporomoka, kuongezeka kwa yatima kutokana na ugonjwa hatari wa UKIMWI na kuongezeka kwa umaskini.

Alisema Tume hiyo inayoundwa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), inahudumia asasi za afya zipatazo 712 ambapo kati ya hizo kuna hospitali 81, vituo vya afya 631, hospitali teule za wilaya 18 na hospitali za rufaa mbili.

Aidha, Mhashamu NiweMugizi alisema kuwa asasi za afya za makanisa zinavyo vitanda 12021 sawa na asilimia 40.5.

Kuhusu elimu, Mhashamu NiweMugizi alisema kuwa chini ya Tume hiyo, zipo asasi 402 ambapo kati ya hizo, shule za msingi ni 40, shule za sekondari 200, vyuo vya ufundi 54, vyuo vya elimu sita na vyuo vikuu viwili.

Zaidi ya shilingi milioni 29 zilipatikana katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, serikali na wafanyabishara ambapo Waziri Mkuu Sumaye alichangia shilingi milioni moja.

 

 

 It is prepared by Miss. Christina Nyambo. Authorised and run by Rev. Fr. Revocatus Makonge, Exec. Sec. of the Communications Department of TEC.

 

Please visit the TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE WEB SITE