Ndoa na familia katika maadhimisho ya Yubilei ya Bwana

KATIKA maadhimisho ya Yuilei kama familia ya Mungu, Kanisa mwaka huu linaendelea na maadhimisho ya kijubilei. Katika programu za makanisa mahalia juu ya jubilei yako mengi yaliyojitokeza kama matatizo ya kichungaji, mfano uibukaji wa kasi wa familia za mzazi mmoja.

Kwa upande mwingine familia nyingi zimepata nafasi ya kutafakari juu ya Sakramenti ya Ndoa, maisha ya ndoa katika familia, wajibu wa wanandoa na jinsi wanandoa wanavyoshiriki utume wa Kanisa kwa kuwa wainjilishaji wa watoto wao na kuchukua jukumu la kujitakatifuza.

Kwetu Afrika ndoa na familia huthaminiwa na ndio maana Sinodi ya Afrika 1994 ilichukua familia kama kigezo kikuu cha Kanisa "Kanisa kama familia ya Mungu".

Katika makala hii, Katibu Mtendaji wa Idara ya Liturujia katika Baraza la Maaskofu katoliki Tanzania (TEC), Padre Julian Kangalawe anaelezea kuelezea mtazamo wa idara hiyo kitaifa juu ya masuala ya ndoa na familia katika maadhimisho ya Jubilei ya Bwana

Kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa, Wakristo waliofunga ndoa hudhihirisha na kushiriki katika fumbo la umoja na upendo uzaao matunda uliopo kati ya Kristo na Kanisa lake.

Kama vile Kristo alivyolipenda Kanisa lake na kujitoa sadaka kwa ajili yake, kwa njia ya ndoa na Roho Mtakatifu anawawezesha Wakristo, wafunga ndoa wakuze upendo wao, wakithamini usawa kati yao na kujitoa kila mmoja kwa mwenzake na kupendana kwa upendo usiogawanyika ambao upendo wake asili yake ni chemichemi ya upendo wa Kimungu.

4. FAMILIA KATIKA MPANGO WA MUNGU

Tuelewe kwamba kwa vyovyote, ndoa huwaingiza wapendanao katika mpango wa Mungu wa Familia. Ni vitu visivyotengana moja haiwezi ikasimama bila nyingine.

Jumuiya ya Watu wa ndoa huanzishwa kwa ukubaliano wa mume na mke.

Ndoa na familia imepangwa na manufaa ya mume na mke na kwa ajili ya uzazi na malezi ya watoto.

Mapendo ya mume na mke na uzazi wa watoto huanzisha kati ya watu wa familia moja uhusiano wa pekee na uwajibikaji wa kwanza.

Mungu kwa kumuumba mwanaume na mwanamke alianzisha familia ya kibinadamu na kuijalia katiba yake ya msingi.

Ndoa ya Kikristu hulenga katika familia ya Kikristu, hufanya ufunuo na udhihirisho maalum wa ushirika wa Kanisa na kwa sababu hiyo, familia ya Kikristo inaweza na inatakiwa kuitwa kanisa la nyumbani.

Hii ni familia ya Imani, matumaini na mapendo. Katika Kanisa ina umuhimu wake wa pekee kama ilivyodhihirishwa katika Agano jipya. Efe. 5:21 -6::4; Kol. 31:18-21; 1Pet 3:1-7

Kwa njia ya sakramenti ya Kikristo familia ni umoja wa watu, ishara na mfano wa umoja wa Baba na Mwana katika Roho Mtakatifu.

Kazi ya familia ya uzazi na malezi ya watoto huinurisha kazi ya Baba ya uumbaji.

Familia kwa namna moja au nyingine, huitwa kushiriki sala na sadaka ya Kristo. Familia ya Kikristo kwa namna hiyo kwa sala zake na uadhimishaji wa Neno la Mungu, ina kazi msingi ya uinjilishaji na umisionari.

Familia ni chembe ya kwanza ya maisha ya jamii.

Ni jumuiya ambamo tangu utoto, mmoja aweza kujifunza tunu za maadili, kuanza kumcha Mungu na mambo mengi.

Hivyo kifamilia tunasema kuwa:-

1. Maisha huanzia katika familia Cfr Humanae Vitae, Familiaris Consortio.

2. Ni Shule ya awali:

wajibu wa mzazi ni muhimu kiafrika tunu zote hupitishwa kwa njia ya familia.

3. Ni nguvu ya awali ya uinjilishaji na Katekesi.

Bila ndoa nzuri, hakuna na hakutakuwa na familia nzuri wala jumuiya ndogondogo zenye familia yenye uimara.

Kwani inakuwa ni familia inayoshiriki maisha na utume wa Kanisa.

Hujiinjilisha na kugeuka kuwa chombo msingi cha uinjilishaji.

4. Ni jumuiya ya maendeleo ya huduma kwa watu.

5. Wajibu wa Kanisa mahalia juu ya Sakramenti ya Ndoa

Kwa vile katika tamaduni mbalimbali za kiafrika, familia ni tunu ya pekee, hupewa kipaumbele. Hivyo, watarajiwa wa ndoa huandaliwa kwa muda mrefu na hata jamii nzima inajihusisha.

Hivyo basi, ndoa kwa Mwafrika sio tendo la siku moja tu.

Wanandoa wanapotangaza na kukubiliwa rasmi na kuwa na sherehe.

Ili dhamiri yetu ya kulielewa Kanisa kama familia ya Mungu ifanikiwe, ni vema kila Kanisa mahalia kichungaji lingekuwa na:

1. utaratibu wa kufafanua maana na hadhi ya Sakramenti ya Ndoa; wajibu na utume wa wanandoa.

Mafundisho yawe ya muda mrefu walau isipungue miezi mitatu. Kama vile tunavyowaandaa kwa Komonyo au Kipaimara, ingefaa kila parokia iwe na timu ya kuandaa wanandoa.

2. Semina za mara kwa mara kwa familia ili zikue na kupata mbinu za kupitisha tunu za sakramenti kwa watoto wao..

STAR LUBRICANTS

Watu wengine tunaweza kuwa na maswali mengi ambayo kwa namna moja au nyingine tunashindwa kupata majibu yake. Hii ni kutokana na ujuzi tofauti tulio nao kuhusu vyombo au matumizi ya oili katika magari yetu. Katika makala hii, mwandishi Ndugu JOsephat Rwezaura wa Star Lubricants Camp (Elf) anakuletea maswali na majibu yanayotoa mwanga kuhusu matumzi ya oili.

1. Utajuaje kuwa oili inatakiwa kubadilishwa.

Sababu zinazoweza kusababisha oili ibadilishwe ni pamoja na:-

Upungufu wa utendaji wa oili ambao unaweza kuangaliwa kwa kutumia majaribio ya karatasi maalum ‘blotting paper’ au kuangalia kama ‘TBN’ bado inatosha (hasa kwa magari ya diesel) au unene wa oili (viscosity) kama unatosha.

Njia nzuri ya kuangalia kama oili bado inafaa au la ni kuipima katika maabara jambo ambalo linaweza kuwa gumu katika maisha ya kawaida hasa katika nchi zinazoendelea.

Kama oili imeongezeka au imepungua sana unene wake basi inatakiwa kubadilishwa.

Kwa kuwa katika maisha ya kila siku mtaani si rahisi kupeleka oili katika maabara mara moja, yafuatayo yanatakiwa kuzingatiwa katika kujua kama oili inatakiwa kubadilishwa.

Oili inakuwa nyeusi, inakuwa na harufu kali (yakuungua) unene wa oili unabadilika (hii inaweza kuangaliwa kwa kuchukua oili na kusugua kwenye kiganja).

Hapo unaweza kuangalia kama oili bado inafaa au la. Hizi zote ni dalili tu za kuangalia kama oili ni nzuri au hapana, kwa uhakika wa kujua kama oili inafaa inatakiwa kufanya uchunguzi katika maabara.Namna nyingine ya kuangalia kama virutubisho vya oili bado vinafanya kazi hasa kwa upande wa oili za magari ya diesel; chukua oili iweke kwenye karatasi ijulikanayo kama ‘blotting paper’.Oili itasambaa na kutengeneza mzunguko. Kama chembe chembe nyeusi zitakaa katikati na oili nyingine kusambaa pembeni basi oili hiyo haina tena nguvu na inatakiwa kubadilishwa. Kama oili na chembe chembe nyeusi vitasambaa pamoja kwenye karatasi basi oili hiyo bado inafaa.

Kwenye maabara unene (viscosity) na TBN vinapokuwa nusu ya viwango vya oili nzima basi oili hiyo haifai tena kwa matumizi.

Kwa uhakika zaidi mwenye gari anatakiwa kufuata mapendekezo ya mtengenezaji wa gari kuhusu matumizi ya oili hasa muda wa kubadilisha.

2. Je kama sampuli ya oili ni nyeusi, oili inatakiwa kubadilishwa haraka?

Kazi mojawapo ya oili ni kusafisha uchafu uliopo kwenye injini. Kama kuna uchafu kwenye mtambo, oili itausafisha na utachanganyika na oili yenyewe.

Kwa jinsi hii, oili inaweza kuonekana nyeusi kutokana na uchafu iliyokuta kwenye injini. Kwa hiyo itakuwa si uamuzi mzuri kusema kuwa oili haifai kwa sababu ni nyeusi.

Oili inaweza kuwa nyeusi kwa kufanya kazi yake vizuri kusafisha injini.

Mambo mawili yanaweza kufanyika kama oili inaonekana ni nyeusi sana. Unaweza kutumia jaribio la karatasi (blotting paper) kama ilivyoelezwa hapo juu , na jambo lingine ni kuangalia unene wa oili.

3. Je, Kama oili ina harufu ya kuungua, ina maana oili hiyo ni mbaya?

Kama oili ina harufu ya kuungua sana, inawezekana oili imechanganyika na mafuta (diesel au petrol).

Oili ikichanganyika na mafuta, unene wake unapungua sana. Angalia unene wa oii kwa kutumia njia zilizoelezwa hapo juu. Kama unene wa Oili umepungua sana kutokana na kuchanganyika na mafuta basi oili hiyo ibadilishwe.

4. Ni faida gani unaweza kupata kwa kutumia oili yenye viwango tofauti (Multigrade oil)?

Kimsingi oili yenye viwango tofauti (multigrade) ni oili iliyobadilishwa unene wake ili kupunguza kima (muda) cha kupungua unene kadiri joto linavyoongezeka. Mfano wa oili yenye viwango tofauti ni kama vile SAE15W40, SAE 20W50, SAE80W90, SAE85W140, n.k. Oili ya aina hii huonekana nyepesi katika joto la kawaida (room temperature) na uongezeka unene wake jinsi joto linavyoongezeka. Kwa hiyo unaweza kupata faida zifuatazo kwa kutumia oili ya aina hii.

Gari linapokuwa limezimwa kwa muda fulani, oili yote huwa haiko chini Gari linapowashwa kuna muda fulani ambapo oili inakuwa bado haijapanda kwenye injini (labda sekunde chache). Oili yenye viwango tofauti kwa kuwa huwa ni nyepesi wakati wa joto la chini, huweza kupanda haraka kwenye injini mara tu gari linapowashwa kuliko oili zenye kiwango kimoja (Monograde) kwa jinsi hii, oili huanza kufanya kazi haraka sana na kupunguza uwezekano wa msuguano ndani ya injini.

Inasemekana kuwa kutumia oili zenye viwango tofauti kunapunguza matumizi ya mafuta kwa 1.5% - 3%na gari linakuwa na nguvu za msukumo zaidi.

Oili zenye viwango tofauti hutoa ulinzi kwa injini wakati wa joto kali kuliko oili zenye kiwango kimoja kwa sababu kima cha ubadilikaji wake (Viscosity Index) na joto ni kidogo.

5. Je ni kweli kwamba oili nyekundu ni bora kuliko oili ya rangi ya kawaida (golden colour)?

Si kweli kwamba Oili nyekundu ni bora kuliko oili ya rangi ya kawaida kwa sababu rangi ya oili haichangii cho chote katika utendaji wa oili, Rangi nyekundu inasababishwa na ‘dye’ inayoongezwa kwenye oili kuweka uwekundu. Sababu za kuweka rangi kwenye oili zimekuwa ni kwa ajili ya kupambanua oili tu.

6. Je, nitajuaje kama kuna maji kwenye oili?

Kwa hali ya kawaida oili yenye maji huonekana kama maziwa au njia nyingine ya kuangalia kama kuna maji ni kwamba, chemsha oili kwa muda fulani kama oili itatokota basi kuna maji kwenye oili hiyo.

7. Je, kama oili inaonekana nyepesi katika joto la kawaida (room temperature) ina maana kuwa haitafanya kazi zake vizuri kwenye injini wakati wa joto kali?

Hapana: kwa sababu Oili inaweza kuwa na viwango tofauti vya unene (Kama ilivyoelezwa hapo juu kwenye jibu la swali la nne) Oili zenye viwango tofauti huwa nyembamba wakati wa joto la kawaida lakini kadri joto linavyoongezeka ndivyo oili inavyotanuka na kuongezeka unene wake. Kwa jinsi hii oili ya aina hii hufanya kazi vizuri sana wakati wa joto kali kama ilivyoelezwa hapo juu.

Vile vile unene staili wa oili kwenye injini husika unatengemeana na mapendekezo ya mtengenezaji sio tu kwa kuangalia kwa macho. Kuna magari hasa ya kisasa yametengenezwa kutumia oili nyepesi. Oili zilizotengenezwa na ‘Synthetic Base oil’ ni nyepesi kwa macho japo ni imara na nzuri sana. Kikubwa ni kufuata ushauri wa mtengenezaji wa mtambo.

8. Je, ni sahihi kuweka Oili kwenye mafuta (diesel au Petrol) kwa injili ambazo ni ‘four stroke’?

Hapana, kwa sababu oili haichomeki haraka kama mafuta. Hii husababisha injini kuwa na uchafu mwingi uanaogandamana chini.

Hii pia husababisha injini kutofanya kazi zake vizuri.

9. Inakuaje Injini inanoki?

Kunoki ni kitendo cha vyuma katika injini kupata joto kali sana na kulika sana mpaka kupandana. Hii inasababisha mzunguko wa injini kusimama kabisa na hivyo tunasema kuwa injini imenoki.

Injini inaweza kunoki inapokuwa na oili ndogo, nyepesi au kutokuwepo kwa oili kabisa katika injini. Hii inaweza kusababishwa na oili kuvuja au kutumika kwa muda mrefu sana kuliko wakati wake. Hali hii husababisha kuwepo na msuguano mkubwa kwenye injini na injini kuwa na joto kali sana ambalo linakuwa halipozwi.

Matokeo yake injini unoki.

unoki kwa injili kunaweza kusababishwa vile vile na oili kuwa nyepesi sana kutokana na kuchanganyika na mafuta.

Wakati mwingine kunoki kwa Injini kunasababishwa na ‘Oil Pump’ kutofanya kazi vizuri (Mechanical Failure).

Uendeshaji mbaya vile vile ni hatari kwa maisha ya gari. Hii ni kama kupakia mzigo mkubwa kuliko uwezo wa gari na hivyo kusababisha gari kupata joto sana na hatimaye kunoki.

10. Ni sababu zipi zinaweza kusababisha kupungua msukumo wa oili kwenye injini?

Katika utendaji wa kawaida wa injini ya gari, oili hufanya pamoja na kazi zingine kazi ya kuziba matundu madogo madogo kwenye injini.

Utendaji mzuri wa oili kusababisha msukumo mzuri katika injini. Kwa hiyo kama msukumo wa oili unaonekana kwenda chini unawezekana kuwa:-

Oili imekuwa nyepesi sana

Oili iliyopo haitoshi.

Unapoangalia ujazo wa oili hakikisha kuwa gari limezimwa kwa muda mrefu kidogo ili oili yote iwe imetulia katika ‘sump’ yake.

11. Nini Kinasababisha oili kupungua haraka kwenye Injini?

Kitu cha kwanza kinachoweza kusababisha oili kupungua haraka kwenye injini ni kuvuja kwenye ‘oil pump, oil filter’ au katika sehemu zingine kwenye mzunguko wake. Kwa hiyo hiki ni kitu cha kwanza kuangalia na kurekebisha kabla ya kuendelea na uchunguzi mwingine.

Katika utendaji wa kawaida wa injini ambazo ni ‘four stroke’ au gari huwa linatumia oili kama mafuta mengine. Piston zinapofanya kazi zake, kuna kiasi cha oili ambacho huwa kinatumika na hivyo kusababisha oili kupungua kwenye injini.

12. Je inatakiwa nibadilishe oili baada ya muda gani?

Kubadilishwa kwa oili kwa kawaida kunategemea umbali au muda wa utendaji kazi wa magari au mtambo. Magari huhesabu kilomita wakati mitambo ya viwandani au mashambani (matrekta) huhesabu masaa ya kazi.

Kubadilishwa kwa oili pia kunategemea na ubora wa oil (Performance level) . oili za ubora wa juu API: SH-SJ kwa petrol au API: CF4 - CG4 kwa Diesel; oili hubadilishwa baada ya kilomita 15,000 mpaka 45,000. Oili za ubora wa chini API : SF au API:CC- CD ni kati ya kilomita 1,000 mpaka 3,000.

Kubadilisha kwa oili vile vile kunategemea mazingira ya utendaji kazi. Mazingira ya vumbi, tope, uchafu kama mashambani, ujenzi wa barabara, uwanja wa vita au barabara zisizo na lami oili zinatumika katika mazingira hayo yanapaswa ibadilishwe muda mfupi. Hii ni tofauti na oili ambazo zinatumika mahali pasipo na vumbi au tope kama barabara zenye lami mijini ambazo zinaweza kutumia muda mrefu zaidi.

Oili ikiwa imechoka kama ilivyokwisha kuelezwa hapo juu inafaa kubadilishwa. Mapendekezo ya mtengenezaji wa magari au mtambo lini oili ibadilishwe ni muhimu sana kuzingatiwa.

Mfano ufuatao unaonyesha kiwango cha utendaji wa oili, aina ya gari na umbali ambao inaweza kufanya kazi vizuri.

Mpemba na Muunguja, nani Mzanzibar?

HISTORIA ya Visiwa vya Unguja na Pemba imekuwa ni ya migogoro na migongano baina ya makundi yanayo tofautiana kwa asili, rangi ya ngozi, uchumi na kisiasa.

Katika makala hii Mwandishi Widimi Elinewiga wa DSJ, anajaribu kueleza juu ya migongano hiyo ya kihistoria visiwani humo.

Hakuna kundi lolote miongoni mwa wakazi wa Zanzibar linaloweza kudai kuwa ndilo wakazi wa asili katika visiwa hivi kwa sababu si wenyeji visiwani humo.

Karibu wakazi wote walihamia visiwani humo kutoka sehemu mbalimbali duniani. Wakazi hao walianza kufika katika Visiwa vya Zanzibar na Pemba kwa ajili ya kufanya biashara kuanzia Karne ya Kwanza.

Mwaka 110 baada ya Kristo(BK) msafiri mmmoja wa Kiingereza aliandika taarifa kuhusu biashara iliyoendeshwa kwenye Bahari ya Hindi iliyoitwa, The Periphis of the Erythrean Sea.

Wagiriki, Warumi na Waarabu ndio waliochangamkia biashara hiyo kwa karne nyingi. Bidhaa kama ngozi, pembe za ndovu na watumwa kutoka Afrika Mashariki, ziliwavutia wafanyabiashara kutoka China, India, Ujerumani, Misri na Arabia kuja kwenye ukanda na kuweka maskani yao Zanzibar ambapo awali palikuwa hapakaliwi na watu.

Zanzibar ndipo kilikuwa kituo kikuu cha biashara na hivyo, baadhi yao walibaki huko na kuanzisha makazi ya kudumu.

Wafanyabiashara toka Bara kwa kile kilichofahamika kama biashara ya masafa marefu, walipeleka bidhaa zao Pwani kuzibadilisha na bidhaa zingine. Makabila kama vile Wanyamwezi, Wayao, Wamanyema na Wakamba ndio waliokuwa wafanyabiashara toka Bara.Baharia wa Kiarabu, Ibin Batuta alipotembelea Zanzibar mwaka 1331, alikuta watu mchanganyiko waliokuwa na utamaduni tofauti baina ya wafanyabiashara toka Bara na wageni waliofika Zanzibar.

Matokeo yake, kizazi kipya kiliunda utamaduni mpya na lugha ya Kiswahili ndiyo iliyokuwa ikiwaunganisha kimawasiliano.

Kumbukumbu zinaonesha kwamba tangu mwanzo Zanzibar pamoja na kuwa mchanganyiko, walijali zaidi umoja na walikuwa tayari kusahau tofauti zao ili kulinda uhuru wao usivamiwe na kuharibiwa na watu toka mahali pengine.

Hata hivyo Waarabu walileta desturi haramu ya kumiliki na kuuza watu kama bidhaa (watumwa), kwa ajili ya kazi za majumbani na mashambani jambo ambalo lilikuza biashara ya utumwa.

Kutokana na kukua kwa biashara hiyo, Zanzibar kukawa na kituo kikuu cha biashara ya watumwa kutoka Bara.

Mahitaji makubwa ya watumwa wa Kiafrika huko Uarabuni, Uajemi, India na Visiwa vya Mauritius, yalikuza biashara hii na kuufanya mji wa Zanzibar kuwa maarufu kwa biashara hiyo.

Zanzibar pamoja na kuwa na soko kuu la biashara hii, ilikuwa pia na mashamba makubwa ya karafuu yanayohitaji nguvu kazi ya watumwa wa Kiafrika.

Misafara ya watumwa toka Bara ilileta maelfu ya watumwa wa Kiafrika visiwani Zanzibar na Pemba.

Kuongezeka kwa watumwa visiwani humo kilizusha migogoro kati ya Wazanzibari wenye asili ya Kiafrika, na wale wenye asili ya Kiarabu.

Mwaka 1897, wakoloni walitangaza uhuru wa watumwa, wakati huo, mtumwa alitakiwa kupeleka maombi kupitia mahakama ili kuachiwa huru.

Mwaka 1909 utumwa ulipigwa marufuku duniani. Ingawa utumwa huo ulitoweka lakini wale waliokuwa watumwa walijikuta hawana kazi na malazi. Hii ina maana kwamba, kundi lililokuwa kubwa la Waafrika ambalo ndilo lililokuwa la watumwa, lilijikuta linashikilia nafasi ya chini kabisa katika uchumi visiwani humo.

Uhasama baina ya makundi mbalimbali katika jamii ya Zanzibar ilichochewa na mkoloni ambaye aliwahudumia wananchi visiwani humo kiubaguzi kulingana na rangi ya ngozi zao.

Ubaguzi huu ulidhibitika wakati wa Vita Kuu ya Kwanza na ya Pili ambapo ugawaji wa chakula ulitolewa kulingana na asili ya mkazi. Pishi za mchele zilitolewa kwa Waarabu na Washirazi lakini Waafrika walikuwa wanaambulia pishi za unga wa dona.

Waarabu pia waliogawiwa unga wa ngano walipohitaji sembe, walipewa huku Waafrika wakikosa mgao huo. Kutokana na hali hiyo, vikundi vya siasa vilivyoanzishwa visiwani humo, vilichukua sura ya kibaguzi, kwani kulikuwa na vile vya Kiarabu na damu mchanganyiko na vile vya Kiafrika.

Mfano wa vyama hivyo, ni pamoja na Arab Association, Indian Association na Shiraz Association.

Vikundi hivi viliwakilishwa pia kwenye Baraza la Kutunga Sheria kwa kufuata rangi zao ambapo Waarabu na Wahindi walipewa nafasi zaidi. Jambo lilofanya Sultan apendekeze kufanyika kwa uchaguzi wa kuamua jinsi ya kujaza nafasi za wawakilishi.

Kufika mwaka 1956 vikundi hivi viligeuzwa kuwa vyama vya siasa, Waarabu waliunda Zanzibar Nationalist Party(ZNP).

Waafrika waliungana na kuunda chama cha Afro Shiraz Party (ASP) ambapo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1957, chama hicho kilipata ushindi mkubwa uliosababisha ghasia na mapambano kati ya Waarabu na Waafrika.

Wakati wa maandalizi ya kujitawala, iliazimiwa kwamba chama kitakachopata viti vingi katika uchaguzi, kitaruhusiwa kuunda serikali .

Kwa kuwahofia Waafrika kushinda, Waarabu waliwashawishi Washiraz kuunda chama cha tatu kilichoitwa Zanzibar and Pemba People’s Party(ZPPP) na katika uchaguzi mwingine uliofanyika Januari 1961, ASP ilipata viti 10. ZNP viti 9 na ZPPP viti 3.

Kutokana na matokeo hayo, jitihada za kuunda serikali zilishindikana wawakilishi wa ZPP walipogawanyika. Hivyo, ilibidi kuitisha uchaguzi mwingine mwezi Juni mwaka huo huo.

Ghasia, fujo na uchochezi kutoka nje vilitawala katika kipindi chote cha uchaguzi na watu 68 waliuawa na hali ya hatari kutangazwa. Katika uchaguzi huo Sultan alikula njama na serikali ya kikoloni ambayo ilimwezesha kuunda majimbo mengi zaidi sehemu zilizokuwa zikishikiliwa na Waarabu.

Kutokana na uchaguzi kuwa mbaya, ingawa ASP iliongoza kwa wingi wa kura ambapo ilipata viti 10 sawa na ZNP, ZPPP na ASP ilipokonywa ushindi wake.

Baada ya uchaguzi huo, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyekuwa Rais wa Tanganyika, aliilaumu Uingereza kwa kusema kwamba katika makoloni yake yote wakati wa kutoa uhuru, ilikabidhi madaraka kwa serikali ya walio wengi isipokuwa Zanzibar.

Matokeo ya uchaguzi huo hayakupokelewa na Waafrika walio wengi walikuwa chini ya ASP jambo lililo sababisha kupangwa kwa mapinduzi.

Mapinduzi hayo yalifanyika Januari 12 mwaka 1964 ili kuondoa tofauti za kisiasa na kiuchumi baina ya kundi la Waafrika walio wengi na Waarabu walio wachache.

Baada ya ushindi huo wa mapinduzi, kundi la Waafrika liliapa kamwe halitaruhusu tena visiwa hivyo vitawaliwe na watu wenye asili nyingine.

Maisha na Mikasa

MLOKOLE AELEZA ALIYOKUTANA NAYO KATIKA NDOA

Aliokoka baada ya kukatwa mkono, kiganja kikadondoka chini akakiona

lHivi sasa ana jicho moja, asema alidhani ni utani kumbe....

lAdai alisali miaka mitatu, mumewe akatolewa gerezani

lHawajakutana tena uso kwa uso

Benjamin Mwakibinga na Schola Nkondola

"Nilidhani sitapona na kwamba huo ndio ungekuwa mwisho wa maisha yangu hapa duniani lakini, Mungu ameniokoa; amenisaidia walau nitazidi kuwapo hivyo hivyo na kuendelea kuwa hapa duniani pamoaja na elemavu wangu si kitu."

Hayo ni maneno aliyoyasema Bi. Dora Elisongoya, kwa hali inayoonesha kutokuwa na matumaini mema wakati akisimulia juu ya mkasa mkubwa uliompata kwa waandishi wa mkasa huu.

Huku akiwa na furaha iliyochanganyika na huzuni, Bi. Dora anasema, "Kabla binadamu hujafa, hujaumbika. Hiyo nimeamini kwa kuwa saa yoyote, jambo lolote linaweza kukupata katika maisha yako hata ukawa kilema.

Bi. Dora anasema kuwa ulemavu alionao si kwamba umetokana na umbo lake la asili alilopewa na Mwenyezi Mungu, bali unatokana na shambulio alilolipata toka kwa mumewe aliyemtaja kwa jina la Goodrick Gabriel Materu.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 40 sasa, aliwaambia waandishi wa mkasa huu kuwa yeye na mumewe Bwana Materu waliishi maisha ya kawaida tu japo kwa muda wote wa miaka mitatu, hawakuwa wamejaliwa kupata watoto katika maisha yao.

Bi. Dora anaitaja tarehe 22 ya mwezi octoba mwaka 1992 kuwa ndiyo siku ambayo aliiona kama ni siku ya kiama kwa upande wake.

Mama huyo alisema jioni ya siku hiyo, alitoka akiwa yeye na mumewe; wakaenda kwa jirani yao aliyekuwa anauza pombe ili wapate kunywa kidogo ya kuwondolea uchovu baada ya mihangaiko ya kutwa nzima.

"Sasa pale wanapouza pombe, tukaendelea kunywa pombe huku tunazungumza yetu ya kawaida bila wasiwasi wowote. Si ni mtu na mumewe!" alisema Bi. Dora na kuongeza kuwa baadaye kidogo, mumewe akavua shati alilokuwa amevaa.

Baada ya kuona hivyo Bi. Dora akaamua kumsemea aache kuvua nguo hadharani na kama anajisikia kuzidiwa, basi warudi nyumbani.

Anasema alipoona mwenzake hamsikilizi, aliamua kuondoka na kurudi zake nyumbani kwake kwa kuwa hata muda nao ulikuwa umeshaanza kuisha na huku anatakiwa kuandaa chakula cha jioni.

Hata hivyo Bi. Dora anasema kuwa, haukupita muda mumewe naye akawa amefika hapo nyumbani kwao. Naye akaendelea na shughuli zake za kuandaa chakula mpaka alipomaliza.

Chakula kilipoletwa mezani Bi. Dora anasema, Bw. Materu alikataa kula na badala yake, akaamua kumtuma mtoto wa kazi (House girl) aende dukani kumnunulia sigara.

"Baada ya mtoto huyo kwenda dukani , basi, tukabaki sisi wawili. Sasa huyu mume wangu akaanza kuongea maneno mengi mengi juu yangu. Lakini mimi sikushituka wala kushangaa sana kwa kuwa ilikuwa ni tabia yake.

Hata mimi nilishamzoea , akirudi kutoka kwenye pombe zake, lazima maneno kama hayo yaanze. Sasa nikashangaa maana akawa anasema, KWANZA NIKIACHANA NA WEWE, HUTAPATA MTU WA KUKUPENDA, Mimi nikaendelea na shughuli zangu tu, kwa kuwa nilishamzoea. Sikuwa na wasiwasi kwa vile nilidhani ananitania tu, na hayo ni mambo ya pombe maana wanasema eti haina dreva na hata hivyo wanangu, (Waandishi) mimi nilikuwa nimeishamzoea."

Bi. Dora anaendelea kusimulia kuwa, "Mume wangu aliendelea kusema kuwa kama ningethubutu kujibu kitu, angenifanyia kitendo ambacho nisingekaa kukisahau katika maisha yangu.

Akaona hayo hayatoshi na mimi nimetulia, akasema waziwazi kuwa ataniua Tena anasema kwa hasira kali kabisa,‘nitakuuwa we mwanamke’.

Kwa upande wangu, sikuwa na hofu yoyote kuhusiana na maneno hayo aliyokuwa akiyasema mume wangu, na niliendelea kunyamaza kimya tu yeye aseme aliyo nayo, mpaka achoke.

Bi. Dora anaeleza kuwa akiwa bado, anasikiliza maneno hayo ya vitisho kutoka kwa Bw. Materu, aliyoendelea kuyaona na kudhani kuwa ni ya utani tu, mumewe naye akawa kama amenyamaza kidogo na kisha akatoka pale na kuingia ndani.

katika mazungumzo hayo na waandishi, Bi. Dora anasema hakujua mmewe akwenda kuchukua kitu gani ndani lakini, alishanga kumuona ametoka kwa hasira huku ameshikilia panga.

Kabla mtoto aliyetumwa dukani hajarejea bado, mume wangu alinisogelea huku ameshika panga mkononi mwake akasema, ‘Leo lazima nikuue.’,

Alizidi kunisogelea na huku akisema leo nakuua, nakuua leo! Yani nakusemesha unajidai kunyamaza? Tutaona sasa." akatulia kidogo, kisha akaendelea.

Nikashitukia anaanza kunipiga na panga kwa mara ya kwanza kichwani, nikiwa bado siamini kwa kuwa sijui nilifanya kosa gani, akanipiga panga lingine la kichwa", anaeleza Bi. Dora.

Kisha akasema kuwa, katika juhudi zake za kupambana na mmewe asiitumie sawia ile panga kama alivyokusudia kumchinja, ndipo wakati mwingine akawa anampiga kwa ubapa wa panga hilo na mara kadhaa, akamkata kichwani.

Anasema katika juhudi na mapambano hayo, mwanaume huyo aliambulia kumjeruhi kwa kumkata na kumjeruhi vibaya hata kumdhuru na kumfanyia chongo.

Huku akionesha makovu kadhaa ya majeraha yaliyotokana na kukatwa panga kichwani, Bi Dora aliwaambia waandishi hawa mkasa huu, "Oneni wanangu; oneni, alitaka kuniua kabisa.

Anasema kuwa, baada ya kupigwa mapanga mawili kichwani, alianguka chini na safari hii akawa anaelewa kuwa mumewe huyo hana tena utani, isipokuwa amedhamiria kufanya mauaji.

"Nikiwa bado nipo chini, akalenga panga lingine mara hii alitaka kunikata koo lakini hakufanikiwa isipokuwa panga hilo lilinijeruhi jicho la upande wa kulia nikiwa hata nashindwa kumuona maana damu nyingi zilinitoka na kufunika uso wote.

Jamani mume wangu huyu! Akachukua panga na kuning'ang'ania huku nikiwa chini maana niliona wazi anachotaka kwangu,ni kunikata koo lakini kwa uwezo wa Mungu, nikafanikiwa kumzuia.

hapo ndipo tulianza kupambana naye. Hata hivyo, sikumudu vizuri maana jicho langu moja lilikuwa likitoka damu nyingi na nilihisi maumivu makali. Si unaliona lilivyo mpaka sasa".(anaonesha jicho lake la kushoto lenye ulemavu).

"Tukiwa bado tunapambana, akafanikiwa kunikata kidevu changu" anasimulia Bi. Dora ambaye alama ya kukatwa katika kidevu chake inaonekana hadi sasa kwenye kidevu chake.

Ifuatayo ni sehemu tu, ya mazungumzo kati ya Bi. Dora na gazeti hili yalikuwa hivi,

Gazeti: Wakati mnapambana na Bw Materu hakukuwa na watu waliokuja kuwaamua?

Bi. Dora: Mmh! Hapakuwa na mtu kwa vile tulikuwa ndani na tena yeye mwenyewe (mumewe) alikuwa ameshika panga hivyo sidhani kama kuna jirani yeyote ambaye angeweza kusogelea hapo.

Gazeti: Wakati unaona anazidi kukushambulia kwa nini hukujihami kwa kukimbia wala kupiga kelele?.

Bi. Dora: Ningeweza kukimbia lakini nilikuwa nimeishiwa nguvu hivyo nilichoweza kufanya ni kumzuia kwa kutumia mikono tu.

Akiendelea kusimulia juu ya mkasa huo, Bi. Dora anasema kuwa mumewe aliendelea kumpiga mapanga katika maeneo mbalimbali ya mwili.

"Mume wangu aliendelea na nia yake ya kutaka kunikata shingo, akiwa amenilenga shingoni alinizua kwa mkono .

hata hivyo, matokeo ya kuuzuia, ni ghafla, nikashituka kipande cha mkono wangu ikiwa na kiganja kimekatika na kudondoka chini.

Nawambia sasa damu ilivuja kama maji na mimi nilijisikia kuwa katika dunia nyingine na hata sasa ninapokiona kipande hiki cha mkono,...Maumivu yalinizidi nguvu zikaniishia nikawa nagagaa chini, Mume wangu (Bwana Materu) hakuishia hapo akaamua kunikata mapanga mawili kichwani. Yeye alikuwa na nia ya kunimaliza kabisa.

Nikiwa bado sijitambui kabisa, mume wangu akakimbia . Kuanzia hapo nilipoteza fahamu hivyo nilijikuta na wala sikujua ni wakati gani nimefikishwa hospitalini."

Gazeti: Je, unaweza kukumbuka ni akina nani waliokufikisha hospitali?

Bi.Dora: Sikuwajua kwa kuwa ni baada ya muda mimi nilishitukia tu, niko hospitali ila tu ninawashukuru sana majirani zangu walionisaidia kwa huduma hiyo.

Gazeti: Ulikaa hospitalini hapo kwa muda gani na sijui ni akina nani waliokuhudumia ukiwa hapo hospitalini.?

Bi.Dora: Nilikuwa nahudumiwa na kupata msaada toka kwa ndugu na majirani na hasa mtoto wa dada yangu ndiye aliyenipa msaada na ndiye aliyenitunza mpaka hivi sasa.

Mwandishi: Vipi kuhusu mumeo huyo bwana ( Materu), baada ya tukio hilo yeye alifanya nini?.

Bi.Dora: Kipindi chote, mume huyo hakunihudumia lolote .Miezi mitatu mizima nilichokuwa ninatibiwa hapo hospitalini, sikumuona; ni watu wengine tu, ndio walikuwa wanahangaika na mimi. Yani hata sijui mmaskini mme wangu nilimkosea kitu gani.

Mwanamke huyo anaelezea kuwa mumewe hakuonekana kwa muda wa miezi tisa, baadaye polisi walifanikiwa kumkamata na akahukumiwa kwenda jela kwa muda miaka saba .

Baadaye mimi nikaruhusiwa kurudi nyumbani. Nikaenda kuishi kwa mwanangu (mtoto wa dada yake) katika kijiji cha Msalanga huko Moshi.

Nilipofika huko, aniliamua kuokoka ikiwa kama shukrani kwa Mungu ambaye alikuwa ameniponyesha na kuninusuru na kifo hicho.Siku hizi nimeokoka. ninasali Asemblizi (Kanisa la Tanzania Assembelies of God) huko Moshi katika kijiji cha Msalanga.

Bi. Dora aliendelea kusema kuwa, baada ya kumpokea Yesu maishani mwake ameamua kumsamehe mumewe kwa yale yote aliyomtendea na hivyo akaamua kufanya maombi maalum ili mumewe aachiliwe kutoka katika kifungo.

"Baada ya maombi hayo mume wangu akaachiwa huru miaka mitatu tu baada ya kuanza kutumikia adhabu aliyopewa na mahakama".

Bi. Dora anaongeza kuwa alimshukuru Mungu kwa kusikia maombi yake.

Gazeti hili lilizidi kutaka kujua zaidi, "Je unayaonaje maisha yako ya sasa baada ya kupata ulemavu huu. ?"

Bi.Dora akajibu akaendelea, "Naishi maisha ya kutaabika sana kwa vile nashindwa kufanya mambo mengi kwa kuwa hata yale niliyokuwa ninatambia kuyafanya kwa kujiamiani, sasa ninayafanya kwa tabu mno.

Mara nyingi mpaka nisaidiwe kama mtoto mdogo siwezi tena na kwamba maisha yangu ni ya kutegemea misaada tu, lakini ndiyo hivyo tena binadamu kabla hujafa hujaumbika" alisema Bi. Dora.

Hata hivyo Bi. Dora alisema mumewe huyo tangu aachiliwe huru hajawahi kuonana naye uso kwa uso na ikitokea wakaribia kuonana uso kwa uso, Bw Materu humshangaza kwa kukwepa na kumkimbia njiani ili wasionane.

Mama huyo aliwaambia waandishi wa mkasa huu kuwa sasa mumewe anaishi huko Old Moshi.Bi Dora anasema kwa sasa anahitaji msaada kutoka wa watu mbalimbali watakao kuwa na uwezo wa kumsaidia, na kwamba anatoa shukrani kwa wale wote waliomsaidia alipokuwa hospitali na wanaoendelea kumsaidia katika kuendesha maisha yake kwa kipindi hiki.

Mwanamama huyo alitoa wito kwa watu wenye uwezo, kuwasaidia wale wote wenye matatizo, "Tuwasaidie wenye matatizo kwa vile mambo hayo leo ni kwangu na kesho kwako" alisema.

Kwa wale watakaotaka kumsaidia Bi. Dora anaomba autume au awasiliane naye kupitia kwa anuani ifuatayo; Bi.Dora Elisongoya, c/o Michael Munishi, S.L.P 8235 . Moshi.