Michezo

Nikipata maslahi mazuri, najiunga na Yanga

Na Gerald Kamia

BEKI wa kutumainiwa wa timu ya Prisons ya Mbeya, ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa Stars, Gerald Hillu, amesema yuko tayari kuacha kazi na kujiunga na timu ya Yanga ambayo inamhitaji iwapo itampatia maslahi mazuri.

Akiongea na Mwandishi wa habari hizi mara baada ya mchezo kati ya timu ya Prisons na Moro United kumalizika kweye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro,

Hillu alisema ni kweli amefanya mazungumzo na viongozi wa Yanga ya kumtaka ajiunge na timu hiyo tayari kwa ajili ya msimu ujao.

Alisema kuwa anachosubiri sasa, ni kutekelezwa kwa baadhi ya mambo ambayo waliyokubaliana ili kusukuma ndiga katika klabu hiyo yenye maskani yake mtaa wa Jangwani jijini Dar-Es-Salaam.

Aliendelea kusema kuwa, soka ya Tanzania inategemea maslahi na kwamba endapo yeye atapewa maslahi mazuri, hana pingamizi lolote kumfanya asiichezee timu hiyo.

"Tunachoangalia ni maslahi ya kutuwezesha kuyamudu maisha haya kwani mpira ndio kazi yetu kwa hiyo, nikipata sehemu yenye maslahi mazuri zaidi ya hapa nilipo, sina kinyongo chochote ninajiunga na timu hiyo," alisema Hiluu.

Kauli ya mchezaji huyo inafuatia kauli ya hivi karibuni ya Mwenyekiti wa klabu hiyo Tarimba Abasi, kusema kuwa, sasa timu yake inahitaji mabeki namba 3 na namba 2 aliowataja kutaka kuwawania kuwa ni Gerald Hiluu na Jumanne Sabura, wote kutoka klabu ya soka ya Prisons.

Wakati huo huo: KIUNGO tegemeo wa timu ya Simba na Taifa Stars Willcef Cetto amesema kuwa kilichomtoa katika Klabu ya Simba na hatimaye kutua Mtibwa, ni migogoro isiyoisha ndani ya klabu hiyo pamoja na ukata wa fedha.

Alisema mjini hapa kuwa, hali ya migogoro inayoikumba klabu hiyo ndio hasa chanzo cha wachezaji kuihama klabu hiyo kwa kuwa viongozi wanakuwa hawawajibiki kuangalia matatizo ya wachezaji na badala yake, wanaipa kipaumbele migogoro.

‘Ningependa wanasimba wanielewe kuwa mimi bado naipenda Simba ila kutokana na migogoro na maslahi duni tunayopewa wachezaji kwa kweli nimeshindwa kuendelea kuichezea timu hiyo kwani mpira ndio kazi yangu na maisha yangu yanategemea mpira," alisema.

Kauli ya mchezaji huyo inafuatia habari kuwa klabu ya Mtibwa imeshakamilisha taratibu zote za usajili wa mchezaji huyo kutoka timu ya Simba ya jijini.

Wapenzi wa Michezo wapendekeza TOC ivunjwe

Na Modest Msangi

WAPENZI wa michezo nchini wameitaka FAT kutumia wembe ilioinyolea BMT kuinyolea TOC kwa kuwa ni miongo miwili sasa TOC inavurunda.

Wakizungumza na KIONGOZI kwa nyakati tofauti, baadhi ya wanamichezo haonchini, walidai kamati ya Michezo ya Olimpiki Tanzania(TOC), inayoongozwa na Mwenyekiti Raphel Kubaga na Katibu wake Erasto Zambi, imekuwa madarakani kwa kipindi cha takribani miaka 20, lakini hakuna mafanikio yoyote ambayo TOC imekwisha yaonesha.

Walisema njia pekee ya kutokujiendekesha kwa hasara kimichezo, ni kuivunja TOC

Kwani muda huo ni mrefu sana kwa kutokuonesha matunda huku serikali ikiwa kimya.

Bondia wa zamani wa ngumi za ridhaa, Fikiri Kilingo alisem, "Viongozi hao wa TOC wamekuwa madarakani kwa muda mrefu lakini hakuna jipya walilofanya. Sasa kuna haja gani TOC kuendelea kuwapo."

Alisema kutokana wizara kuwateua viongozi wa kamati hiyo, kumesababisha viongozi hao kujiwekea mizizi ambayo kuing’oa imekuwa vigumu kama dondandugu lisilo sikia dawa.

Mchezaji wa zamani wa timu ya Majimanji ya Songea, Ibrahimu Buzi alisema kwamba serikali ivunje kamati hiyo na kuunda kamati mpya,

BAADA YA KUBORONGA, SHUNGU SASA AWALAUMU WACHEZAJI NA KUSEMA

Hawazingatii kujituma, ndio maana wanashindwa

Na Gerald Kamia

BAADA ya Timu yake kuboronga mechi mbili mfululizo kwa kulazimishwa kutoka sare na timu za Kajumulo na Mtibwa, Kocha Mkuu wa timu ya Yanga Roul Shungu, amesema kuwa uzembe wa wachezaji wa timu hiyo ndio chanzo cha timu hiyo kushindwa kufanya vizuri.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi wiki iliyopita yalipo Makao Makuu ya Klabu hiyo mtaa wa Jangwani, kocha huyo amesema kuwa wachezaji wa timu hiyo hawazingatii wanachofundishwa na ndio maana wanashindwa kujituma wawapo uwanjani.

Shungu ameendelea kusema kuwa kutoa suluhu kwa timu yake sio kufanya vibaya kwani mpaka sasa ndiyo timu pekee katika ligi hiyo ambayo haijafungwa kwa hiyo amewataka wanayanga kuwa na subira kwani timu yao itafanya vizuri na hatimaye kutwaa ubingwa huo wa Muungano.

Kauli ya kocha huyo inafuatia kauli ya hivi karibuni ya wanachama na mashabiki wa timu hiyo ya kudai kuwa kiwango cha kocha huyo kuendelea kuifundisha klabu hiyo kimeishia ukingoni kutokana na timu hiyo kushindwa kufanya vizuri.