Michezo

Super ligi yaanza na balaa

Na Mwandishi Wetu

LIGI kuu ya timu nane bora, leo inaanza kwenye viwanja mbalimbali nchini, huku ikiwa imegubikwa na matatizo chungu nzima.

Kwa mujibu wa ratiba ya FAT iliyotolewa hivi karibuni, ligi hiyo wakati Yanga ya jijini itakuwa na kazi ngumu ya kuumana na Kajumulo World Soccer huku ikiwa haina viongozi wa kueleweka.

Prisons ambao ni mabingwa watetezi, wamekuwa na upinzani na Mtibwa ya Morogoro katika siku za hivi karibuni, hali iliyoifanya mechi hiyo kuonekana kuwa kali.

Lakini, wakati timu nyingine zikijipinda kuwania Kombe la Muungano, pamoja na uwakilishi katika vikombe vya kimataifa, timu kongwe ya Yanga inahangaika kortini ambapo viongozi wake wanang’ang’ania madaraka na kuitelekeza timu.

Viongozi wa muda wa klabu ya Yanga, chini ya akina Abass Tarimba, na wenzake nao hauna nguvu tena kwa kuwa tayari umepokonywa mamlaka na mahakama ambayo imewarejesha madarakani viongozi waliochaguliwa.

Hata hivyo, kocha wa timu hiyo, Roul Shungu, toka Jamhuri ya Kongo, ameahidi kuiingiza timu kupambana na timu ya Kajumulo.

Timu hizo zilitoka sare katika mechi zote mbili za mzunguko wa makundi.

Keegan aonja joto ya Euro 2000

lUingereza hatarini kufungasha virago

Brussels, Ubelgiji,

KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya Uingereza Kevin Keegan ,ameanza kuonja chungu ya jiwe ya washabiki wenye fujo wa London,baada ya timu yake kufungwa na Ureno kwenye raundi ya kwanza ya michuano ya Ulaya.

Akihojiwa na Televisheni ya ITV ya Uingereza Keegan alisema mara baada ya mpambano huo uliokuwa mkali,mashabiki wa London walimrushia matusi ya nguoni ambayo hata kuyatamka hadharani hayafai.

"Nilijisikia vibaya sana na kujiuliza je kama angekuwepo mwanangu karibu ningejisikiaje?"alihoji kocha huyo mcheshi na mwenye kupenda kuongea na Waandishi wa habari.

Katika kisanga hicho mashabiki wenye sifa mbaya ,mchezaji kiungo watimu hiyo David Beckam ambaye alishindwa kuvumilia na akawajibu mashabiki hao kwa kuwaonyesha alama ya matusi kwakidole chake cha mkono wa kushoto.

Magazeti ya Ulaya yalinasa picha ya kitendo hicho cha Beckam lakini tayari Shirikisho la soka la Ulaya limeishatoa msimamo wake kuwa halitampa adhabu yoyote mchezaji huyo ambaye anashika nafasi ya pili kwa uchezaji bora Duniani.

Nacho cha Soka cha Uingereza kimeeleza masikitiko yake kuhusu tukio hilo na kudai kuwa mashabiki hao walikuwa wamelewa sana.

Aidha kiliahidi kuwasiliana na kamati ya maandalizi ya mechi hiyo ili ulinzi uongezwe katika pambano la tatu Leo litakalofanyika leo kati ya England na Ujerumani.

Kama England itafungwa pambano la leo basi itakuwa imekata tiketi yake ya kurudi kwao na kiziachia Ujeruama na Ureno kuingia robo fainali.

"Veterani"wa Yanga afariki

Na Leocardia Moswery

MCHEZAJI wa zamani wa Timu ya Yanga ya Jijini,Charles Mwanga (47) amefariki dunia juzi katika Hospitali ya Hindu Mandari alipokuwa amelazwa kwa matibabu.

Ndugu wa karibu wa marehemu Mwanga,Rashid Azuhuni ameliambia gazeti hili jana kuwa marehemu alikuwa akisumbuliwa na ini na figo ugonjwa ambao ulikuwa ukimsumbua kwa muda mrefu na alizikwa nyumbani kwao Ugweno Wilayani Mwanga katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Azuhuni ambaye alikuwa akizungumza na Mwandishi wa habari hizi nyumbani kwa marehemu huko Kigogo Jijini,alisema kabla mauti hayajamfikia mwanamichezo huyo,alikaa hospitali muda wa wili moja.

Akielezea undani wa mwanamichezo huyo ambaye alikuwa akicheza nafasi ya beki namba mbili kwenye miaka ya 1980,Ahuzuni alisema kuwa ameacha mke na watoto kadhaa ambao hata hivyo hakuweza kutaja idadi yake.

Marehemu huyo alijiunga na timu ya Yanga mnamo mwaka 1974 ambapo alichezea timu hiyo kwa kipindi cha miaka sita na baada ya hapo alijiunga na timu ya Mwadui Mkoani Shinyanga.

Hadi mauti yanamchukua Mwanasoka huyo alikuwa ni Mwajiriwa wa Kampuni ya Wakala wa Meli nchini (NASACO).