Makanisani Wiki hii

Rais wa Chuo Kikuu akemea uchoyo, uroho

Na Leocardia Moswery

MAKAMU wa Rais wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostine cha mjini Mwanza (SAUT), Padre Deogratias Rweyongeza, amekemea tabia ya choyo na uroho wa kuhodhi mali huku wengine wakiihitaji inayoibuka kwa walei na watumishi mbalimbali wa Mungu.

Aliyasema hayo wakati akizungumza katika mahubiri katika Kanisa la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumapili iliyopita.

Padre Rweyongeza alisema kuwa tabia ya uroho na kutaka kujilimbikizia mali, imewasababisha hata wanaume wengi kuzitelekeza familia zao wakiziacha zinalala njaa.

"Hebu tafakari neno CHOYO. Huoni kuwa linasababisha hata familia kutoelewana kutokana na neno hilo kuwa sambamba na UROHO?" alihoji Padre Rweyongeza.

Aliongeza kuwa hata akina mama wengi wametawaliwa na hali ya uroho kutaka vitu vingi vinavyowafanyia usumbufu na familia zao mpaka wavipate na kwamba wanapovipata hata kama ni kwa wingi, hawatakikuwasaidia wengine wanaohitaji pia.

"Eti hata akina baba wanakubali kuwaacha watoto na familia zao wakilala njaa, eti hawatakikutoa. Hii yote inatokana na uroho na uchoyo," alisema na kuonya kuwa tabia hiyo ya uchoyo inayoibuka hata kwa watumishi mbalimbali wa Mungu, haina budi kuepukwa ili jamii ifike katika ufalme wa Mungu.

Hata hivyo alisema kuwa moyo wa kutoa siyo tu kuwa unapaswa kuwa kwa watu matajiri peke yao, bali hata maskini na watu wasio na kipato kikubwa wanapaswa kujenga moyo wa kweli wa kutoa kwa wanaohitaji.

Wakati huo huo: Katika ibada hiyo, waamini walimwombea Mungu ampe pumziko la milele, aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Idara ya habari ya baraza la Maaskofu katoliki Tanzania (TEC), Marehemu Padre Norbert Kija, aliyefariki Septemba 19, 2000.

Mshirikiane vema kuwalea watoto

Na Faustin Mkaudo, Arusha

WAZAZI wameshauriwa kudumisha upendo katika ndoa ili kuwalea watoto wao katika maadili mema yanayompendeza Mungu, jamii na taifa kwa jumla.

Hayo yamesemwa na Padre Joseph Babu, alipokuwa akitoa Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 150, kwa niaba ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Mhashamu Josaphat Lebulu.

Katika mahubiri yake katika kanisa la Moyo Safi wa Bikira Maria, parokia ya Unga Ltd, Padre Babu alisema wazazi hawana budi kudumu katika upendo ili ndoa zao zisiingiliwe na maovu ya shetani.

Alisema bila sala ndoa haziwezi kudumu na kwamba ni vema wazazi waweke mbele sala wakimwomba Mungu awazidishie baraka ili kusitokee mifarakano ndani ya ndoa yao.

Alisema bila ushirikiano wa karibu katika kuwalea, watoto watapotea na hatimaye kujiingiza katika vitendo viovu kama vile uvutaji bangi, utumiaji madawa ya kulevya na hata utoaji mimba ambavyo ni machukizo kwa Mungu.

Aidha Padre Babu aliwaasa wazazi ambao hawapendi kushirikiana katika kuwalea watoto wao katika maadili mema waache tabia hiyo ili waweze kukaa pamoja katika jumuiya na kutafakari yale ambayo yanampendeza Mungu, na kuachana na ulevi wa kupindukia ambapo ni kikwazo katika familia.

Padre Babu, aliwaasa waliopokea Sakramenti ya Kipaimara wasiwe na tabia ya kuzurura ovyo pasipo mpangilio na akawashauri kufuata mafundisho mema wanayopata toka kwa wazazi, majirani na wasimamizi wao.

Alidai ili wawe askari wa Yesu, lazima wafuate mafundisho hayo juu ya maisha yao ya kiroho ili wasipotee kimaadili na badala yake wakue katika yale yanayokubalika kijamii.

Alisema familia inayodumu katika sala na ikimuomba Mungu, kamwe shetani hathubutu kuitia vishawishini.

Aliwashukuru waamini wa parokia ya Moyo Safi wa Bikira Maria kwa kujitoa kwa hali na mali katika ujenzi wa nyumba ya Mungu kwa kuwa mfano bora katika jimbo hilo.

'Usimikaji wa Biblia uamshe mioyo, imani kwa Wakristo'

Na Steven Mchongi

‘USIMIKAJI wa Biblia Takatifu utaamsha upya moyo wa imani kwa Wakristo wote katika kuthamini kutekeleza, kulienzi neno la Mungu na kulifanya lienee kote ulimwenguni’.

Hayo yameelezwa hapa jijini Mwanza na Mkurugenzi wa Malezi na Miito kwa Vijana wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Padre Richard Makungu, wakati wa kikao cha Baraza Kuu la Walei.

Padre Makungu alisema kuwa usimikaji wa Biblia Takatifu ni kuleta mwanga na matumaini ya wokovu kwa watu wote waliovunjika moyo.

Alisema kuwa Biblia Takatifu ikizingatiwa, italeta sura mpya ya neema ambapo unyanyasaji na utovu wa maadili utaondolewa.

Amesema kuwa ili kutekeleza hatua hiyo, waamini wote wanapaswa kununua Biblia Takatifu, kuzisoma na kuyaweka mafundisho yake moyoni na kwa matendo kama dira ya maisha safi.

Usimikaji wa Biblia Takatifu kanisani katika jumuiya familia na kwenye vigango vya parokia mbalimbali kwenye jimbo katoliki la Mwanza unafanyika wakati huu wa Rozali Takatifu.

Usimikaji huo wa Biblia takatifu unafanyika kutekeleza agizo la kanisa katoliki jimbo la Mwanza katika mwaka huu mtakatifu wa jubilei kuu ya ukristo duniani.

Padre akemea majivuno katika jamii

Na Getrude Madembwe

MWANGALIZI wa Kituo cha hija kilichopo Pugu jijini Dar-Es-Salaam Padre John Rupia ameitaka jamii kuachana na kasumba ya kuwa na majivuno mbele za watu wengine.

Padre Rupia aliyasema hayo mwanzoni mwa juma wakati wa hija ya parokia ya Segerea iliyokwenda kuhij katika kituo hicho ili kusheherekea Mwaka wa Jubilei Kuu.

Alisema inashangaza na kusikitisha kuona watu wengine wakijivunia vitu fulani au kujiona wao ni bora kuliko wenzao hali aliyosema, haifai mbele za Mungu na jamii nzima.

Padre Rupia aliwanyanyuzia maji ya baraka waamini hao ili wasafishike na kuondokana na matendo maovu yakiwemo ya tamaa za kimwili, na kujilimbikizia mali.

"Nimewanyunyuzia maji ya baraka ili msafishike. Muwe safi na muachane na tabia ya kujivuna na kujilimbikizia mali huku mkitawaliwa na tamaa za mwili. Mrudipo huko majumbani kwenu, msitende dhambi tena," alisema.

Pia aliwataka waamini hao kuungama kila wakati pindi wanapogundua kuwa wamemkosea Mungu ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufika mbinguni na wao wenyewe kusamehana.

"Mkikoseana, msameheane kwani utakuwa unajisumbua kuomba msamaha kwa Mungu wakati wewe hutaki kumsamehe mwenzako."

Naye Paroko Msaidizi wa Parokia ya Segerea Padre George, aliwataka waamini hao kutokuwa na woga wa kufa kwani mtu ukiwa safi utafika mbinguni na huko utakutana uso kwa uso na mwenyezi Mungu."

"Kwa nini unashikwa na woga wakati wa kufa, hautakiwi kuwa na woga kwani mtu kama ulikuwa ukitenda mambo ya kumpendeza Mungu, utaonana naye uso kwa uso," alisema.